2016-03-28 09:18:00

Pasaka ilete mwanga na amani Korea!


Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa ni nuru ya watu! Hivi ndivyo Kardinali Andrew Yeom Soo-yung, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Seoul, Korea ya Kusini anavyoandika katika ujumbe wake wa Pasaka kwa Mwaka 2016, wakati huu Mama Kanisa anaposherehea kilele cha ufunuo wa huruma ya Mungu kwa mwanadamu.

Kardinali Yeom anaitakia familia ya Mungu nchini Korea ya Kusini mwanga wa Kristo mfufuka katika maisha yake! Anawakumbuka na kuwaombea pia wananchi kutoka Korea ya Kaskazini, ili kweli amani na baraka za Mungu ziweze kuwashukia na kukaa nao daima! Ni matumaini ya Kardinali Yeom kwamba, Mwenyezi Mungu atawapatia ujasiri wa kuweza kumaliza mgogoro wa utengenezaji, ulimbikizaji na utumiaji wa silaha za Kinyuklia ambao kwa sasa unatishi usalama na amani ya Jumuiya ya Kimataifa.

Kardinali anakaza kusema, Yesu Kristo ni chemchemi ya maisha mapya na mwanga wa mataifa! Ni nuru inayoangazia dhambi na giza la maisha ya binadamu! Yesu ni mwanga ambao kamwe hakuna kitu chochote kinachoweza kuufifisha na kamwe hauwezi kumezwa na nguvu za giza! Baada ya Yesu Kristo kufufuka kutoka kwa wafu aliwatokea Mitume wake, akawaimarisha na kuwapatia ujumbe wa amani ambao wanapaswa kuutangaza na kuushuhudia sehemu mbali mbali za dunia.

Yesu mfufuka aliweza kufungua nyoyo za mitume wake waliokuwa wameelemewa na woga pamoja na wasi wasi; akawaonesha dira na njia mpya maisha! Jamii ya mwanadamu imeelemewa na giza nene la woga na wasi wasi; vita na mashambulizi ya kigaidi; bila kusahau athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Ulimwengu mamboleo una kiu ya kuona haki, amani na maridhiano yanamwilishwa katika maisha ya watu! Dunia kweli ina kiu ya amani! Wakristo wamepokea zawadi ya amani kutoka kwa Kristo Mfufuka, changamoto na mwaliko wa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mashuhuda wa mwanga wa upendo na matumaini duniani, hususan wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Anawakumbusha wanasiasa kwamba, dhamana na utume wao katika uwanja wa kisiasa unajikita katika huduma.

Uchaguzi mkuu nchini Korea ya Kusini, uwapatia nafasi waamini kuwachagua viongozi wenye ari na moyo wa kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Korea ya Kusini. Wananchi wote wanahamasishwa kutekeleza haki yao msingi kikatiba na kidemokrasia kwa kuwachagua watu ambao kimsingi wanahitaji pia mwanga wa Kristo Mfufuka, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao barabara! Kardinali Yeom anawakumbusha waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, wakati huu Kanisa linaposherehekea ufunuo wa huruma ya Mungu kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Anakaza kusema, iweni na huruma kama Baba yenu wa mbinguni! Huruma ni matunda ya mwanga mpya unaobubujika kutoka kwa neema ya Kristo Mfufuka!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.