2016-04-04 08:24:00

Mabomu ya kutegwa ardhini yana madhara makubwa!


Udhibiti wa mabomu ya kutegwa ardhini ni kitendo cha kibinadamu, ndiyo kauli inayoongoza maadhimisho ya Siku ya Kumi na Moja Ya Kimataifa ya Kudhibiti Mabomu ya kutegwa ardhini, inayoadhimishwa na Umoja wa Mataifa tarehe 4 Aprili 2016. Madhara ya vita ni makubwa kwa watu si tu wakati hata baada ya vita kwani mabomu ya kutegwa ardhini ni hatari sana kwa ulinzi na usalama wa raia.

Bwana Ban Ki-Moon, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa katika ujumbe wake kwa maadhimisho haya anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutoa jibu makini kutokana na changamoto hii na kwamba, kuna haja ya kuwekeza katika misingi ya utu wema, ili kukoleza mchakato wa jamii kuishi kwa amani, upendo na mshikamano. Katika jamii kama hii, wahitaji wanaweza kupata msaada wa hali na mali wanaouhitaji; ulinzi na usalama vitaimarishwa; watoto watapata nafasi ya kwenda shule na kufurahia maisha yao. Mambo haya ni muhimu sana katika kuweka msingi wa amani ya kudumu!

Madhara ya mabomu ya kutegwa ardhini ni kati ya ajenda zitakazojadiliwa kwenye Mkutano wa kwanza wa Kimataifa kwa ajili ya ubinadamu, utakaofanyika huko Instanbul, Uturuki, mwanzoni mwa mwezi Mei, 2016. Wajumbe watapembua kwa kina na mapana madhara ya mabomu ya kutegwa ardhini katika maisha  ya watu na kwamba, kuna haja ya kuheshimu na kuzingatia sheria za kimataifa pamoja na itifaki zilizotiwa sahihi na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.