2016-03-23 09:37:00

Benin mfano bora wa kuigwa kwa demokrasia Barani Afrika!


Wananchi wa Benin wamemchagua Bwana Patrice Talon kuwa Rais mpya wa Benin baada ya kuibuka kidedea katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumapili iliyopita, tarehe 20 Machi 2016 na kujipatia asilimia 65% ya kura zote halali zilizopigwa nchini humo! Waziri mkuu mng’atuka Lionel Zinsou amempigia simu Rais mteule Patrice Talon na kumpongeza kwa kushinda katika uchaguzi mkuu na kwamba, atashirikiana naye katika kipindi hiki cha mpito pamoja na kuendelea kudumisha haki, amani, ustawi na maendeleo ya wananchi wa Benin.

Rais mteule Patrice Talon mwenye umri wa miaka 57 anafahamika na wengi kutokana na umaarufu wake kwenye biashara ya pamba nchini Benin na kwamba, sasa amepewa nafasi na umma wa wananchi wa Benin kumrithi Rais Thomas Boni Yayi anayemaliza kipindi chake cha uongozi kwa awamu mbili. Wachunguzi wa masuala ya kisiasa Barani Afrika wanasema, ushindi wa Bwana Talon Benin ni muhimu sana si tu nchini mwake, bali hata kwa Afrika katika ujumla wake.

Huu ni uchaguzi ambao umefanyika kwa kuzingatia misingi ya haki, amani, usawa, uhuru na ukweli na hata wale wapinzani walioshindwa wameridhika na mchakato mzima wa uchaguzi, ndiyo maana wanapongezana, tayari kushirikiana kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, tofauti kabisa na chaguzi zilizofanyika katika baadhi ya nchi za Kiafrika, kwa wapinzani kususia uchaguzi au mchakato mzima kugubikwa na vurugu na fujo zisizokua na mashiko wala mvuto kwa ustawi na maendeleo ya wengi.

Rais Boni Yayi anaongezwa na wengi kwa kuheshimu na kuzingatia Katiba ya nchi inayompatia dhamana ya kuweza kuongoza kwa vipindi viwili na baadaye kuachia ngazi, ili mwananchi mwingine aweze kuongoza! Mwelekeo huu ni tofauti na hali iliyojitokeza Burundi kwa Serikali kupindisha Katiba; Uganda kwa Rais kuendelea kung’angania madarakani au Congo, Brazzaville kwa Rais kupindisha Katiba ili aendelee kubaki madarakani, mambo ambayo yanadumaza demokrasi na misingi ya utawala bora Barani Afrika!

Rais mteule Patrice Talon wakati wa kampeni amesema, ataanzisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba, ili kupunguza madaraka ya Rais kwa kukuza na kuimarisha demokrasia shirikishi sanjari na kujali Katiba ya nchi. Anataka kukuza na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa watu kujieleza pamoja na demokrasia makini. Lakini Benin inakabiliwa na changamoto ya umaskini mkuwa miongoni mwa wananchi wake, idadi kuwa ya vijana wasiokuwa na fursa za ajira pamoja na kiwango cha chini kabisa cha elimu ambayo haikidhi mahitaji ya mchakato wa maendeleo endelevu nchini Benin.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.