2016-04-05 08:01:00

Simameni kidete kupambana na rushwa na vitendo vya kigaidi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake mkuu, kwa kuwataka wananchi wa Nigeria kusimama kidete kupambana kufa na kupona na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram ambacho kimeendelea kuwa ni tishio kubwa la usalama, amani, utulivu na maendeleo nchini Nigeria. Umefika wakati kwa wananchi wa Nigeria kujifunga kibwebwe kupambana na rushwa pamoja na ufisadi mambo ambayo yanaendekezwa na kundi la watu wachache nchini humo, wakati ambapo kuna maelfu ya watu wanaoendelea kutumbukia na kuogelea katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato!

Ni wajibu wa Serikali kushirikiana na wadau mbali mbali katika kufanya maboresho ya hali ya maisha ya wananchi wengi wa Nigeria. Huu ni ushauri makini ambao umetolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika mkutano wao mkuu uliohitimishwa hivi karibuni! Vitendo vya kigaidi nchini Nigeria vimesababisha madhara makubwa katika maisha na maendeleo ya watu, hususan Kaskazini mwa Nigeria.

Maaskofu wanavipongeza vyombo vya ulinzi na usalama nchini Nigeria kwa kuendelea kupambana na Kikundi cha Boko Haram na kamwe wasikate tamaa, ushindi ni dhahiri, ikiwa kama kutakuwepo na utashi wa kisiasa. Inakadiriwa kwamba, zaidi ya watu laki tisa wamepoteza maisha yao na wengine wengi kujeruhiwa kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kufanywa na Boko Haram. Katika kipindi cha miaka kumi na mitano ya vurugu na mashambulizi ya kigaidi, zaidia ya Wakristo millioni 1. 3 wamelazimika kuyakimbia makazi yao na leo hii wengi wao wanaishi katika kambi za wakimbizi kana kwamba, hawana makwao! Jambo ambalo linasikitisha sana!

Maaskofu kutoka Nigeria wanaendelea kusema kwamba, Boko Haram wamechoma moto na kuharibu Makanisa zaidi elfu kumi na tatu nchini Nigeria. Wamesababisha hasara kubwa katika maisha ya watu. Uwepo wa Wakristo huko Kaskazini mwa Nigeria unaendelea kutiliwa mashaka kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Wakristo. Kuna maeneo mengine idadi ya Wakristo imeongezeka kwani wale wanaokimbia mashambulizi ya kidaidi wanapata hifadhi katika maeneo salama.

Changamoto kubwa ni mafungamano ya kijamii yanayotiswa kutokana na udini usiokuwa na mashiko wala mvuto. Wakristo na Waislam wanapaswa kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kutokana na changamoto na madhara yote haya, Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama havina budi kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, Boko Haram inashikishwa adabu; utawala wa sheria unarejeshwa, haki, amani na maridhiano kati ya wananchi wa Nigeria vinadumishwa.

Maaskofu Katoliki Nigeria wanazidi kufafanua kwamba, rushwa ni adui wa haki na maendeleo ya wengi. Rushwa inaharibu mzizi wa mafungamano ya kijamii, kiasi cha kuwanyima watu matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi; rushwa inawanyanyasa wanyonge na kuwakweza watu wachache ndani ya jamii. Mapambano ya rushwa hayana budi kwenda sanjari na maboresho ya maisha ya watu kwa kupambana na umaskini wa hali na kipato;  kwa kuboresha huduma za afya na elimu, ili hata watoto wa maskini waweze kuona mwanga katika maisha yao.

Mapambano ya rushwa na ufisadi yajengwe kwa kuimarisha misingi ya usawa, haki na mafao ya wengi. Serikali iwe ni mwelekeo mpana zaidi wa sera na mikakati yake ya kiuchumi badala ya kutegemea kwa kiasi kikubwa nishati ya mafuta kama chanzo kikuu cha pato la serikali. Wafanyabiashara wa kati na wadogo wadogo waendelee kusaidiwa ili kuimarisha shughuli zao za uzalishaji na utoaji wa huduma.

Maaskofu wanakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na Mwaka wa Upatanisho Barani Afrika, iwe ni nafasi ya toba na wongofu wa ndani; wakati wa kumwilisha kanuni maadili na utu wema; kwa kuwasaidia watu kiroho na kimwili pamoja na kujikita katika kutafuta mafao na ustawi wa wengi. Hapa kwa namna ya pekee, waamini wanahamasishwa: kutubu, kuongoka na kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.