2016-04-02 12:19:00

Huruma ya Mungu inamwilishwa katika maisha ya kila siku!


Mpendwa msikilizaji wa kipindi cha Hazina Yetu, Tumsifu Yesu Kristo na heri na baraka tele kwa sherehe za Pasaka ya Bwana. Tukingalimo shagweni humu mwa Paska, tunapenda kuendelea kutafakari nawe mpendwa msikilizaji juu ya sauti ya huruma ya Mungu ambayo kwa wakati wote wa Kwaresma  Mama Kanisa alipenda tushirikishwe kwa namna ya pekee zaidi. Bado Mama Kanisa anatualika sote kuendelea kuimwilisha huruma hiyo ya Mungu katika maisha baada ya Pasaka.

Tutakumbuka kwamba wakati wa kwaresma, kwa msaada wa Neno la Mungu na mafundisho mbalimbali ya wachungaji wetu, tulialikwa kuuambata wongofu na hivyo kufungua kurasa mpya za maisha yetu. Na sasa baada ya Pasaka tunajibidisha kwa msaada wa huruma ileile ya Mungu kuandika ukurasa mpya wa maisha yetu ya Kikristo. Tunaalikwa kuchochea zaidi maisha adili ya fadhili. Kukuza zaidi imani, matumaini na mapendo yetu kwa Mungu na jirani.

Tunaalikwa kukuza fadhili mbalimbali zinazo upambanua Ukristo wetu kwa mwonekano wa kufaa zaidi; yaani kuwa watu wenye huruma, upole, uaminifu, kiasi, bidii njema, wenye haki na wenye kujibidisha katika kutafuta na kutunza amani ambayo ni zawadi ya kwanza kabisa ya Kristo Mfufuka kwa mitume wake.

Mpendwa msikilizaji, baada ya kuzipokea baraka hizo za Pasaka, sote tunajawa na hamu ya kutaka kuiishi huruma ya Mungu kwa upeo mtimilifu. Lakini huruma hiyo ya Mungu ili itusindikize katika maisha yetu na itufaidie vilivyo; tunahitaji kushiriki kikamilifu; yaani kuwa tayari kushirikiana na huruma ya Mungu inayokuja kwetu kwa njia mbalimbali. Ili kutekeleza hilo ndugu yangu, tunahitaji mapinduzi ya fikra. Namna yetu ya kufikiri iwe ni ile ya kujitakia mema sisi wenyewe na kuwatakia mema wengine pia.

Tutaukubali ukweli kwamba, namna mtu anavyo ishi, hutokana zaidi na namna yake ya kufikiri; ambayo humpelekea katika namna fulani ya kutenda mambo. Kwa mtazamo huo, tunaamini kwamba, tukiwa na jicho chanya kwa watu na mitaala mbalimbali ya maisha ya watu adili; tutangundua kuwa kuna milango mingi sana ya huruma ya Mungu.

Na hii ni moja ya vinasaba vya Hekima kuu ya Mungu wetu. Yaani, Mungu huweza kutuelekezea huruma yake, hata kupitia katika mazingira tatanishi, au kupitia kwa watu ambao hawakubaliki katika jamii. Mungu pia anaweza kukupelekea huruma na msaada wake kupitia watu ambao wewe hupapendi kabisa. Ukidumu katika fikra hasi, utajifungia katika undani wako na kuifungia nje huruma ya Mungu.

Hilo linadhihirika pia hata katika Maandiko Matakatifu. Mungu alipokuwa anatekeleza mpango wa ukombozi, anawakomboa taifa la Israeli kutoka utumwani Misri; kabla ya kuvuka mto Yordani walitumwa wapelelezi kwenda kuipeleleza nchi watakayoiingia. Kwa sababu waligundulika kuwa ni wageni, usalama wao ukawa shakani. Lakini Mungu aliwaokoa kupitia Kahaba mmoja aliyeitwa Rahabu. Naye mama huyu kwa hekima na upendo mkubwa, akawasalimisha wapelelezi wale kwa kuwatorosha kupitia dirishani. (Rej. Yosh 2).

Na baadaye kwa huruma hiyohiyo ya Mungu, waana wa Israeli walimfanyia hisani mama huyu, wakamchukua kwao, na hivyo kuiacha kabisa kazi aliyokuwa akiifanya na akawa mmoja katika familia ya Waisraeli. Kama haitoshi, Mungu wa huruma akamfanya mama huyu Rahabu, kuwa mmoja kati ya wazazi wanaotajwa katika Orodha ya Ukoo wa Yesu kama tusomavyo “Salmoni alimzaa Boazi kwa Rahabu” (Mt. 1:5). Si hivyo tu, katika orodha hiyo hiyo ya Ukoo wa Yesu tunamkuta pia Solomon mwana wa Daudi, aliyemzaa kwa yule mke wa Uria (Mt. 1:6), pia tunawakuta Feresi na Zera, ambao Yuda aliwazaa kwa Tamar.

Kwa mtazamo wa kidunia hapa unaweza kuuliza swali, mbona kuna mazingira potofu kimaadili ya kuzaliwa kwa hawa watu; inakuwaje wapo katika Ukoo wa Kimasiya? Kwa nini Mungu amependa mstari wa kimasiya upitie kwa watu hao?

Hapo ndipo tutakaposhangazwa na huruma kuu ya Mungu, na hiyo ni tabia ya huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu huwaokoa wote, huwafariji wote, huwakusanya wote. Huruma ya Mungu hudhihirika hata katika mazingira, matukio na watu wasipoeleweka kirahisi kwa akili ya Mwanadamu. Na ndiyo maana ni huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu hutakasa, huinua, huoko, hubadilisha kabisa. Hivyo usiachwe kinywa na usijawe na shaka unapomwona mtu mwovu kabisa anatenda matendo mema ya upendo. Unapomwona mtu asiyefaa kijamii ananena hekima, mtu mwenye kuleta hofu na wasiwasi, analeta faraja, matumaini na amani. Ndivyo Mungu atendavyo kazi. Hutumia hata viumbe dhaifu ili kufikisha wema wake kwa viumbe wake.

Hivyo mpendwa msikilizaji, utaweza kushuhudia katika maisha kwamba, kuna watu ambao huwapendi wala kuwatakia mema, lakini hao ndio waliokusaidia sana na pengine wanakuombea daima. Kuna mazingira ambao hayapendezi kabisa, lakini Mungu akainua neema zake. Ni mwaliko kwetu sote, kuwa vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wote. Na tena kuwa tayari kupokea huruma na wema wa Mungu unaotujia kutoka kwa wenzetu; na zaidi kukubali kutumwa na kutumika na Mungu ili kuwafikishia watu wake wema, huruma na upendo wake. Mwisho tutasema wote “Yote yametendwa na Bwana…nayo ni ajabu machoni petu”.

Pokea wingi wa baraka na heri ya Pasaka kutoka Studio za Radio Vatican. Kukuletea makala hii ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.