2016-03-30 11:26:00

Waamini kuwasha moto wa Injili, Kesha la Jumapili ya Huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ya Huruma ya Mungu, tarehe 3 Aprili 2016 anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada hii ya Misa Takatifu itatanguliwa na mkesha wa Jumapili ya huruma ya Mungu, utakayofanyika Jumamosi, tarehe 2 Aprili 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na vikundi vya “Udugu wa Kitume wa Huruma ya Mungu” kutoka majimbo mbali mbali nchini Italia. Utume huu ulianzishwa takribani miaka 20 iliyopita na  Padre Pasqualino di Dio.

Wanachama wa utume huu wanajitosa kwa namna ya pekee kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na matendo ya huruma kwa jirani zao. Hiki ni Kikundi kinachotaka kuishi kiaminifu huruma ya Mungu kwa njia ya tasaufi inayojikita katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu; Tafakari ya Neno la Mungu na huduma kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa njia hii, wanachama hawa wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaowasukuma kumwilisha matendo ya huruma; kiroho na kimwili kwa jirani zao.

Wanachama wa utume huu wameanzisha umoja wa wananchama wa huruma ya Mungu “Dives Misericordia, ONOLUS”, huko Gela, Caltanisetta. Kituo hiki kilianzishwa kunako tarehe 2 Aprili 2013 Baada ya Baba Mtakatifu Francisko kumwomba Pasqualiano di Dio kuanzisha nyumba ambayo watu wote wangeweza kujisikia kuwa wanakumbatiwa na huruma ya Mungu katika maisha yao kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kituo hiki kikazinduliwa tarehe 22 Machi 2014 na Kardinali Francesco Montenegro, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Agrigento, Italia.

Hii ni nyumba ambayo inataka kujielekeza zaidi katika utangazaji na ushuuda wa Habari Njema ya Wokovu unaojikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kwa kuwaendea maskini na wahitaji zaidi. Huduma hii inaungwa mkono na Askofu Rosario Gisana wa Jimbo Katoliki Piazza Armerina, Italia, ambaye mara kwa mara anatoa katekesi kuhusu Neno la Munguna familia. Utume huu unapania pamoja na mambo mengine kuhamasisha na kuendeleza Ibada ya huruma kwa watu mbali mbali ndani na nje ya Italia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.