2016-03-26 09:26:00

Kufa kunoga!


Hatima ya binadamu ni sawa kwa wote. Watu warefu kwa wafupi, wanene kwa wembamba, matajiri kwa fukara, watawala kwa watawaliwa, Wanawake kwa wanaume, watoto kwa wazee, hatima yao wote ni kifo. Waswahili wanasema: “Asiyejua kufa aangalie kaburi.” Lakini fikra zetu zinatofautiana juu ya maisha baada ya kufa. Binadamu anatafiti juu ya kifo lakini hasa juu ya fumbo la hatima ya kifo, yaani baada ya kifo kuna nini zaidi. Wanaofikiri kwamba baada ya kifo hakuna kitu cha pekee,  hao ndiyo akina “Kufabasi”au akina “Pondamali kufa kwaja.” Wengine wanafikiri baada ya kufa kutakuwa na kufaidi vya kufaidi. Hao ndiyo akina “Yaani wee acha tu.” Kwa vyovyote hatima ya maiti ni fumbo kuu analolijua maiti mwenyewe tu. Ama kweli “adhabu ya kaburi aijuae maiti.” Kwa kusngazwa na Fumbo la kifo, mtu mmoja akajiita, “Kufakunoga”! 

Hebu tuangalie historia ya utafiti huo wa hatima ya maiti baada ya kuzikwa kaburini. Wayahudi waliamini kwamba kila mfu anaishia katika kaburi waliloita sheol yaani ulimwengu ulio chini zaidi ya ardhi. Huko katika sheol maiti anaoza na kugeuka mavumbi.“Binadamu kumbuka kuwa wewe ni mavumbi na mavumbini utarudi.” Kwa Wagiriki (wayunani) hatima ya maiti ni Hades, neno ambalo lugha ya kiingereza limefasiri kuwa Hell. kwa kiswahili ni motoni. Neno jingine la kigiriki Jehena lenye maana ya Ziwa la moto au tanuru la moto (Mateo 13:42).

Kadhalika Wabantu wanaamini kuwa binadamu anaishia ardhini. Mtu akifa anaoshwa katika shimo linaloitwa mfuva, kisha anazikwa katika kaburi, wanaloita litinda. Hilo ni kama jina analopewa mtoto wa mwisho kuzaliwa kitinda mimba, yaani mwisho. Kwa hiyo maana ya litinda ni zaidi ya kaburi au shimo. Kadhalika sheol siyo kaburi au shimo kwani kaburi kwa Kiebrania huitwa queber. Kwa kiebrania sheol maana yake ni kuita. Sheol lilikuwa ni shimo kubwa lililochongwa katika mwamba. Nje ya shimo hilo kulikuwa na mfuniko wa jiwe kubwa la mviringo linalofunika sheol. Kabla ya kumzika mfu, shimo hilo lilibaki wazi na lilikuwa na umbo kama mdomo wa mtu aliyeachama. Hivi mlango ule wa sheol ni alama ya mdomo wazi unaowaita na kuwaalika watu wote kuingia. Ndiyo maana kwa Wayahudi sheol hata kwa Waafrika litinda halifadhaishi sana kwani binadamu wote tunaitwa kuliingia. Kinachotuogopesha ni kule kuitwa tukiwa watoto au bado vijana kwani kufa uzeeni ni baraka: “Ibrahimu akafariki, naye akafa katika uzee mwema, mzee sana, ameshiba siku, akakusanyika kwa watu wake.” (Mwa. 25:8). Kadhalika ni baraka kuungana na ndugu na jamaa, kama Yakobo baada ya kufiwa na mtoto wake Yosefu aliposikia kuwa ameliwa na mnyama mkali: “Nitaenda chini kwenye sheol kumlilia mwanangu.” (Mwa 37:35).

Ufumbuzi wa kwanza wa hatima ya maiti tunausikia baada ya kifo cha Lazaro, “Marta akamwambia Yesu: Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo siku ya mwisho.” (Yoh 11:24). Yaani, pale ufalme wa Mungu utakapotawala katika ulimwengu huu, ndipo wenye haki watafufuliwa na kushiriki ufalme wake. Ufumbuzi wa pili ni pale Yesu alipomjibu Marta: “Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa (kimwili) atakuwa anaisha; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele.” (Yoh 11:25). Wakristo tunajivunia tamko la Yesu kwa sababu sasa tuna imani na matumaini juu hatima ya kifo. Lakini hata kama kusingekuwa na matumaini ya kuishi baada ya kufa kwa vyovyote Yesu ameyapa hadhi sana na utu wa hali ya juu sana wa maisha ya binadamu. Wakristu tunajivunia sana mapendekezo ya utu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hakuna yeyote aliyewahi kupendekeza mawazo kama hayo kabla na kuyatetea hadi kufa kwake kama alivyofanya Yesu.

Ufumbuzi wa tatu ni Yesu mwenyewe, pale alipoitwa kuingia katika domo la sheol. Huko sheol akakutana na walioingia humo kabla, akawapa uhai, hakurudi nao tena duniani, bali  akawaongoza mbele kwenye maisha yasiyorudiwa wala kuharibika. Kwa hiyo ufufuko huo hauwezi kudhihirishwa kwa macho ya kibinadamu. Kwa fikra hizo, hebu sasa tuangalie fasuli ya Injili ya leo. “Asubuhi ya kwanza ya sabato” yaani mwanzo wa siku mpya baada ya usiku wa giza uliowaweka watu kwa miaka mingi katika hofu na mahangaiko mbalimbali ya maisha. “Wanafika wanawake kaburini kumpaka Yesu mafuta” yaani, katika mahangaiko ya giza hilo, wanawake wanataka kupaka harufu nzuri kwenye maiti yasinuke, bila kukumbuka kwamba: “La kuvunda halina ubani.” Ndivyo binadamu anavyojaribu kuweka maiti yasioze, yaani kuyapatia maiti hadhi na heshima ili yaendelee kubaki. Kumbe wanawake wale “Wanalikuta jiwe limeondolewa kutoka kaburini.”

Wanawake wanachungulia ndani ya sheol hawaoni mwili wa Yesu. Kutokuuona mwili siyo kithibiti cha ufufuko bali ni alama tu. Kitendo cha kuchungulia kaburini ni mwaliko wa kutafakari sheol, isiyo na maiti ndani. Tunaalikwa nasi kutafakari kaburi. Baada ya tafakari, wanawake wakiwa na mafuta mkononi wakabaki mdomo wazi kama mdomo wa sheol. Kwa bahati nzuri wanawake wale “wakawaona wanaume wawili walio na mavazi meupe.” Hii ni picha ya kibiblia yenye kufafanua mambo yanayopita mahasa au vionjo vyetu yanahitaji kufunuliwa na Mungu mwenyewe. Mavazi meupe kuonesha usafi wa hali ya mbinguni. Mwinjili Marko anasema kijana ndiye aliyewatokea wanawake. Kijana huyo ni alama ya maisha mapya. Katika Injili  ya Mateo, malaika anashuka toka mbinguni, analiviringisha jiwe na kukaa juu yake. Hiyo ni ni alama ya ushindi kwamba msulibiwa hayupo.

Katika Injili ya Yohane wanatokea Malaika wawili, kuonesha ufunuo toka kwa Mungu mwenyewe. Kumbe Luka anatutajia watu wawili namba yenye kumaanisha ushahidi wa kweli wa watu wawili. Mbele ya domo lile la sheol, wanawake wanafunuliwa na Mungu (kwa njia ya wanaume hao wawili) na kuhakikishiwa kwamba nguvu za kimbingu zimeingilia kati na kushinda kifo. Kwamba, suala la hatima ya kifo liko mikononi mwa Mungu peke yake, na hakuna mtu yeyote anayeweza kulichakachua. Ndiyo maana Kanisa Katoliki linapinga adhabu ya kifo! Kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mapato yake,“Wanawake wanabaki kuogopa.” Hii ni alama ya jumuia ya kikristu inayobaki kushangazwa na tukio hili la kaburi wazi. Wanaume hao wawili wanawaambia wanawake: “Kwa nini mnamtafuta mzima katika wafu.” Kwamba wanayemtafuta angekuwa amehuishwa basi angebaki bado anatawaliwa na mauti. Kumbe huyo ni mzima na haguswi tena na mauti. Amefufuka, hayuko hapa kwani ufufuko siyo kurudi tena duniani, bali kwenda kwenye ulimwengu ambako hakuna alama yoyote ya kufa.

Kisha Wanaume hawa wanawakumbusha wanawake aliyosema Yesu kule Galilaya: “Ninayatoa maisha yangu, lakini siku ya tatu nitaingia kwenye maisha ya milele.” Kwamba, maisha yaliyotolewa kwa ajili ya wengine hayafi bali yanawekezwa kwa ajili ya umilele. Maisha ya upendo na ya kujitolea kwa wengine hudumu milele. “Na wanawake wakakumbuka maneno hayo.” Maneno hayo yanatuhusu sisi binadamu jinsi gani tunaweza kuwa na mang’amuzi ya ufufuko. Kaburi wazi siyo kithibiti cha ufufuko wa Yesu bali ni mwanga unaotukumbusha juu ya maisha ya Kristu. Hutufumbua macho kuyaona mambo yasiyoonekana. Yesu mwenye moyo safi ameishia kuona ulimwengu wa Mungu. Kadhalika wenye moyo safi ni wale walio na akili na moyo huru wa kuona mwanga utokao mbinguni. Heri wenye moyo safi kwani watamwona Mungu. “Wanawake wanarudi na kwenda kwa mitume na kuwaambia mang’amuzi yao.” Nao mitume wanashangaa wanachoambiwa, wanaamua kwenda kaburini. Nao wanashuhudia kwamba kweli kaburi ni wazi nao wanaingiwa na mashaka.

Hapa tunafundishwa kwamba, imani ya kweli budi ipitie mashaka na woga kama ya mitume na wanawake. Mashaka kwamba baada ya kufa unaingia ulimwengu wa Mungu. Kumbe hiyo ni safari ya wale wenye moyo safi ndiyo wanaopitia njia ya mashaka kama yale ya Mitume. Lakini ukikumbuka kile kilichotokea alichosema Yesu Galilaya, hapo unafikia kumwona mfufuka katika mtazamo wa imani na kuwa na uhakika kwamba maisha ya majitoleo na ya upendo hayapotei bali unayawekeza na kuyahifadhi katika ulimwengu wa Mungu. Kwa hiyo, wakristo wameachiwa na Yesu dhamana ya kutoa jibu sahihi juu ya hatima ya kifo kwa kufanya matendo ya upendo na huruma kama Kristo alivyofanya. Na hii ndiyo changamoto kubwa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha kilele cha upendo na huruma ya Mungu kwa mwanadamu! Heri kwa Sikukuu ya Pasaka.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.