2016-04-03 09:50:00

Mh. Padre Tanzi ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Isangi, DRC!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Dieudonnè Madrapile Tanzi, kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Isangi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo. Askofu mteule alizaliwa tarehe 18 Agosti 1958 Jimboni Isiro-Niangara. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kipadre, tarehe 25 Agosti 1985 akapewa Daraja Takatifu la Upadre.

Katika maisha na utume wake kama Padre, amewahi kuwa mlezi, Seminari ndigi ya Rungu na baadaye akateuliwa kuwa ni Baba wa maisha ya kiroho, Seminari kuu ya Falsafa ya Mtakatifu Agostini, Kisangani. Alikwishawahi kuteuliwa kuwa ni Makamu Askofu na Msimamizi wa kitume Jimbo Katoliki la Isiro – Niangara. Kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2006 alikuwa ni Msimamizi mkuu wa Madhabahu ya Mwenyeheri Anuarite.

Baadaye akapelekwa Roma kwa ajili ya masomo ya juu na hatimaye kujipatia shahada ya uzamivu kuhusu Umissionari wa Kanisa. Akiwa Roma kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2013 alitoa huduma za kichungaji kwa Watawa wa Don Guanella. Kuanzia mwaka 2012 amekuwa akifundisha pia Chuo kikuu cha kipapa cha Urbaniana, kilichoko mjini Roma kwa mwaliko maalum!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.