2016-04-01 15:34:00

Kardinali George Cottier amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 93


Baba Mtakatifu Francisko ametuma salam za rambi rambi kwa Mama Marie Emmanuel Pastore Cottier,  kufuatia kifo cha Kardinali George Cottier aliyefariki dunia akiwa na umari wa miaka 93! Baba Mtakatifu anasema ameguswa sana na taarifa za kifo cha Kardinali Cottier na anapenda kuungana na wale wote wanaoomboleza msiba huu mzito wa Mtumishi mwaminifu wa Injili. Baba Mtakatifu anamkumbuka Marehemu Kardinali Cottier kutokana na imani yake thabiti, upendo wa kibaba na umakini wake katika shughuli za kitamaduni na kikanisa, hasa kwa kutoa huduma makini kwa Mtakatifu Yohane Paulo II na Benedikto XVI kama mwanataalimungu wa nyumba ya kipapa.

Baba Mtakatifu anapenda kumwombea Marehemu Kardinali Cottier huruma ya Mungu kwa maombezi ya Bikira Maria na ya Mtakatifu Dominiko, ili aweze kupata tuzo ambalo Kristo aliwaahidia watumishi wake waaminifu. Baba Mtakatifu amewapatia baraka zake za kitume wale wote walioguswa na msiba huu kutokana na huduma yake ya Kipadre na kwa viongozi wakuu wa Kanisa katika ujumla wao!

WASIFU WA MAREHEMU KARDINALI COTTIER

Kardinali Georges Marie Martin Cottier, OP. Mwanataalimungu mstaafu wa nyumba ya Kipapa amefariki dunia katika usiku wa kuamkia tarehe 1 Aprili 2016 kwenye Hospitali ya Gemelli alikokuwa amelazwa. Ibada ya Misa ya mazishi itaadhimishwa Jumamosi tarehe 2 Aprili, 2016 majira ya saa 2: 30 za asubuhi kwa saa za Ulaya na kuongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali.

Itakumbukwa kwamba, Marehemu Kardinali Cottier alizaliwa tarehe 25 Aprili 1922, huko Geneva, Uswiss. Kardinali Cottier alijiunga na Shirika la Wadominikani kunako mwaka 1945 na kujipatia masomo yake kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Thoma wa Akwino, maarufu kama Angelicum hadi mwaka 1952. Tarehe 2 Julai 1951 akapewa Daraja Takatifu la Upadre.

Baada ya kurejea nchini Uswiss, Kardinali Cottier alijiendeleza zaidi na kuanzia Mwaka 1962 akawa ni jaalim na baadaye mkuu wa Kitivo cha Fasihi Andishi kwenye Chuo kikuu cha Frbourg. Amefundisha kwa nyakati mbali mbali kwenye Vyuo vikuu vya Montreal, Canada, Chuo kikuu cha Kikatoliki, Paris, Ufaransa; Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Moyo Mtakatifu wa Yesu, Milano, Italia. Alishiriki katika maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kama mtaalam. Alikuwa pia mjumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya majadiliano na wale wasioamini.

Kunako mwaka 1986 akateuliwa kuwa ni mwanachama wa Tume ya Kitaalimungu kimataifa na mwaka 1989 akachaguliwa kuwa Katibu wake mkuu. Mwaka 1990 Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa ni mwanataalimungu wa nyumba ya kipapa pamoja na kuendelea kuwa ni mtaalam mshauri wa Mabaraza na Tume mbali mbali za Kipapa mjini Vatican. Alishiriki kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya maadhimisho ya Jubilei kuu ya miaka elfu mbili ya Ukristo. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu mkuu tarehe 7 Oktoba 2003 na kuwekwa wakfu hapo tarehe 20 Oktoba 2003. Papa Yohane Paulo II kunako tarehe 21 Oktoba 2003 akamtangaza kuwa Kardinali. Kuanzia tarehe 1 Desemba 2005 akang’atuka katika utume wa kuwa ni mwanataalimungu wa nyumba ya kipapa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.