2016-03-24 09:04:00

Siku ya XXIV ya Wamissionari mashuhuda wa huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Injili ya furaha, “Evangelii gaudium” anasema wainjilishaji waliojazwa roho humaanisha wainjilishaji ambao bila woga wako wazi kwa kazi ya Roho Mtakatifu ambaye anawawezesha kutoka katika undani wao na kuwageuza kuwa ni watangazaji na mashuhuda wa matendo makuu ya Mungu! Hawa ni mashuhuda wenye uwezo wa kuzungumza na watu katika lugha zao, ni jasiri katika kutangaza upya wa Injili kwa ushupavu zaidi, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao!

Tarehe 24 Machi 2016 Kanisa linaadhimisha Siku ya XXIV ya Wamissiomari Wafiadini! Hawa kwa njia ya maisha yao, wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wa nyakati hizi! Ni Siku ambayo Kanisa linafanya kumbu kumbu ya kifodini cha Mwenyeheri Oscar Armulfo Romero, Askofu mkuu wa El Salvador, aliyeuwawa kikatili kunako mwaka 1980 wakati akiadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Wamissionari mashuhuda wa imani wameyamimina maisha yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili ya imani na matumaini kwa watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia. Wakaiona ile sura Kristo mteswa kati ya wagonjwa, maskini na wazee, kama ilivyotokea kwa Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta waliouwawa hivi karibuni nchini Yemen. Wamissionari mashuhuda wa huruma ya Mungu wamekuwa tayari kuyamimina maisha yao, kielelezo cha upendo mkuu unaomwilishwa katika huduma makini.

Takwimu zinaonesha kwamba, katika kipindi cha mwaka 2015 kuna Wamissionari wa huruma ya Mungu 22 waliouwawa kikatili sehemu mbali mbali za dunia. Baadhi ya wamissionari hawa wameuwawa kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, wengine wakati wa majaribio ya unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na vitendo vya ujambazi vinavyoonesha changamoto ya kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema.

Hawa ni mashuhuda waliokita maisha yao katika kutangaza Neno la Mungu, kuadhimisha Sakramenti za Kanisa na huduma za kichungaji kwa familia ya Mungu. Kuna baadhi yao wametekwa nyara na hawafahamiki mahali walipo kama kesi ya Padre Paolo Dall’Oglio, aliyetekwa nyara nchini Syria kunako mwaka 2013 hadi sasa hafahamiki mahali alipo! Wamissionari hawa wamekuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waja wake sehemu mbali mbali za dunia.

Katika mkesha wa maadhimisho ya Siku ya mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake iliyoandaliwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, katika mkesha huu, Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya wakleri, amewakumbuka Wakristo na wamissionari walioyamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake sehemu mbali mbali za dunia. Hiki ni kipindi cha mashuhuda wa imani, pengine kuliko hata wakati mwingine wowote katika historia na maisha ya Kanisa.

Kardinali Stella ametumia fursa hii kuwaomba wale waliowateka nyara  mihimili ya Uinjilishaji kuwaachia ili waendelee na huduma yao kwa familia ya Mungu. Kanisa limewakumbuka hata wale wote wanaoendelea kupoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuimarisha ulinzi na usalama sanjari na kuwa na sera na mikakati ya pamoja katika kupambana na vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu, heshima na mafungamano ya kijamii.

Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji. Kardinali Stella anakaza kusema mashuhuda wa imani ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa Kanisa kwa kumwambata Kristo katika Fumbo la Msalaba, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake.Wakristo wanapaswa kuendelea kuwa kweli ni mwanga wa mataifa na chumvi ya dunia kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! Lakini ni jambo lisilokubalika kutumia dini kwa ajili ya ukatili na mauaji! Jina la Mungu linaalika upendo na ukarimu; baraka na huruma; udugu na mshikamano! Huu ndio ujumbe unaofumbatwa katika jina la Mungu ambaye ni huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.