2016-03-31 15:07:00

Kesha la Jumapili ya huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema huruma ya Mungu inapaswa kumwandama mwamini katika maisha yake ya kila siku, waamini washangazwe na huruma ya Mungu katika maisha yao, kwani daima anawaonesha kwamba: anawapenda na anataka kuwashirikisha maisha yake ya kimungu! Ukweli wa maisha ya Kanisa unaweza kueleweka vyema zaidi ikiwa kama Kanisa litakuwa mstari wa mbele kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu.

Kanisa liwe ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu kwa watu wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na sababu mbali mbali, ili wote hawa waweze kuzamishwa kwenye Fumbo la huruma ya Mungu, kwa kuutazama Uso wa Kristo! Kanisa linaitwa kwa namna ya pekee kuwa shahidi mwaminifu wa huruma ya Mungu, kwa kuitangaza na kuishuhudia, kama kiini cha ufunuo wa Kristo Yesu. Ikumbukwe kwamba, Fumbo la Utatu Mtakatifu ni chimbuko la huruma ya Mungu ambayo haina mipaka!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Pasaka, maarufu kama Jumapili ya Huruma ya Mungu, tarehe 3 Aprili 2016 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii ya Misa Takatifu ni maalum kwa waamini na vyama vyenye Ibada kwa huruma ya Mungu. Ibada ya MisaTakatifu itaanza majira ya saa 4:30 asubuhi kwa saa za Ulaya. Tukio hili litatanguliwa na mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu utakaofanyika Jumamosi tarehe 2 Aprili 2016 kuanzia majira ya 12:00 za jioni. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kushiriki katika mkesha huu na wanachama pamoja na vyama vya kitume vyenye Ibada kwa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.