2016-03-27 10:05:00

Papa Francisko ameonya dhidi ya kuufanya Ukristo kuwa kama shirika la Kimataifa


Baba Mtakatifu Francisko , akiongoza Ibada ya Mkesha wa Pasaka, katika homilía yake aliwaonya Wakristo kuitangaza furaha ya kweli ya Pasaka si kwa maneno lakini kwa vitendo ili kwamba Ukristo usionekana kama ni chama au shirika la Kimataifa lenye kuwa na wafuasi wengi na sheria teletele.  Alisisita Wakristo ni lazima waonyeshe tumaini jema linalotafutwa na watu wengi. Akiongoza Ibada hiyo ya Mkesha wa Pasaka Papa alibatiza wakatukumeni 12 wakiwa ni raia wa Italia, Cameroon , Korea, India na China.

Katika homilía yake ,  Papa alitafakari kitendo cha Mtume Petro kukimbilia  katika kaburi la Yesu baada ya kupewa habari na wanawake kwamba Yesu hayumo kaburini, akitoa ufafanuzi kwamba, Petro hana tena nafasi ya kuendelea kufunikwa na giza la huzuni , lakini aliruhusu mwanga wa Mungu kuingia moyoni mwake. Akili na moyo wa Petro mara viliguswa na habari kwamba Bwana wake hayumo kaburini.  Petro ingawa hakuamini ushuhuda wa wanawake, hakubaki ameketi alipokuwa,  hakubaki amejiinamia katika huzuni ya kifo cha mpendwa mwalimu wake, aliyemkana mara tatu, bali   hima, aliinuka na kukimbilia kaburini.  Papa amesema, hili  linaonyesha mabadiliko ndani ya moyo wake . Huu ulikuwa ni mwanzo wa moyo wa Petro kufufuka kutoka mawazo ya kale. Moyo wake unapata wogofu mpya, uliofukuza giza la woga, huzuni  na mashaka na  badala yake kujawa na matumaini, akiruhusu mwanga wa Mungu kuingia moyoni mwake,  na kubadilisha maisha yake.

Kama ilivyokuwa kwa Petro na wanawake, waliotoka mapema asubuhi kwenda kufanya tendo la huruma kuuhudumia mwili wa  Yesu , wanawake waliokuwa wamechukua Marhamu na manukato kaburini,  wanawake waliokuwa mwanzo wamejawa na hofu na kuinamisha vichwa vyao, kwa maneno ya malaika yaliyosema mnamtafuta aliye hai kati ya wafu, vivyo hivyo nasi hatupaswi kubaki tumejifungia ndani ya uchungu wetu wenyewe , lakini ni lazima kuiskiliza sauti ya Malaika anayevunja mihuri ya makaburi yetu ya kiroho na kutupa ujumbe kwamba Yesu amefufuka hayumo tena Kaburini . Ni muhimu kumruhusu Yesu Mfufuka aingie mioyoni mwetu., ili  mwanga wake umulike katika changamoto nyingi zinazotukabili,  na kuwa na utambuzi kwamba Yeye daima yu upande wetu na wala hatatutelekezi. 

Papa aliendelea kusisitiza kwamba hatuwezi kugundua hali ya maisha yetu kwa kubaki tumejifungia katika dimbwi la huzuni, woga na mashaka kwa   kuishi bila ya kuwa na matumaini. Tusiendelee kukaa ndani ya vifungo vyetu  wenyewe, lakini tuivunje mihuri ya makaburi yetu  na kutoka nje, ili Bwana apate kuingia katika  maisha yetu. Ni lazima kuachana na hofu za nyuma , udhaifu wa nyuma na maporomoko ya nyuma na kumpa mkono Yesu anayetaka kutuokoa katika dhiki zetu..  Papa alieleza na kuhimiza kwamba, usiku huo ulikuwa ni usiku wa kulisongeza kando jiwe la dhambi, dhambi zinazotufnga ndani ya utumwa wa maisha.  Aliendelea kumwomba Bwana, atuweke huru dhidi ya mitego ya kuwa Wakristo wasiokuwa na matumaini,  kuishi kama vile  Bwana  hakufufuka, kama vile hayuko katikati ya matatizo ya maisha yetu.

Hata hivyo Baba Mtakatifu aliweka bayana kwamba,  hii haina maana kwamba,  hatutapambana na matatizo. Matatizo ya kidunia yataendelea kuwepo daima, ndiyo maana tunatakiwa kukesha macho, kuupokea mwanga huu wa usiku huo wa Pasaka ,  mwanga  wa kipekee wa Bwana Mfufuka wenye kumlika katika matatizo yetu, ukitutaka tusiruhusu giza na hofu ya kudhibiti maisha  yetu;  lakini  tuongeze matumaini yetu na furaha yetu kubwa kwamba, Bwana Mfufuka  daima yu upande wetu na kamwe hatutelekezi.

Huu ndiyo msingi wa tumaini letu, si matumaini yenye mtizamo ya  kisaikolojia au kutafuta ufahari wa kidunia lakini ni kuwa na matumaini  ya maisha mazuri ya Kikristo,  ambayo ni  zawadi kutoka kwa Mungu. Zawadi yenye kutupa uhuru wa kweli wenye  kufungua furaha zote za mioyo yetu kwake. Tumaini lisilo  hadaa kwa sababu, humiminwa na  Roho Mtakatifu mioyoni mwetu. Papa aliitaja Ibada hiyo ya Usiku kuwa ni adhimisho la  tumaini hilo,  adhimisho la  ukweli huo, na wala hakuna kitu kinachoweza kulitenga na upendo wa Bwana kwa binadamu.  

Kwa maelezo hayo , Papa alitoa wito akimtaka kila mtu, kutoka nje na kuutangaza Ujumbe huu wa  kwa nia ya kuamsha na kufufua ari mpya katika matumaini kwa mioyo iliyozongwa na mzigo na huzuni na dhambi.  Kwa wale wanaopambana na changamoto katika kupata maana ya  maisha yenye matumiani baada ya maisha haya ya kidunia. Mkristo ni lazima kutangaza matumaini  ya maisha yajayo ya mbinguni , kama watumishi  wa matumaini hayo ya Upendo wa Kristo Mfufuka kwa kila binadamu,  vinginevyo Ukriso unakuwa kama chama tu  au shirika la kimataifa lenye  wafuasi wa  sheria nyingi nzuri, lakini wasiokuwa na matumaini kwa maisha ya baadaye .

Papa alitaja jinsi ya kuimarisha moyo katika tumaini hili, akisema ni kwa kukumbuka kazi za Mungu,  uaminifu wa Mungu na historia  ya upendo wake kwetu. Na muhimu kusoma Neno la Injili lenye kutukumbusha maneno yna matendo ya Bwana wetu Yesu Kristo. Vinginevyo alionya tutapoteza matumaini.  Ni kukumbuka wema wake na maneno ya Yesu  yenye kugusa na kuhuisha mioyo yetu. Haleluya Bwana Yesu amefufuka  Haleluya! 








All the contents on this site are copyrighted ©.