2016-03-23 14:28:00

Papa aitafakari huruma ya Mungu katika Juma kuu


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano hii akitoa mafundisho yake kwa mahujaji na wageni , alitazama kwa makini zaidi Siku Tatu Kuu za Wiki Takatifu, Alhamis, Ijumaa Kuu na Jumamosi Kuu katika mwanga wa adhimisho la Jubilee ya Huruma ya Mungu,  akianisha na Maandiko Matakatifu ya Injili. Amekitaja kipindi hiki cha siku tatu kuu, kuwa wakati muhimu wenye kutuingiza katika kina cha kutafakri zaidi fumbo hili la Imani ya Kikristo, mateso, kifo na Ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo.

Kwa maoni hayo, Papa ametoa mwaliko kwa waamini wote, kujiandaa kwa maadhimisho ya siku hizi tatu kuu za Pasaka, kwa namna ya pekee, kipindi kinachoanza na  Alhamisi Kuu,  ambamo Yesu mwenyewe anajitolea kwetu kama chakula cha Kiroho. Aidha katika siku hii Yesu aliwaosha miguu  mitume wake, kama kielelezo cha upendo unaomwilishwa katika huduma makini!

Na ameitaja Ijumaa Kuu kwamba ni  siku ya kuzamisha  tafakari  katika Fumbo la  upendo usio kifani wa kifo cha Kristo msalabani. Yesu anakubali kufa Msalabani, akitimiza kazi aliyopewa na Baba yake ya kuleta wokovu kwa dunia nzima , upendo wa majitoleo yasiyokuwa ya kujibakiza na  bila mpaka.  Ni upendo wenye kumkubatia kila mmoja, na hakuna anayetengwa nao. Ni upendo unaoendelea kuwepo katika nyakati zote na mahali pote , kama chemichemi ya wokovu ambamo kila mdhambi apate kuokolewa.  Papa ameeleza na kutoa wito kwamba, iwapo Mungu ametuonyesha upendo wake kupitia kifo cha  Yesu , kumbe nasi tukiwa tumejazwa na Roho Mtakatifu, tunaweza na inabidi kuwapenda wengine kama Kristo alivyotupenda.

Mwisho Papa alitoa maelezo juu ya Jumamosi Kuu, akiitaja kwamba ni siku ya Ukimya wa Mungu, yenye kutualiaka sote, kuifanya siku hiyo kuwa ya ukimya mwingi kwa kuwa asili yake kama ilivyokuwa wakati ule , ni siku ya ukimya wa Mungu.  Yesu alilazwa kaburi ili ashiriki hatua zote za kifo cha binadamu . Ni ukimya wenye kuzungumza na kuonyesha upendo wa kweli katika kushikamana na wengine na hasa walio telekezwa, ambamo Mwana wa Mungu aliionyesha sura ya Huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka wala ukomo, katika ukamilifu wake. Katika siku hiI yaUkimya inakuwa ni wakAti wa kusubiri kwa hamu ufufuko wa Bwana . Ni siku ya kutafakari ukimya wa Mama Bikira Maria aliyesadiki kwamba katika ukimya kuna Ufufuko . Na hivyo Mama Maria anakuwa daima ni alama ya ukimya huu wa Jumamosi Takatifu.

Papa ameeleza na kutoa mwaliko kwa kila mmoja katika siku hizi kujiandaa kikamilifu, kwa ajili ya kukutana na Huruma hii ya Mungu isiyokuwa na mipaka. Siku hizi tatu Kuu  ni wakati wa kutafakari sura hii ya mateso na kifo cha Bwana, na kukumbatia yote katika ukimya wa Jumamosi Kuu, huku tukijiandaa kusherehekea siku zijazo kwa moyo wa shukrani kwa siri hii kuu ya huruma ya Mungu, iliyotolewa kwa ajili yetu juu ya msalaba wa wokovu wetu.








All the contents on this site are copyrighted ©.