2016-03-25 09:43:00

Maungamo ni sanaa ya maisha ya kiroho!


Maungamo ni sanaa ya maisha ya kiroho inayomwezesha mwamini kuchunguza dhamiri yake, kutubu, kuungama na hatimaye, kutimiza malipizi ya dhambi zake, tayari kuambata huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Maungamo si mchezo wa kuigiza, yanahitaji maandalizi makini ili kuweza kupokeza zawadi ya huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Muungamishaji anapaswa kutambua kwamba, kwanza kabisa ni mdhambi ambaye ametubu na kuonjeshwa huruma na upendo wa Mungu ambao anawashirikisha waamini wanaokimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu, yaani Sakramenti ya Upatanisho.

Hii ni tafakari iliyotolewa hivi karibuni na Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume wakati wa kozi maalum kwa ajili ya waungamishaji, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambamo Sakramenti ya Upatanisho na ushuhuda wa imani unaomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili vinapewa msukumo wa pekee. Waungamishaji hawana budi kuandaliwa na kufundwa barabara katika maisha ya kiroho na mafundisho tanzu ya Kanisa, ili kuweza kukabiliana na changamoto zinazoendelea kuibuka katika shughuli za kichungaji na kitaalimungu, ambazo Mapadre wengi wanakumbana nazo katika ulimwengu mamboleo.

Padre muungamishaji anapotekeleza dhamana na wajibu wake katika kiti cha huruma ya Mungu anapaswa kuonesha katika maneno na matendo yake ukweli wa Kiinjili unaopaswa kushuhudiwa na Mama Kanisa; mafundisho tanzu ya Kanisa Katoliki na kwamba, huruma ya Mungu ni kubwa zaidi kuliko hata dhambi ambazo zinatendwa na mwamini. Kumbe, lengo la kozi hii maalum ni kuwasaidia Mapadre vijana kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini na vyombo vya huruma ya Mungu.

Kardinali Mauro anasema, Idara ya Toba ya Kitume ni huduma makini ya maisha ya kiroho inayojikita katika maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na uwepo wa Kanisa la Kristo, kwa ajili ya wokovu wa roho za watu “Salus animarum”. Ni Idara inayowahamasisha waamini kuanza mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kujipatanisha na Mungu, Kanisa na ndugu zao, kwani upatanisho ulioletwa na Kristo Yesu na kutekelezwa na Roho Mtakatifu katika maisha ya waamini unamwilishwa kwa njia ya Kanisa. Kanisa linaishi na kutenda katika nyakati na historia ya mwanadamu kwa kuungana na Kristo ambaye ni kichwa cha Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa.

Padre muungamishaji ni daraja kati ya huruma ya Mungu na udhaifu wa mwanadamu. Ni kielelezo cha upendo angavu wa Mungu na kiungo muhimu cha mwaliko kwa mwamini kukimbilia na kuambata utakatifu wa maisha, ili kuwa kweli ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa. Padre muungamishaji si hakimu wa mambo matakatifu, bali ni dira inayomwongoza mwamini kuelekea katika uhuru kamili wa mtoto wa Mungu. Padre muungamishaji ajifunze kuwapenda na kuwathamini wadhambi wanaokimbilia huruma ya Mungu, ili aweze kuwasaidia kuwa waaminifu kwa ahadi zao za Ubatizo. Lengo kwa waamini ni kutotumbukia katika dhambi za mazoea, kwa kuwa na dhamiri nyofu inayoangazwa na mwanga wa Injili sanjari na Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili kukabiliana na changamoto za kiimani, kimaadili na utu wema!

Kardinali Mauro Piacenza amewakumbusha Mapadre na waungamishaji wa siku za usoni kwamba, wao ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa mwanadamu; ni madaktari waliojeruhiwa na kuponywa kwa huruma na upendo wa Mungu, sasa wanatumwa kuwaponya na kuwaganga wale wanaokimbilia huruma, msamaha na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Wahudumu wa Sakramenti ya Kitubio wawe wa kwanza kukimbilia huruma ya Mungu katika maisha yao.

Sakramenti hii iwe ni ushuhuda wa furaha kati ya mdhambi na Kristo, chemchemi ya maisha mapya, anayewazamisha wadhambi katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Mwamini anapokimbilia kiti cha huruma ya Mungu anataka kuonja wema na upole; ukarimu na msamaha; upendo na huruma ya Mungu; ili kuwa watu huru zaidi. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa makini kwa Mama Kanisa kuendelea kuwaalika waamini kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.