2016-03-21 07:12:00

Vita Syria haina tija wala mashiko!


Monsinyo Richard Gyhra, afisa mwandamizi wa mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko mjini Geneva, hivi karibuni akichangia kwenye mkutano kuhusu Syria, amekazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujikita katika majadiliano kwani kwa sasa wananchi wengi wa Syria wanajiona si mali kitu; kuna uvunjaji mkubwa wa sheria na haki msingi za binadamu na kwamba, hata sheria za kimataifa hazithaminiwi tena.

Raia wanaendelea kushambuliwa kila kukicha, kumbe, mwendelezo wa majadiliano ya kisiasa ni alama ya matumaini kwa wananchi wengi wa Syria kwa wakati huu. Wanasiasa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuguswa na mahangaiko ya wananchi wa Syria tayari kushiriki majadiliano yanayopania ustawi na maendeleo ya wananchi wa Syria katika umoja wao! Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa pamoja na wadau wa mgogoro wa kivita nchini Syria kusitisha mapigano, ili kuokoa maisha ya wananchi wengi wa Syria, tayari kuambata amani na utulivu kwa ajili ya mafao ya wengi. Vinginevyo wananchi wa Syria wataendelea kukumbwa na maafa pamoja na majanga ya kila aina.

Ili kweli amani ya kudumu iweze kupatikana na kushamiri katika akili na nyoyo za watu, kuna haja ya kuanza pia mchakato wa upatanisho na ujenzi wa misingi ya haki, amani na utulivu, kwa kuzihusisha pande zote zinazohusika na mgogoro huu na kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa pia kutekeleza dhamana na wajibu wake, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Ukanda wa Mashariki ya Kati. Maamuzi yatakayopatikana katika majadiliano haya hayana budi kujikita katika misingi ya sheria, haki, uhuru pamoja na kuheshimu haki msingi za binadamu.

Wananchi wa Syria pia wanapaswa kuheshimiana na kuthaminiana na kwamba, tofauti zao ni utajiri unaopaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Wananchi watambue na kudumisha haki zao msingi. Upatanisho utaweza kuzaa matunda yanayokusudiwa, ikiwa kama wakimbizi na wahamiaji wataruhusiwa kurejea tena nchini mwao, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi na upatanisho wa nchi yao. Vatican itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria.

Ujumbe wa Vatican unakaza kusema, suluhu ya kisiasa itapatikana pale tu, kutakapokuwepo ulinzi wa raia na mali zao; haki msingi; maisha, utu na heshima ya binadamu vitakapoheshimiwa na kuthaminiwa. Ni matumaini ya wapenda amani duniani kwamba, kusitishwa kwa makombora huko Syria ni mwanzo mwema wa kumalizika kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imedumu kwa miaka mitano sasa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.