2016-03-24 11:47:00

Homilia ya Papa kwa adhimisho la Ibada ya Misa ya Krisma ya wokovu


Kanisa limekianza  kipindi maalum cha  Siku Tatu Kuu za Pasaka, kwa adhimisho la Alhamis Kuu, ambamo kwa namna ya kipekee, huadhimisha matukio matatu ya kiliturujia, Ibada ya Krisma ya wokovu, huduma ya kuosha miguu na  Karamu ya Mwisho, yaani Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Baba Mtakatifu Francisko, amefungua maadhimisho haya mapema Alhamis, kwa kuongoza Ibada ya Misa ya kubariki Krisma ya wokovu,  katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro hapa Vatican . Na majira ya jioni Papa anaadhimisha Ibada ya Misa kwenye kituo cha wakimbizi wa kisiasa wanaoomba hifadhi nchini Italia, kituo  kilichoko huko Castel Nouvo di Porto nje kidogo ya mji wa Roma, ambako anawaosha miguu wahamiaji kumi na mmoja, kama ishara ya kuguswa na hali za watu walio katika mahangaiko ya maisha yaliyo nje ya uwezo wao.

Katika homilia yake ya wakati wa Ibada ya  Krisma ya Wokovu, aliyarejea masomo ya siku akilenga  kwa mara nyingine akiifafanua huruma ya Mungu , kwamba, huanza na kukutana na Bwana,  pili ni kuona thamani ya Msahama wa Bwana.

Papa alitafari kwa kuyalenga masomo ya siku akisema, ilitazamiwa  katika hali ya kawaida watu waliokuwa katika Sinagogi wakimsikiliza Yesu,  wamshangilie  kwa furaha lakini ilikuwa kinyume chake, kwa wengi wao mioyo yao ilizongwa na kinyongo cha wivu na chuki na hivyo kuwa watu wa kuhoji maswali mengi juu yake, wakimtaka aondoke zake, wakisahau maneno na matendo yake yote waliyokuwa wakiyastaajabia ,mwanzoni. Papa amesema hii, ilikuwa ni kutimiza unabii Mzee Simeoni, kwa Bikira Maria kwamba atakuwa, Yesu atakuwa ishara ya matatizo. Na kwamba, Yesu kwa maneno na matendo yake, anaweka nje siri za moyo wa kila mwanamme na mwanamke.

Papa aliendelea kuzungumzia Injili ya huruma ya Baba inayotangazwa  bila masharti,  kwa maskini,  na wanao onewa akisema kwamba ni wito unaotutaka tuchukue msimamo imara katika kupigana vita vizuri vya imani.  Si vita kati ya binadamu,  wanaume na wanawake, lakini dhidi ya shetani, adui wa binadamu. Papa amewahakikishia waamini kwamba hakuna sababu za kuongopa kupambana na shetani kwa kuwa Yesu huinglia kati, na ni Yeye mwenye kuleta hali mpya yenye kuponya na kutuweka huru dhidi ya dhambi.

Papa ameeleza na kutaja kwamba, hakuna maneno yanayoweza eleza kuu na umilele wa huruma ya Mungu kwa Mdhambi. Hili linabaki kuwa siri kubwa, katika huruma yake ya  milele , ambayo huonekana katika hatua zote zamaisha ya kila siku, katika upigaji wa  hatua mbele kidogo kidogo, hata katika hali za giza la kutofautiana na fujo na ghasia zinazoendelea duniani. Ili kupambana na hali hizo, Papa ametoa wito kwa watu wote kuiga mfano wa Msamaria Mwema, mtu mwenye kuonyesha sura ya mtu mwenye huruma. Aidha amemtaka kila mmoja kuyachunguza maisha yake mwenyewe iwapo yanakwenda sawa na huruma ya Mungu .Anasema kila mmoja na afanye jitihada katika kukumbuka njia ambamo  Bwana amekuwa na huruma kwetu, kuliko  hata tunavyoweza  kufikiri . Kwa kufanya hivyo,  tunaweza kupata ujasiri wa kuomba ,  hatua zaidi zenye kudhihirisha huruma yake katika siku zijazo  kwa kuomba, ”Tuonyeshe, Bwana, huruma yako".  Papa ameeleza na kumtaka kila mmoja kuvunja mduara wa  ukatili na kiburi cha ubinafsi, badala yake kujikita katika njia sahihi za kuwa na roho ya Kimungu yenye kufurika huruma yake ya  milele.  

Katika Ibada hii ya Krisma ya Wokovu, Papa pia aliwageukia wachungaji wa kanisa,  Mapadre au  Makuhani, akiwataka wawe mashahidi na wahudumu kweli wa  huruma ya Baba wa Mbinguni. Na ili waweze kugusa mioyo ya watu amesema , wanapaswa kufurahia zawadi waliopokea ya kushiriki katika kazi za kuimwilisha huruma ya Mungu kama alivyofanya Yesu, ambaye alihubiri Injili ya Upendo huku  akitenda mema na kuponya. Hii itasaidia watu wote,  kuelewa ukweli na utendaji wa huruma  ya Mungu katika njia zake zenye  kuheshimu utamaduni wa familia na watu mahalia.

Aidha homilia  ya Papa imeainisha  Alhamisi hii Takatika katika kipindi cha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya  huruma ya Mungu, akitaja  maeneo mawili, yanayo onekana zaidi katika matendo ya huruma, kwamba ni kukutana na pili ni msamaha wa Mungu wenye kumrudishia binadamu hadhi na utu wake! Amefafanua hatua ya kwanza ya kukutana na Mungu kwa kufanya rejea  kwa mfano wa Mwana Mpotevu, aliyerejea nyumbani kwa baba yake na Baba akampokea mwana huyo kwa huruma kubwa licha ya kurudi akiwa mikono mitupu. Baba ambaye hakuanza kuhesabu makosa ya mwanae lakini alichojali zaidi ni mwana wake kumrudia. Hiyo ndiyo sababu ya Baba Huyo alifurahi na kuitisha siku kuu kubwa.  Pia kama ilivyokuwa kwa yule mkoma aliyekutana na Yesu na kuponywa, mkoma huyo, alipiga magoti mbele ya Bwana,  kumtukuza na kumshukuru Mungu kwa sauti. Na ndivyo ilivyo pia kwa kila mdhamb anayetafuta msamaha wa Mungu, kwanza anapaswa kuona aiba kwa  dhambi zake na kisha arejee kwa Mungu na kuomba msamaha na Mungu atamsamehe kumrudishia heshima ya utu wake. Papa pia alirejea tukio la Mtume Petro, ambaye baada ya kumkana Yesu,  alitambua makosa yake na kujionea aibu mwenyewe na kuomba msamaha. .

Aidha Papa amewakumbusha Mapadre wenzake,  hatari za kufunikwa na giza la mambo ya kidunia kupitia uwepo wa mambo mengi mbalimbali ya kisasa yenye kuwa na ushawishi mkubwa wa  kwenda nje ya uadilifu wa kikuhani na kuwafanya wasahau lengo lao la kuwatumikia maskini , wanyonge na wafungwa. Amesisitiza kama Makuhani ni lazima  kutambua kwamba , kuna watu  maskini, wasiokuwa na  elimu na  wafungwa, ambao wanajikuta katika hali kama hizo zenye kuwaweka katika mateso.  Amewataka  Mapadre  daima watafute kutopungukiwa na mwanga wa imani, daima wawe na kiu ya kiroho inayotafuta kupozwa kwa kazi za kuhudumia maskini na wanaodhulumiwa si  kwa vitisho na mashinikizo, lakini kwa kuongozwa na upendo na urafiki kwa watu wote , wanaume na waume, ambao kama kondoo wanaosubiri kusikia  sauti ya mchungaji wao.

Papa alikamilisha kwa kuomba katika Jubilee hii ya Mwaka wa Huruma, kama Mapadre waiadhimishe kwa moyo shukrani na unyenyekevu wenye kuikumbuka  huruma yake ya  milele, inayoonekana katika majeraha ya  Bwana wetu Yesu Kristo. Na pia waombe kusafishwa dhambi zote na kuwekwa huru dhidi ya kila ovu. Na kwa neema ya Roho Mtakatifu, warudie ahadi yao upya ya kuifikisha  huruma ya Mungu kwa wanaume na wanawake wote, wakifanya kazi kwa kuhamasishwa na Roho  Mtakatifu  kwa ajili ya manufaa ya taifa zima la Mungu.








All the contents on this site are copyrighted ©.