Baba Mtakatifu Francisko katika Katekesi yake kwa mahujaji na wageni , akiwa katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro,mapema Jumatano hii, alifungua ukurasa mpya, ambamo ameanza kuizungumzia huruma ya Mungu, akilenga moja kwa moja juu ya Utume wa Kristo katika kutimiza ahadi ya kumkomboa binadamu dhidi ya dhambi zake. Maelezo ya Papa yamesisitiza kwamba, huruma ya Mungu, inayoonekana kupitia kifo na Ufufuko wa mwanae Yesu Kristo Msalabani, haibagui mtu.
Baba Mtakatifu Francisko aliianza Katekesi akisema, baada ya kutafakari juu huruma ya Mungu katika Agano la Kale, sasa na tutafakari jinsi Yesu alivyotumwa na Baba yake kwa ajili ya kutimiza ahadi yake. Moja kwa moja amemtaja Yesu, kuwa ni huruma wa Mungu, iliyomwilishwa, kama anavyonekana katika utendaji wa maisha yake ya kila siku hapa duniani, alitangaza upendo, kukutana na watu, kuwaponya wagonjwa, kufariji wenye huzuni na kusahaulika , kusamehe dhambi n.k. Matendo ya Yesu yanaonyesha wazi kwamba alitenda kwa upendo mkuu usiokuwa na mipaka. Ulikuwa ni upendo safi, na ulio huru kabisa. Upendo uliofikia kilele chake katika kujitoa sadaka msalabani. Haya yote yanatuonyesha kwam ba kwa kweli Injili ni Neno la Huruma, kwa sababu Yesu mwenyewe ni Huruma.
Baba Mtakatifu ameendelea kuyatazama maisha ya Yeus tangu mwanzo akisema Yesu alianza utume wake kwa unyenyekevu , kama ilivyoandikwa katika Injili zote nne zikishuhudia kwamba, hata kabla ya kuanza huduma yake, kwa unyenyekevu alijiunga katika msatari wa kwenda kubatizwa na Yohana Mbatizaji. Hakujiweka kando kama mtu mkubwa na mwenye mamlaka, au mwenye kuhitaji huduma ya kipekee lakini alijichanganya na wengine kama mtu wa kawaida. Katika hili, Papa anasema , linaonyesha dhamira zima ya maamuzi ya Kristo. Unyenyekevu wa Yesu ulionekana hata wakati wa wakati wa kutolewa hekalu, aliwasilishwa kama mtu wa kawaida , bila mbwembwe za kutangazwa kwa sauti ya baragumu, au kujionyeshwa kama ni Hakimu Mkuu, mtu mashuhuri . Badala yake, aliishi kama mtu wa kawaida kwa miaka thelathini katika nchi yake ya Nazareth. Yesu alikwenda katika Mto Jordan, pamoja na watu wengi , akajipanga sambamba na wenye dhambi, ili abatizwe. Na hapo ndipo Baba wa Mbinguni alipomdhihirishwa kuwa ndiye Masihi, ishara ya Roho Mtakatifu aliyeonekana katika umbile ya njiwa juu yake na sauti kutoka mbinguni ikasema, ” Huyu ndiye Mwanangu, mpendwa; ninaye pendezwa nae”.
Papa amelitafakari tukio zima la fumbo hili kubwa la upendo wa Yesu, kwa kuutazama sana msalaba , ambako Yesu aliyatoa maisha yake sadaka kwa huruma ya kusafisha dhambi za dunia , dhambi zetu. Kutoka katika msalaba wake , Yesu anatuonyesha kwamba, hakuna anayebaguliwa katika Upendo wa huruma ya Mungu , kama alivyosema, ” Baba wasamehe maana hawajui watendalo”. Na hivyo kumbe juu ya msalaba wa Yesu, hakuna sababu za kuwa na hofu katika kutambua na kukiri dhambi zetu kwa sababu kila dhambi , kwa Sakramenti ya Upatanisho tunapata msamaha, unaotiririka toka msalabani na kutufanya upya kwa neema ya huruma yake, iliyotupatia sisi ushindi. Hatupaswi kuogopa dhambi zetu , kwa kuwa nguvu ya upendo wa Msulubiwa hajui vikwazo na kamwe haimwachi nje anayeiungamia.
Papa ameeleza na kutoa wito kwa watu wote kwamba, katika hii Jubilee hii ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu, ni wakati wa kukumbatia Injili kwa moyo wa shauku kubwa zaidi , nguvu ya Injili ya huruma yenye uwezo wa kuyabadili maisha yetu, nguvu inayotuwezesha kuingia ndani ya moyo wa Mungu, nguvu yenye kutuwezesha kutoa msamaha kwa wanaotukosea na kuitazama dunia kwa wema zaidi. Amehimiza , kwa kuikubali Injili ya Yesu Kristo Msulubiwa na Mfufuka, maisha yetu yote yanapata umbo jipya kwa nguvu ya upendo wake wenye kutubadilisha.
Baada ya Katekesi , Papa alisalimia makundi ya watu waliokuwa wakimsikiliza kulingana na lugha zao. Katika Kundi la wanaozungumza Kiingereza , walikuwepo mahujaji kutoka Kenya na Zimbabwe . Aliwaasa tukiwa bado katika kipindi cha maadhimisho ya Pasaka , na tuifungue mioyo yetu kwa Bwana Mfufuka ili kwamba kwa kuimarisha na neema zake , tuweze kwa pamoja na familia zetu na jumuiya zetu kushirikishana ujumbe wa Injili ya huruma yenye kutukomboa dhidi ya mizigo ya dhamb i. Mwisho kwao wote aliwapa baraka zake za Kipapa.
All the contents on this site are copyrighted ©. |