2016-03-25 10:16:00

Chuchumilieni utakatifu wa maisha!


Kwaresima kimekuwa ni kipindi cha sala, toba na wongofu wa ndani; muda muafaka wa kutafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Askofu Titus Joseph Mdoe wa Jimbo Katoliki Mtwara katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, haya ni malengo ya jumla kwa waamini wote. Lakini, ikumbukwe kwamba, waamini wanaitwa kuuishi imani kikamilifu, kwa kuchuchumilia utakatifu wa maisha. Huu ndio wito mkubwa unaotolewa na Mwenyezi Mungu kwa waja wake.

Askofu Mdoe anasema, Kipindi cha Kwaresima kimekwisha, lakini waamini wanapaswa kuendelea kufanya maboresho katika maisha na mahusiano yao na jirani pamoja na Mwenyezi Mungu, kwa kutambua kwamba, shetani bado anazunguka zunguka akitamani kuwabwaga dhambini. Waamini wawe na ujasiri wa kutumainia maongozi ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Waendelee kuchunguza dhamiri zao kwani mapambano baado yanaendelea ili kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika maisha yao ya kiroho na kimwili.

Askofu Mdoe anakaza kusema, pale ambapo waamini wamefanya vyema katika maisha yao, basi wapaendeleze zaidi na pale ambapo wametindikiwa neema na baraka, wawe na ujasiri wa kluomba huruma na neema ya Mungu, tayari kujikita katika mchakato wa maboresho ya maisha, kwani hiki ni kipindi cha utakaso, tayari kuadhimisha Fumbo la Pasaka wakiwa wapya katika maisha ya kiroho sanjari na kuendelea kujikita kwa Yesu Kristo! Waamini wasibweteke kwa kumaliza mfungo wa Kwaresima, bali watambue kwamba, mapambano ya maisha ya kiroho bado yanaendelea hadi pale Kristo atakapokuwa yote katika wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.