2016-03-26 11:29:00

Padre Cantalamessa; Kifo cha Kristo ni ushahidi wa huruma ya Mungu


Padre Raniero Cantalamessa, mhubiri wa nyumba ya Kipapa  wa wakati Ibada ya Ijumaa Kuu , alitoa  mahubiri yake katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya tafakari ya Neno la Mungu, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Fumbo la mateso na kifo cha Kristo, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu, mwaliko kwa waamini kujipatanisha na Mungu!

Padre Cantalamessa,  alilenga zaidi mada ya kujipatanisha na Mungu,  kupitia kwa Kristo ambaye alijipatanisha nasi na kutuachia kazi ya kufanikisha maridhiano kati ya watu.  Alieleza na kumshukuru Bwana kwamba, pamoja na dhaifu wetu wa  kiroho na dhambi,  kwa kufanya kazi pamoja nae Kristo aliyefanywa aonekana kama mdhambi ingawa hakuwa hata na doa la dhambi, katika  njia yake,  pia sisi tunawezeshwa kuwa watu wa haki mbele ya Mungu. Na kwa kufanya kazi pamoja nae Kristo, tunapata kuingia katika  huruma ya Mungu,  isiyoshindwa na jambo.

Padre Cantalamessa alisisitiza hilo kwa kuyarejea maandiko Mtakatifu mbalimbali kama ilivyoandikwa katika waraka wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (2Cor 5:18-) “ Yote ni kazi ya Mungu mwenye kutupatanisha sisi naye kwa njia ya Kristo , na kutupa jukumu la kuwatanisha watu naye”.

 Padre Cantalamessa anaendelea kueleza maana ya kujipatanisha na Mungu, akitazama uhalisia wake au iwapo ni hisia za kisaikolojia tu  au kama ni suala la kufikirika kidini au kiimani katika dunia ya leo hii,  ambayo imemezwa na fikira potovu juu ya Mungu. Alisema mbaya zaidi watu wengi wanamwelekeo wa kuhusisha mapenzi ya Mungu na kila jambo baya au lenye kuleta uchungu, ikionekana kama vile Mungu huvuruga  uhuru wa mtu na maendeleo yake. Humwona Mungu kama adui wa binadamu, kwa kila lililo jema  na furaha zake.

Aliendelea kueleza jinsi watu wengi wanauona  ukuu na nguvu ya Mungu katika muonekanao potovu kama ni Mkatili na mwenye hasira za  kulipiza kisasi kwa kila anayevunja sheria yake. Hivyo wengi kwa  sababu hiyo, hujenga hofu na hata chuki kwa  Mungu. Padre Cantalamessa alisema ,   mawazo na imani kama hiyo  ni upangani kwa mtu mwenye kuiijua sura halisi ya Mungu.

Mungu wa kweli daima amekuwa ni Mungu wa Huruma kwa binadamu hata wakati tunapomkosea, kama historia ya wokovu wa binadamu inavyoeleza,  tangu mwanzo wa kuuumbwa binadamu hadi kufikia nyakati za kuzaliwa Ukristo , imekuwa ni mwendeleo wa huruma ya Mungu kwa binadamu.

Padre Cantalamessa alieleza na kutoa mwaliko katika mwaka huu Jubilee ya Huruma, ni vyema kwa kila mmoja wetu,  kusoma maandiko Matakatifu  ili kuweza kuipata picha ya kweli ya Mungu, kupata kuelewa kwamba Mungu si tu anahuruma lakini Yeye mwenyewe ni huruma.

Na kwamba madai haya jasiri,  yanataka kuzingatia ukweli kwamba "Mungu ni upendo" (1 Yohana 4: 8, 16). Upendo  unaodhihirika katika Utatu Mtakatifu. Hivyo kumbe ,  Mungu ni upendo, na hakuna upendo wa kweli usiokuwa na huruma yenye kuandamana na utendaji wa haki.

Padre Cantalamessa, ameutaja  wakati huu kuwa ni wakati wa kupata utambuzi kwamba,  huruma daima huambatana na haki. Katika maisha ya Yesu tunaona kwamba huruma yake haikupingana na haki ,lakini  haki inatimiza sheria ya upendo na huruma, na si kutenda kwa sheria ya chuki na fitina za kulipiza kisasi, jicho kwa jicho , au jino kwa jino, lakini kulipa mabaya kwa huruma kama Msamaria Mwema. Ni muhimu kuona kwamba hatusamehewi dhambi zetu kwa sababu tumetenda mema, lakini kutokana na huruma yake ya kweli na halisi. Mungu hutenda kwa wingi wa huruma zake , kwa upendo wake mkuuu alionao kwetu sisi binadamu , upendo usiokoma hata pale tunapofishwa na mapungufu yetu na dhambi , bado Yeye hutufanya kuwa hai tena, kupitia msamaha wa dhambi uliotolewa na Mwanae Yesu Kristo katika kifo chake Msalabani.

Na kwamba, kifo cha Kristo  kilihitajika,  ili kuonyesha kwa kila mtu ushahidi mkuu wa huruma ya Mungu kwa  wenye dhambi.  Na ndiyo maana Yesu alikufa kifo cha kudharirika hadharani  akiwa katikati ya wezi wawili. Alipenda kubaki rafiki na wenye dhambi hadi mwisho, hivyo alikufa kama mmoja wao na pamoja nao.

Padre Cantalamessa alikamilisha homilía yake kwa kumwomba Mungu Baba wa Mbinguni , baraka za mwanae Yesu Kristo  aliyetundikwa juu ya msalaba kama mdhambi, atuwezeshe kuondoa kila roho ya kutaka kutenda mabaya iwe kibinafsi, au kifamilia, kijamii au kama taifa. Badala yake tujawe na upendo na huruma.  Baba wa Mbinguni na atuwezeshe katika Mwaka huu wa Jubilee ya Huruma  kuuishi upendo wa kweli katika maisha yetu, katika kuishuhudia furaha ya kweli inayotoka katika kina cha roho wa mapatano.  








All the contents on this site are copyrighted ©.