2016-04-06 07:08:00

Dr. Alberto Gasbarri atunukiwa tuzo ya heshima na Papa Francisko


Baba Mtakatifu Francisko amemtunukia nishani ya heshima ya utumishi uliotukuka Dr. Alberto Gasbarri, aliyekuwa mratibu wa hija za kitume za kipapa na mkurugenzi mkuu wa utawala Radio Vatican. Katika hotuba yake, ya shukrani kwa Dr. Gasbarri, Askofu mkuu  Angelo Becciu, katibu mkuu msaidizi wa Vatican amesema kwamba, nishani hii imetolewa na Baba Mtakatifu kwa kutambua ukweli na weledi uliomwilishwa na Dr. Gasbarri katika huduma yake mjini Vatican. Nishani hii ni changamoto ya kusonga mbele ili kuendelea kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia fursa hii kumshukuru kwa namna ya pekee Dr. Gasbarri aliyekuwa naye karibu katika safari zake. Tukio hili limeadhimishwa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, iliyoko mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Dr. Gasbarri ameitumikia Vatican kwa kipindi cha miaka 47. Ameng’atuka kutoka madarakani hapo tarehe 1 Machi 2016. Dr. Gasbarri alikuwa ni mtu maarufu sana, lakini mnyenyekevu, ndiye aliyeratibu hija zote za kichungaji zilizofanywa na Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko. Kabla ya kupewa dhamana hii, Dr. Gasbarri alikuwa ni msaidizi mkuu wa Kardinali Roberto Tucci kuanzia mwaka 1982 hadi mwaka 2005.

Hija za kitume zinazofanywa na Khalifa wa Mtakatifu Petro ni matukio makuu katika maisha na utume wa Makanisa mahalia. Hiki ni kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni matukio ya Ibada na mikutano mbali mbali inayopaswa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa, ili kupata matunda yanayokusudiwa. Hii ndiyo kazi aliyokuwa anatekeleza Dr. Gasbarri.

Baba Mtakatifu anamshukuru sana Dr. Gasbarri kwa majitoleo na sadaka yake kwa ajili ya huduma kwa Vatican na Kanisa katika ujumla wake. Nishani hii ya hali ya juu ni utambuzi wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Dr. Gasbarri aliyejitoa bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, hija za kimataifa zinafanikiwa kama ilivyopangwa. Dr. Gasbarri kwenye tukio hili la kutunukiwa tuzo ya heshima ya hali ya juu, ameongozana na familia yake. Hafla hii fupi imehudhuriwa pia na viongozi waandamizi kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican. Nishani hii ya hali ya juu inayotolewa na Vatican kwa watu maalum ilianzishwa na Papa Pio IX kunako mwaka 1847.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.