2016-04-04 10:31:00

Injili ya huruma ya Mungu!


Mapadre waungamishaji wanapaswa kuonesha ile sura ya huruma na upendo wa Mungu kwa wadhambi wanaokwenda kutubu ili kumwongokea Mungu katika hija ya maisha yao, ili kweli waweze kujisikia kwamba, Mwenyezi Mungu anawakaribisha, ili kuwapatia tena nafasi ya kuweza kupyaisha maisha yao! Hii ni changamoto ambayo imetolewa hivi karibuni na  Monsinyo Krzysztof  Nykiel, afisa mwanadamizi kutoka katika Baraza la Toba ya Kitume, wakati wa kuhitimisha kongamano lililokuwa linajadili kwa kina na mapana Waraka wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, yaani Uso wa huruma, “Misericordiae vultus”.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kukimbilia tena na tena katika kiti cha huruma ya Mungu tayari kuomba na kuambata huruma ya Mungu, inayowapatia nafasi ya kupyaisha maisha yao! Kumbe, dhamana ya Padre muungamishaji ni muhimu sana, ili kuhakikisha kwamba, waamini hawa wanapata tiba ya uhakika katika mahangaiko yao ya ndani.

Monsinyo Nykiel anakaza kusema, mwaka huu, waamini wengi wamegundua ndani mwao umuhimu wa Sakramenti ya Upatanisho inayowakirimia huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahamasisha Mapadre kuwa mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu na wala si mahakimu wakatili; waamini nao waoneshe jitihada za kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu! Mapadre waungamishaji wawe na huruma na upendo kama katika mfano wa Baba mwenye huruma anavyosimliwa katika Injili.

Muungamishaji ni chombo cha kupokea na kubariki matunda ya toba na wongofu wa ndani, mbegu iliyopandikizwa na Mungu mwenyewe! Mungu ndiye chanzo cha maisha mapya, ndiyo maana Baba Mtakatifu anawataka Mapadre kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu; wawe tayari kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza ili kuwapatia watu huruma ya Baba wa milele! Katika kongamano hili, washiriki wameonja kwa namna ya pekee jinsi ambavyo huruma ni kiini cha Habari Njema ya wokovu. Kwa hakika waamini wanaalikwa kuimba  Zaburi ya shukrani kwa kusema “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.

Huruma ya Mungu inaonesha jinsi ambavyo Mungu anavyopenda kuendeleza maisha ya mdhambi kwa kumpatia nafasi ya kutubu na kumwongokea! Yesu ndiye huruma ya Baba wa milele, aliyeshuhudia nguvu ya huruma ya Mungu katika maisha na utume wake. Kanisa ni Mama wa huruma ya Mungu, Sakramenti ya wokovu na chemchemi ya mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu. 

Itakumbukwa kwamba, Kardinali Mauro Piacenza, mwanzoni mwa kongamano hili, alifafanua kwa kina na mapana kuhusu huruma ya Mungu inayobubujika kutoka kwenye Moyo Mtakatifu wa Yesu anayelijenga na kulitegemeza Kanisa lake kwa njia ya Sakramenti mbali mbali, ili kuendeleza ile kazi ya ukombozi ambayo ilianzishwa na Kristo mwenyewe. Kumbe, maisha na utume wa Kanisa unajikita katika huruma ya Mungu!

Kanisa linatumwa kutangaza, lakini zaidi kushuhudia huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Ufanisi wa Kanisa unapimwa kutokana na kujikita katika utangazaji wa huruma ya Mungu ambayo imefunuliwa kwa njia ya Yesu Kristo. Hivi ndivyo anavyosema Padre Laurent Touze wakati akichangia mada kwenye kongamano la Uso wa huruma ya Mungu. Mwamini anapokimbilia kwenye kiti cha toba anasamehewa dhambi zake na kulipokea Fumbo la Utatu Mtakatifu na huo ni mwanzo wa maisha mapya yanayojikita katika toba na wongofu wa ndani; msamaha, haki na huruma; waamini wanapaswa kuwashirikisha jirani zao tunu hizi katika maisha!

Upendo wa Mungu wadumu milele na kamwe hauwezi kuzimishwa kutokana na dhambi zinazotendwa na wanadamu. Huruma ya Mungu inamkumbusha mwamini asili yake ya wema na utakatifu; inawawezesha waamini kupyaisha maisha yao ili kufunga Agano na Mwenyezi Mungu. Huruma ya Mungu inamkumbusha mwamini kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, heri wenye rehema maana hao watapata rehema.

Padre Antonio Sicari kwa upande wake amesema, huruma ya Mungu inawasukuma waamini kuwa na huruma, kama ilivyojionesha kwa Watakatifu mashuhuda wa huruma ya Mungu kama vile: Theresa wa Mtoto Yesu, Mama Theresa wa Calcutta, Sr. Faustina Kowalska, Vincenti wa Paulo, Damiano  De Veuster, Leopoldo Mandic. Kanisa katika maisha na utume wake, limekuwa daima mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, dhamana inayopaswa kuendelezwa kwa ari na moyo mkuu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.