2016-03-23 08:21:00

Mshikamano na Wakristo wanaoteseka!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, matendo ya huruma na upendo ni kielelezo makini cha Kristo ambaye ni ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; huu ni utajiri na utamaduni wa Kanisa. Katika ulimwengu mamboleo mkazo unatolewa zaidi kwa watoto yatima, wajane, wagonjwa, wafungwa na wageni.

Hawa ni watu wanaopaswa kukumbukwa wakati wa kufunga na kujinyima kunakofanywa na waamini katika kipindi cha wokovu, ili kiweze kuwa pia ni kipindi cha wokovu na faraja kwa makundi haya ya watu! Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, kuna maskini wa aina mpya ya umaskini unaogusa watu si tu katika masuala ya kiuchumi; bali hata kiroho, kiakili, kisaikolojia, kiutu na kijamii. Maskini wa roho kimwili ni wadhambi; watu waliokata tamaa; wakajitenga na Kanisa n ahata wakati mwingine kulijeruhi Kanisa kutokana na misimamo na maamuzi yao.

Wadhambi hawa pia wanahitaji huruma na msamaha unaotolewa na Mama Kanisa kwa kuwakumbatia na kuwapokea wote ili kuwapatia fursa ya kutubu na kumwongokea Mungu. Kanisa linachukia dhambi, lakini linamkumbatia na kumhurumia mdhambi ili aweze kutubu na kumwongokea Mungu. Waamini wanapaswa kushinda kishawishi cha kuwakumbatia wadhambi na kuhalalisha dhambi zao, huu ni ugonjwa na fedheha kubwa kwa Kanisa. Wakristo wasimame kidete kupambana na vishawishi na nafasi za dhambi; lakini wajenge madaraja ya kukutana na wadhambi, ili wapate kutubu na kumwongokea Mungu.

Askofu mkuu Ruwwaichi anaendelea kukazia umuhimu wa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujipatanisha na Mungu ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Waamini wafanye upatanisho katika nafsi zao; jirani, watu, jamii na mazingira; wajipatanishe na Mwenyezi Mungu kwa kukimbilia kwenye kiti cha huruma na upendo wa Mungu. Kwa namna ya pekee, Askofu mkuu Ruwaichi anawaalika Wakristo kuonesha upendo na mshikamano na Wakristo wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; wakristo wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake; Wakristo wanaonyimwa uhuru wa kuabudu hasa huko Somalia, Mashariki ya Kati, Iraq, Syria, Pakistan na sehemu mbali mbali za dunia ambako madhulumu na nyanyaso hizi zinafanyika katika ukimya na usiri mkuu. Lengo ni kuonesha mshikamano na Kanisa linaloteseka pamoja na wale wote wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.