2016-03-27 11:49:00

Shindeni kishawishi cha chuki na kinzani!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa na taarifa ya shambulizi la kujitoa mhanga lililofanywa kwenye Uwanja wa michezo wa Iskanderiya, Iran tarehe 26 Machi 2016 na kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Alberto Orthega Martin, Balozi wa Vatican nchini Iraq, unasema, Baba Mtakatifu anapenda kuwakumbuka na kuwaombea wale walioguswa na mashambulizi haya ya kigaidi; familia, ndugu na jamaa ili waweze kufarijiwa na Mwenyezi Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anawaombea marehemu wote waliopoteza maisha katika shambulio hili mwanga na pumziko la milele. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wananchi wa Iraq wataweza kujibu mashambulizi haya ya kigaidi yasiokuwa na tija wala mashiko kwa kujenga umoja na mshikamano, daima wakipania kushinda kishawishi chuki na kinzani, tayari kushirikiana kwa pamoja katika kujenga na kudumisha uhuru, mshikamano na heshima kwa wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.