2016-04-02 14:02:00

Onesha kitambulisho chako!


Kwa kawaida mwanachama wa chama au kikundi chochote kile anakuwa na kitambulisho maalumu na anaona fahari kutangaza sera za chama au za kikundi chake. Leo tutakiona kitambulisho cha Kristu mfufuka anachotakiwa kukivaa mfuasi wake. Injili ya leo inaeleza awamu mbili ambazo Yesu mfufuka anakutana na wanafunzi wake. Awamu ya kwanza ilikuwa jioni ya siku ile aliyofufuka (Jumapili), “Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu ya Wayahudi.” Awamu ya pili ilikuwa siku nane baadaye. Katika awamu zote mbili kikundi hiki kidogo cha wanafunzi kilijitenga na kujifungia ndani ya chumba kwa hofu ya Wayahudi.

Mandhari hii inawakilisha hali halisi ya mahusiano yaliyoko kati ya vyama na vikundi vingi, ambapo wanachama wake hujifungia katika ulimwengu wa itikadi zao tu na kuwaogopa walio nje kama wapinzani.  Hapo inazuka hofu inayomgeuza mtu hadi kuwa wa siasa kali, yaani kukereketwa kunapitiliza mipaka. Kama mkereketwa huyo ni mkristo basi atajifungia katika akili na utashi wake bila kutaka majadiliano na yeyote asiyefuata itikadi za dini yake. Mtu wa aina hiyo atanadisha sera za imani yake kwa kupandisha majini na kupaza sauti, hata kuwadhulumu wengine. Hizo ni alama wazi za hofu iliopitiliza.

Katika historia ya Ukristo, kumewahi kuwa na vipindi vya hofu kama hiyo. Kumekuwa na hofu ya elimu ya sayansi, kwamba ingeweza kuharibu imani ya kikristo. Kadhalika hofu ya elimu ya mambo ya kale na teknolojia hasa ya nadharia ya mvuvumko iliyoonekana kupingana na nadharia ya uumbaji. Kanisa likahofu kuwa ulimwengu huo ungeangamiza na kuharibu dini ya kikristo. Kumbe mkristo hatakiwi kuuhofu ukweli, kwani akili ya binadamu imeumbwa na Mungu ili kuujua na kutafuta ukweli. Yesu alitangaza Injili ya ukweli na akataka ukweli wa Injili uenee ulimwenguni.“Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” (Yoh 8:30-31).

Kujitenga na kujifungia ndani ni hofu itokanayo na kutojua kitambulisho cha Yesu Kristo mfufuka. Hofu iliyosababishwa na kutomjua Kristo mfufuka kwamba maisha yake ya upendo na huruma yasingeweza kufa tu basi, bali yanadumu milele. Katika mazingira ya hofu, Yesu ajitokeza katikati ya wanafunzi wake na kuwaonesha kitambulisho vyake. “Akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake.” Kitambulisho cha mfufuka ni mikono na ubavu wake. Mikono iliyotobolewa misumari na kusulubiwa ni alama ya nguvu. “Mkono wa kuume wa Bwana umetenda makuu.” (Zab 118:15).

Kwa hiyo, Yesu anaonesha mikono aliyotumia kutenda matendo ya huruma kama vile kuwaponya wakoma, kuwaponya vipofu na viziwi, kumwokoa Petro alipotaka kuzama majini, kuwabeba watoto, mikono iliyoosha miguu ya mitume nk. Kitambulisho hiki cha Yesu chatakiwa kiwe cha kila mbatizwa, yaani kutumikia na kutenda matendo ya huruma. Kadhalika ubavuni ilikotoka damu na maji baada ya kuchomwa moyo uliojaa upendo na huruma. Mkristo asukumwe na moyo wa huruma na upendo katika kutumikia na kutenda mema.

Mapato ya Yesu kuwa katikati yao,“Wanafunzi walifurahi kumwona Bwana.” Hapa wanafunzi wanayo furaha ya kweli anapokutana na kuona kuona vitambulisho vya aliyetoa maisha yake kwa ajili wengine. Hivi wafuasi wa Kristu wanafurahi kukutana na yule anayefahamu uzuri wa kutoa maisha kwa ajili ya wengine. Baada ya kufurahiana huko, Yesu anawaingiza wanafunzi wake katika ufuasi.“Yesu anawatuma mitume wake akasema: Kama Baba alivyonituma mimi nami nawatuma ninyi. Kisha akawavuvia na kusema: Pokeeni roho mtakatifu.” Kuvuvia ni kuingiza roho, yaani kutia nguvu ya Mungu ndani ya mitume. Zawadi ya nguvu za Mungu iliyomfanya Yesu kuleta maisha duniani sasa wanashirikishwa wote na kutumwa kwenda ulimwenguni bila hofu kama kondoo kati ya mbwa mwitu. Wanaagizwa, “Wowote mtakaowasamehe wamesahemewa, wale mtakaowafungia watakuwa wamefungiwa” yaani kila mmoja anao wajibu wa kuwatoa watu toka njia mbovu ya dhambi na kuwaongoza katika njia iliyo sawa inayoelekea kwenye utakatifu wa maisha!

Baada ya mitume kuingizwa uanachama wa kundi la Kristu, sasa awamu ya pili inahusu kupewa vitambulisho wafuasi wengine tuliobaki. Ndiyo maana katika awamu hii tunaambiwa ilikuwa ni siku nane baadaye. Maana yake siku ya kwanza baada ya kwisha siku saba rasmi za uumbaji, Sasa hufuata maisha ya kawaida ya binadamu. Sisi waanzaji wenye mashaka tunawakilishwa na Tomaso. “Baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso aitwaye Pacha pamoja nao. Akaja Yesu, na milango imefungwa, akasimama katikati yao.” 

Tomaso anaitwa Pacha (Didimo) maana yake mawingu. Kwa hiyo huo ni mwito kwetu wa kujitambua kuwa ni mawingi au pacha wa Tomaso. Tunafanana na Tomaso katika mahusiano yetu na Yesu. Yaonekana Tomaso hakuuogopa ulimwengu kama wale mitume waliojifungia chumbani. Aidha isieleweke kwamba alikuwa mpinzani na Yesu. Tomaso hakuwa mpinzani wala hakuwa na hofu ya Wayahudi bali alipeta tu nje. Lakini kwa vyovyote alifanana na mitume katika kuona mashaka juu ya ufufuko. Hali ambayo mara nyingi Yesu anawagombeza mitume kwa kutokusadiki kwao (Marko). Tomaso alianza kulifanya kosa hilo kwa kujitenga na jumuiya yake. Hivyo ndivyo inavyotokea katika maisha ya kila siku katika vikundi mbalimbali.

Hebu tuone ni katika kipengele gani mkristu ni mawingi au pacha, yaani analingana na kutokulingana na Tomaso aitwaye Pacha (Didimo). Pacha asiyelingana na Tomaso Didimo ni yule aliyejitenga na jumuiya yake na kuwadharau wote waliomo humo kuwa hawafai. Huyo ni sawa na anayehama chama cha siasa na kukidharau wakati kimlea na kumkuza hadi kufikia ujiko alionao kwa sasa!. Mwanachama wa kweli ni yule anayebaki imara katika chama hata kama baadhi ya wanajumuyia wake wana makwazo, kwa sababu kuna sera na mambo mema yaliyomo humo; ni mtu anayethubutu kuleta mageuzi kwa kubaki ndani ya chama!

Ndivyo inavyotokea katika Ukristo, kuna wale wanaoasi dini na kujiunga na dini nyingine kwa sababu tu wanajisikia kukatishwa tamaa kutokana na makwazo yanayofanyika humo, kama vile mfumo mbovu wa uongozi, utajiri uliokithiri au kanisa kushindwa kutoa majibu sahihi kwa maswali na shida mbalimbali za waamini. Kumbe, pacha anayelingana na Tomaso ni yule baada ya kuona makwazo hayo, hata kama anashawishika kujitenga na ukristu kwa muda ili kuona ukweli utakaoibuka kutokana na muda unavyopita lakini anarudi tena. Mtu huyo anafanana na yule anayekwepa moshi ili kuweza kuona vizuri ukweli ulipo.

Tomaso hakuasi kundi, ndiyo maana anarudi kundini kuhakikisha kwa akili yake kama upepo umebadilika. Hapo ndipo anapokosa imani pale anapotaka kuuelewa tena kwa kugusa ufufuko wa Kristo. Ufufuko wa wafu hauwezi kufahamika kwa akili ya kibinadamu. Tomaso hakufahamu kwamba binadamu tunayo mang’amuzi ya kimwili tu, kumbe ukweli na mang’amuzi yaliyo ndani ya kaburi unajulikana na yule tu aliye ndani ya vuguvugu zake, yaani mfu peke yake kwani “Adhabu ya kaburi aijuaye maiti.” Kumbe siri ya kaburi anaijua Yesu peke yake mwenye mang’amuzi ya ya kufa na kufufuka. Kwa njia ya Mungu peke yake binadamu tunaweza kuuelewa ufufuko.

Kwa hiyo Pacha wetu Tomaso kama binadamu asingeweza kupata jibu alilolitegemea. Ndiyo maana Kristo mfufuka akamtaka asiendelee kutosadiki bali awe na imani na kusadiki. “Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona wakasadiki.” Mapato yake, Tomaso akabaki tu kuinamisha kichwa na kusema: “Bwana wangu na Mungu wangu.” Inatosha kwetu kujua kwamba kitambulisho cha mfuasi wa kweli wa Kristo Mfufuka ni mikono inayohudumia na moyo (ubavu) alama ya upendo. Leo tunafundisha kutafakari fumbo hili la ufufuko tunapotenda matendo ya huruma. Tunapokuwa na mashaka tumwige pacha wetu Tomaso na kusali: “Bwana wangu na Mungu wangu.”

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.