2016-03-27 09:45:00

Ujumbe wa matumaini kutoka kwa Kristo Mfufuka!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu katika sherehe ya Pasaka ya Bwana, alitoa ujumbe na salam za Pasaka kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake kama zinavyojulikana “Urbi et Orbi”. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele! Yesu Kristo ni umwilisho wa huruma ya Mungu, kutokana na upendo mkuu, amekufa Msalabani na kufufuka kwa wafu, ndiyo maana Kanisa linatangaza: Yesu ni Bwana! Upendo wake wadumu milele, hii ni changamoto ya kumtumainia milele anasema Baba Mtakatifu.

Huruma ya Mungu ndiyo inayoweza kumpatia mwanadamu wokovu kutokana na kukengeuka na kumong’onyoka kwa maadili na utu wema; utupu wa maisha; chuki na kifo. Mwenyezi Mungu ndiye anayeweza kuujaza utupu huu kwa njia ya upendo wake unaowawezesha waamini kuambatana naye kuelekea katika Nchi ya uhuru na maisha tele! Yesu aliyeteswa, akafa, amefufuka kwa wafu! Hili ndilo tangazo la furaha kuu ya Pasaka, faraja kwa waja wake na kwamba, ameshinda kifo na mauti na hivyo anawashirikisha wafuasi wake maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Yesu anawaangalia wafuasi wake kwa uso wenye huruma na mapendo wale: wanaoteseka kutokana na baa la njaa, wenye kiu, wageni, wafungwa na wale waliosukumizwa pembezoni mwa jamii; wahanga wa ukosefu wa haki na vita. Dunia imesheheni watu wanaoteseka kiroho na kimwili, lakini vyombo vya habari vinaendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vitendo vya kikatili vinatendeka katika kuta za kifamilia; vita inayoendelea kusababisha madhara mabuwa kwa watu na mali zao!

Yesu Mfufuka anasema Baba Mtakatifu anapenda kutoa ujumbe wa matumaini kwa Syria, nchi ambayo kwa miaka mingi imetumbukia katika vita ambayo imesababisha uharibifu mkubwa, vifo, dhuluma na nyanyaso dhidi ya utu na heshima ya binadamu kiasi cha kugumisha mafungamano ya kijamii. Baba Mtakatifu anapenda kuweka matumaini yake kwa nguvu ya Kristo Mfufuka, ili kwa njia ya ushirikiano wa dhati, wote waweze kuvuna matunda ya amani, tayari kuanza mchakato wa ujenzi wa jamii inayojikita katika udugu, heshima ya binadamu na haki msingi za kila mwananchi.

Ujumbe wa maisha usikike tena miongoni mwa watu kwa kinywa cha Malaika kwa kufungua malango ya mioyo migumu huko Mediterrania na Mashariki ya Kati, hususan Syria, Yemen na Libya. Sura ya mtu mpya ing’aye juu ya Uso wa Yesu, ili uweze kusaidia mchakato utakaosaidia Wapalestina na Waisraeli kuishi kwa amani na udugu, huku kwa pamoja wakiwajibika kila siku katika mchakato wa ujenzi wa amani ya kweli na dumifu kwa njia ya majadiliano ya moja kwa moja yanayojikita katika ukweli!

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake wa Pasaka anaendelea kusema, Yesu Bwana wa uzima, aendelee kusaidia juhudi zinazofanywa huko Ukraine ili kupata suluhu ya kudumu dhidi ya vita nchini humo; kwa kupata pia msaada wa kiutu pamoja na kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa. Yesu Mfufuka, ni amani ya watu wake, kwa ufufuko wake ameshinda ubaya na dhambi. Sherehe ya Pasaka inawasukuma waamini kuonesha uwepo wao wa karibu kwa waathirika wa vitendo vya kigaidi, vinavyoendelea kusababisha umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia sehemu mbali mbali za dunia, kama ilivyotokea hivi karibuni huko: Ubelgiji, Uturuki, Nigeria, Chad, Cameroon na Pwani ya Pembe na Iraq.

Baba Mtakatifu anaombea matumaini na amani Barani Afrika hasa Burundi, Msumbiji, DRC na Sudan ya Kusini, nchi ambazo zinakabiliwa na hali tete ya kisiasa na kijamii. Kwa njia ya silaha ya mapendo, Mwenyezi Mungu ashinde ubinafsi na kifo; Mwanaye mpendwa ambaye ni Lango la huruma awe wazi kwa wote! Ujumbe wake wa Pasaka uwaendee na kuwafikia wananchi wa Venezuela, ili wale waliopewa dhamana ya kuwaongoza watu watekeleze dhamana yao kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi; majadiliano na ushirikiano na wote. Daima watu wajitahidi kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana, kuheshimiana pamoja na kudumisha haki, kwa kutoa fursa ya wananchi kufaidika kiroho na kimwili.

Kristo Mfufuka anawatangazia walimwengu wote Injili ya uhai, kwa kuwakumbuka na kuwasaidia watu wanaotafuta maisha bora zaidi; hawa ni wakimbizi na wahamiaji; kati yao kuna watoto wanaokimbia vita, baa la njaa, umaskini na ukosefu wa haki msingi jamii. Kwa masikitiko makubwa, watu hawa wakiwa njiani kwenye hija ya matumaini wanakumbana na kifo; ukatili kiasi hata cha kushindwa kukubaliwa kuingia na kupewa msaada wanaohitaji. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Mkutano wa Kimataifa kuhusu Ubinadamu utatoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na utu wake, ili kuibua sera na mikakati inayoweza kuwasaidia na kuwalinda waathirika wa vita, dhuluma na nyanyaso za kidini.

Baba Mtakatifu Francisko anamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi ya uumbaji, ingawa inaendelea kuharibiwa kutokana na ubinafsi na uchu wa utajiri wa haraka haraka unaharibu mazingira, nyumba ya wote! Baba Mtakatifu anawakumbuka wale wote wanaoishi katika maeneo yaliyoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi; watu wanaokumbwa na ukame pamoja na mafuriko kiasi cha kuathiri uhakika wa usalama wa chakula duniani!

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, anawakumbuka na kuwaombea kwa namna ya pekee Wakristo wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na: Uaminifu na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wote hawa anawaambia wasiogope, Yesu ameshinda ulimwengu! Pasaka ni kielelezo cha ushindi huu, Yesu ameyakanyaga mauti na kwa ufufuko wake kwa wafu amewezesha maisha kung’ara tena; amewakomboa watu wake kutoka katika utumwa na kuwaweka huru; kutoka katika huzuni na kuwakirimia furaha; kutoka katika maombolezo na kuwawezesha kushangilia tena; kutokana katika giza na kuingia katika mwanga; kutoka katika utumwa na kukombolewa, ndiyo maana waamini wanaimba Alleluiya!

Baba Mtakatifu anaendelea kuwatia shime wale wote waliokata taama na hawana tena matumaini na hamu ya kuendelea kuishi; wazee wanaoelemewa na upweke hasi pamoja na kuishiwa na nguvu; vijana wasiokuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, wote hawa waweze kupata faraja kutoka kwa Kristo Mfufuka, anayefanya yote kuwa mapya na kuwanywesha kwenye chemchemi ya maisha ya uzima wa milele. Ujumbe huu wa Yesu uwasaidie wote kuanza upya kwa kuwa na ujasiri wa ujenzi wa njia ya upatanisho na Mungu pamoja na jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.