2016-03-25 08:44:00

Mshikamano wa upendo na Wakristo huko Mashariki ya Kati!


Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Makanisa ya Mashariki anasema kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana ili kuondokana na mantiki ya ubinafsi na kuta za utengano ambazo hazina mashiko wala tija kwa watu wanaoishi huko Mashariki ya Kati. Misaada inayotolewa na Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuwafikia walengwa huko: Mashariki ya Kati hasa Syria na Iraq. 

Mchango wa Ijumaa kuu unaotolewa na waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni kielelezo cha upendo wa mshikamano na Wakristo wanaoishi huko Nchi Takatifu. Mahusiano kati ya Israeli na Palestina bado hayajaboreka sana, kumbe bado kuna watu wanateseka na kuhangaika sana kutokana mipasuko ya kijamii, hali ambayo imepelekea pia kushuka kwa idadi ya mahujaji na watalii wanaotembelea Nchi Takatifu.

Kardinali Sandri anasema, hali ya wananchi wa Syria na Iraq ni mbaya sana kutokana na vita pamoja na misigano ya kisiasa, kijamii na kidini inayoendelea katika maeneo haya, hali ambayo imechangia kuibuka kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotaka hifadhi na usalama wa maisha yao. Kuna idadi kubwa ya wakimbizi kutoka Syria wanaopata huduma huko Lebanon. Hata nchini Lebanon, hali ya kisiasa ni tete kutokana na mkwamo wa uchaguzi wa Rais, ingawa Lebanoni ni nchi muhimu sana ambayo ilipewa umuhimu wa pekee katika maabara ya majadiliano ya kidini na kiekumene; ujumbe wa amani na mshikamano na Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI.

Hali ngumu ya maisha huko Mashariki ya Kati ni changamoto kwa Jumuiya ya Kimataifa, lakini hata Kanisa linapaswa kuchangia kwa hali na mali, ili kukuza na kuumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Amani ni njia pekee ambayo ingeweza kudumisha mchakato wa maendeleo huko Mashariki ya kati, lakini hadi wakati huu, amani imewekwa rehani kutokana na misigano ya kisiasa, kiuchumi, kidini na kijamii.

Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa linaendesha hadi wakati huu kampeni ya amani! Waamini wanaalikwa kusali kwa ajili ya kuombea amani ya Yerusalemu. Ukosefu wa amani huko Mashariki ya Kati ni kutokana na kuenea kwa biashara haramu ya silaha inayoendelea kuwanufaisha watu wachache kwa kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kujipanga vizuri zaidi ili kuwasaidia wananchi wa Syria kupata amani, itakayosaidia kuharakisha mchakato wa maendeleo ya watu: kiroho na kimwili.

Kuna idadi kubwa ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria na Iraq wanaohitaji msaada wa hali na mali, changamoto inayopaswa kushughulikiwa kikamilifu na Jumuiya ya Kimataifa, kwa kulinda na kuthamini utu na heshima ya wakimbizi na wahamiaji, badala ya kujenga kuta za utengano, chuki na uhasama kati ya watu. Juhudi zaidi zinahitajika ili kuokoa maisha ya wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania. Si rahisi sana wakimbizi na wahamiaji kurejea tena makwao, kwani huko hawana kitu ambacho wanaweza kukitegemea kwa ajili ya maisha, ustawi na maendeleo yao kwa siku za usoni! Hawa ni watu waliojisadaka katika safari ya matumaini, ambayo wakati mwingine yanazimika kama ndoto ya mchana kwa vifo, shida na changamoto mbali mbali za maisha!

Makanisa yanaendelea kushirikiana kwa kujikita katika Uekumene wa damu na huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji; mambo mengine ni kumwachia Roho Mtakatifu atende kadiri anavyoona inafaa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo. Kimsingi, Wakristo wanafurahi na kumtukuza Mungu wanapoona na kushuhudia umoja na mshikamano unaoshuhudiwa na viongozi wao wakuu wa Makanisa na sadaka ya mshikamano inayotolewa na wakristo wengine, ili kuwaonjesha huduma ya upendo, wale wanaoteseka kutokana na vita, nyanyaso na dhuluma kwa misingi ya kidini, kisiasa, kiuchumi na kijamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.