2016-03-21 08:51:00

Obama atinga timu Cuba!


Rais Barack Obama wa Marekani Jumapili tarehe 21 Machi 2016 amewasili nchini Cuba kwa ziara ya siku tatu, kama sehemu ya mchakato wa kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia yaliyosuasua kwa miaka takribani miaka 50. Rais Obama anaweka historia ya kutembelea Cuba baada ya kupita miaka 88, Rais Calvin Coolidge wa Marekani alipotembelea Cuba kwa mara ya mwisho, yaani kunako mwaka 1928.  Uwanja wa ndege, Rais Obama amelakiwa na viongozi wa ngazi za juu kutoka Cuba.

Rais Obama na Raul Castro wa Cuba wamekuwa ni chachu ya mageuzi ya mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili na kwamba, mahusiano wa kiuchumi pole pole yanaanza kushika kasi. Rais Obama na familia yake, Jumapili wametembelea Havana ya zamani na kushangaliwa na maelfu ya wananchi wa Cuba. Mambo makuu mawili ambayo Rais Obama anapenda kuyapatia kipaumbele cha kwanza uhusiano wa kiuchumi na uhuru wa wananchi, ili kuendelea kusaidia mchakato wa mageuzi ya kiuchumi yaliyoanzishwa na Rais Castro kunako mwaka 2008.

Vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Cuba vimedumu kwa takribani miaka 54, lakini walioumia zaidi na wananchi wa kawaida. Rais Obama akiwa nchini Cuba atazungumza na Rais Raul Castro wa Cuba; wafanyabiashara. Atazungumza kwa faragha na baadhi ya wananchi wa Cuba; atazungumza na wananchi wa Cuba kwa njia ya Televisheni ya Taifa na kuhudhuriaonesho la mchezo wa Baseball, Jumanne, tarehe 22 Machi 2016.

Akiwa mjini Havana, Rais Obama na família yake walitembelea Kanisa kuu la Jimbo kuu la Havana, Cuba lililojengwa kunako karne ya 18. Amezungumza na Kardinali Jaime Ortega aliyeshiriki kikamilifu katika majadiliano ya kidiplomasia yaliyopelekea Marekani na Cuba kurejesha tena mahusiano ya kidiplomasia. Obama na família yake wamepata chakula cha usiku kwenye Hoteli binafsi, matunda ya mageuzi ya kiuchumi yaliyofanywa na Rais Raul kwa kukazia umuhimu wa sekta binafsi kuchangia katika ustawi na maendeleo ya nchi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.