2016-03-23 08:41:00

Changamoto ya wakimbizi Barani Ulaya!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo sehemu mbali mbali za dunia; changamoto ya wakimbizi Barani Ulaya; majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam nchini Ufaransa pamoja na maadhimisho ya Siku ya thelathini na moja ya Vijana Duniani, Jimbo kuu la Cracovia ni kati ya mambo yanayojadiliwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa katika kikao chake kilichofunguliwa, hapo tarehe 15 Machi 2016 huko Lourdes, Ufaransa.

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Askofu Georges Pontier amewakumbuka Wakristo wanaishi undani wa Fumbo la Pasaka kutokana na madhulumu, nyanyaso na mauaji wanayotendewa Wakristo huko Iraq, Syria, Nigeria na baadhi ya Nchi Barani Afrika na Asia. Amezungumzia kuhusu wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha Barani Ulaya, lakini kwa bahati mbaya wanakumbana na pazia la chuma. Hawa ni watu wanaokimbia vita, umaskini na majanga asilia pamoja na vitendo vya kigaidi.

Askofu Georges Pontier anasikitika kusema kwamba, kuna watu wanaofanya vitendo vya kigaidi kwa kisingizio cha misimamo mikali ya kidini, hali inayochafua amani, usalama na mafungamano ya kijamii. Maaskofu Katoliki Ufaransa wanaushauri Umoja wa Ulaya kuwa na jicho la huruma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi Barani Ulaya, changamoto na mwaliko wa kuvuka utaifa na ubinafsi usiokuwa na mashiko na badala yake waoneshe mshikamano wa dhati na watu ambao maisha yao yako hatarini. Wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa utu wao kama binadamu na wala si bidhaa sokoni!

Askofu Pontier anasema, majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi ni muhimu sana miongoni mwa Wakristo na waamini wa dini ya Kiislam nchini Ufaransa; ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu hasa kutokana na vitisho vya vitendo vya kigaidi vinavyosababishwa na baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya kidini. Mashambulizi ya kigaidi yaliyoitikisa Ufaransa kunako mwaka 2015 ni changamoto kubwa katika ushuhuda wa imani. Wasi wasi wa mashambulizi ya kigaidi isiwe ni chanzo cha kufisha uhuru wa kuabudu. Lakini waamini wa dini zote wanapaswa kuwajibika katika kukuza na kudumisha uhuru wa kidini kwa kuwajibika barabara!

Askofu Pontier ameonesha wasi wasi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kutokana na athari za myumbo wa uchumi kitaifa, hasa miongoni mwa wakulima nchini humo wanaotaka kuendeleza uzalishaji katika sekta ya kilimo kwa kulinda na kutunza mazingira, lakini bado wanakumbana na hali ngumu ya maisha inayowakatisha tamaa. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwamba, makubaliano yaliyofikiwa na Jumuiya ya Kimataifa huko Paris, Ufaransa wakati wa mkutano wa athari za mabadiliko ya tabianchi, COP21 utasaidia mchakato wa ekolojia endelevu ili kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira bora nyumba ya wote!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linawaalika na kuwahamasisha vijana kuanza kujiandaa kikamilifu, ili hatimaye, waweze kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yatakayotimua vumbi Jimbo kuu la Cracovia mwishoni mwa mwezi Julai 2016, kwa ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Hii itakuwa ni Jubilei ya vijana katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu.

Maaskofu wamegusia pia matatizo, changamoto na fursa ambazo vijana wanakumbana nazo katika safari ya maisha yao ya kila siku, kiasi kwamba, wengi wao wanashindwa kufanya maamuzi magumu ya kuanza kujenga familia inayosimikwa katika Sakramenti ya ndoa! Matokeo yake ni uchumba sugu! Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki kwamba, Serikali ya Ufaransa itaweza kuibua sera na mikakati makini kwa ajili ya kuwasaidia vijana kuendeleza maisha, kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.