2016-04-03 13:39:00

Yaliyojiri katika mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni tarehe 2 Aprili 2016 ameongoza Ibada ya Mkesha kwa ajili ya maadhimisho ya Jumapili ya huruma ya Mungu iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, ili kuwawezesha waamini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwani hili ni hitaji msingi kwa watu wa nyakati hizi. Mkesha wa sala ulijikita katika Neno la Mungu, ukimya, tafakari na sala kwa ajili ya mahitaji mbali mbali ya Kanisa pamoja na kusali Rozari ya huruma ya Mungu.

Mkesha huu wa sala uligawanyika katika sehemu kuu tano za Ibada! Baada ya kusoma Neno la Mungu, tafakari na sala; waamini waliwaombea viongozi wa Kanisa: Baba Mtakatifu Francisko; Wakleri, watawa na wahudumu wote wa Neno la Mungu. Tafakari iliyotolewa ilikuwa ni Mkesha wa Jumamosi kuu, dunia ilipokumbwa na kimya kikuu, ikafunikwa na giza nene, tayari kutoka, ili kushuhudia mwanga wa Kristo Mfufuka!

Sehemu ya Pili ilijikita katika Neno la Mungu, ukimya na tafakari! Mahubiri yaliyotumiwa ni yale yaliyotolewa na Mtakatifu Gregory wa Nazianzi kuhusu upendo kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini wamesali na kuwakumbuka Wakristo wanaodhulumiwa na kuuwawa sehemu mbali mbali za dunia. Kanisa limewakumbuka waamini waliolegea katika imani yao; wale waliopoteza matumaini; wakristo wasiofahamu kupenda bila kuwasahau wale waliopotea, wakakengeuka na hatimaye, kumezwa na malimwengu!

Sehemu ya tatu; baada ya Neno la Mungu, ilisomwa sehemu ya Waraka wa Mtakatifu Yohane Paulo II kuhusu huruma ya Mungu, Dives in misericordia, kwa kukazia kwamba, Yesu Kristo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa Baba wa milele. Kanisa limeombea huruma kwa ajili ya familia, ili wanandoa waweze kudumu katika maagano na uelewano. Kanisa limewakumbuka watoto wanaoteseka na kunyanyasika; wamewakumbuka na kuwaombea vijana ili waweze kuwa na matumaini. Kanisa limewaombea pia wazee wanaoteseka kwa sababu mbali mbali.

Sehemu ya nne, baada ya Neno na Tafakari; waamini waliwaombea wakristo wanaogelea katika lindi la dhambi na mauti; watu wasioamini; wagomvi, watu wanaowanyanyasa wengine bila kuwasahau wale ambao utu na heshima yao vimewekwa rehani! Ilisomwa pia tafakari ya Massimo muungama imani aliyekazia umuhimu wa wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho; toba na wongofu wa ndani, mwaliko wa kumjifunza Kristo ambaye ni mpole na mnyenyekevu wa moyo!

Sehemu ya tano, Neno la Mungu na tafakari vilisomwa na hatimaye, waamini wakatafakari kuhusu huruma ya Mungu kutoka katika shajara ya Mtakatifu Faustina Kowalska anayemwomba Kristo Yesu, amkirimie neema ya kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa jirani zake! Waamini wamesali na kuwaombea wanaoteseka na kuhuzunika; watu wanaonyanyaswa na kunyonywa; wakimbizi na wahamiaji; watu wapweke na wale waliotelekezwa na ndugu na jamaa zao, mwishoni Kanisa limewakumbuka na kuwaombea huruma ya Mungu wagonjwa na wale walioko kufani! Baada ya Injili, Baba Mtakatifu Francisko aliyoa mahubiri yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.