2016-03-22 12:25:00

Tukio la kihistoria linalozika uhasama wa vita baridi!


Rais Barack Obama wa Marekani, Jumatatu tarehe 21 Machi 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Raul Castro wa Cuba; wote wawili wameonesha yale yanayozikera nchi zao na kutaka kuanza mchakato wa mapambazuko ya mwanzo mpya wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba, mchakato ulioanza kwa Rais Obama na Raul Castro kukutana, tayari kuanza kuandika ukurasa mpya unaovunjilia mbali kinzani za vita baridi kati ya Marekani na Cuba!

Haki msingi za binadamu na ufutwaji wa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba na ukuzaji wa demokrasia pamoja na kufungwa kwa Gereza la Guantanamo ni kati ya mambo yaliyopewa uzito wa juu wakati wa mazungumzo ya viongozi hawa wawili. Vikwazo vya uchumi anasema Rais Castro ni kikwazo kikubwa cha ukuaji na maendeleo ya wananchi wa Cuba. Ameitaka Serikali ya Marekani kurudisha Gereza la Guantanamo kwa Cuba kwani ni mali ya Serikali ya Cuba.

Rais Obama kwa upande wake amefafanua kwamba, bado kuna tofauti kubwa katika mchakato wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Marekani na Cuba, kumbe huu ni mwanzo wa mapambazuko mapya ya mahusiano haya. Marekani inaitaka Serikali ya Cuba kukoleza na kudumisha demokrasia kwa kuwaachia huru wafungwa wa kisiasa. Amekaza kusema, hatima na mustakabali wa maisha ya wananchi wa Cuba yako mikononi mwao wenyewe. Marekani inapania kufuta vikwazo vya kiuchumi kwani havikusaidia kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa nchi hizi mbili katika kipindi chote cha miaka 50 ya uwepo wake!

Rais Obama katika ziara yake ameandamana na wafanyabiashara wanaotumaini kuwekeza vitega uchumi vyao nchini Cuba, mara tu vikwazo vya kiuchumi vitakapong’olewa na Serikali ya Marekani. Kampuni ya Google inataka kuwekeza katika mitandao ya internet ili kurahisisha mawasiliano nchini Cuba kwa bei nafuu. Rais Raul Castro anaendelea kufanya mageuzi ya kiuchumi na kijamii nchini Cuba, ingawa Serikali ya Marekani inaitaka Cuba kupiga hatua kubwa zaidi, kabla ya kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.