2016-03-21 14:11:00

Muhtasari wa Ujumbe wa Maaskofu Katoliki Tanzania!


Mpendwa msikilizaji wa Kipindi cha Hazina yetu, Tumsifu Yesu Kristo. Tupo ndani ya Juma Kuu ambapo tunatafakari kwa kina babisa fumbo la mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Baada ya safari ya siku 40 ya mfungo wa Kwaresma; tunatazamia tumaini lenye heri la kufufuka pamoja na Kristo. Mama Kanisa Mtakatifu daima hutuhimiza kuusindikiza mfungo wetu wa Kwaresma kwa kusali, kufunga/kujinyima na kuwapa maskini. Pamoja na lishe mbalimbali za kiroho ambazo tulizipokea kutoka kwa wachungaji wetu, kwa safari hii; tulisindikizwa pia na Ujumbe  wa Kwaresma kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ambao tulikusomea neno kwa neno.

Na leo mpendwa msikilizaji, tunapenda kukuletea muhtasari wa yale tuliyoyasikia katika ujumbe huo ili tuweze kukazia maarifa.  Tutakumbuka kwamba, ujumbe wa Kwaresma tuliousikia kwa kiasi kikubwa umeunganika-mkabala na maudhui nzima ya maadhimisho ya Jubilei ya  Mwaka  Mtakatifu wa  wa Huruma ya Mungu. Katika ujumbe ule wa Kwaresma, wenye kichwa cha habari “Iweni na Huruma kama Baba yenu alivyo na huruma”, wahashamu maaskofu wetu wamependa tufahamu undani kabisa wa wito wetu wa ukristo na wajibu wetu wa kuimwilisha huruma ya Mungu katika maisha yetu ya kila siku na katika nyanja zote za maisha yetu kama wakristo.

Katika Sura ya kwanza maaskofu wetu wameanza ujumbe wao kwa kututambulisha sura ya Mungu wetu. Wanatufundisha kuwa,  Mungu wetu aliye mwenyezi,  ni Mungu mwenye  kuhurumia na kusamehe, kwa sababu yeye ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli, mwenye kusamehe uovu, makosa na dhambi. Na Mungu anatuonea huruma sisi wanadamu ili tumjue na tupate kuwa wanyoofu. Ni mwaliko kwa waana wa Mungu, kuvaa moyo wa huruma na rehema ili kweli tufanane na Baba yetu wa Mbinguni. Maaskofu wetu wanaendelea kutueleza juu ya mafaa ya huruma ya Mungu. Kwa huruma yake kuu, Mungu wetu hutufariji mfano wa mama kwa mwanaye. Kwa huruma yake kuu hutulinda kama tai alindavyo watoto wake. Ni wajibu wetu sisi kujiaminisha mikononi mwa Mwenyezi Mungu na kukimbilia daima tunza yake ya kibaba, na tutakuwa salama.

Katika sura ya pili, maaskofu wetu wametufundisha juu ya ufunuo wa huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu imejifunua kwetu kwa njia ya Uumbaji, pili kwa njia ya ukombozi baada ya anguko la kwanza la wazee wetu Adamu na Eva. Mungu alidhihirisha huruma yake kwa kumtafuta mwanadamu mkengeufu. Huruma ya Mungu iliendelea kujidhihirisha pale alipoandaa taifa teule kwa njia ya Mababu zetu Ibrahimu, Isaka na Yakobo. Aliahidi ukombozi, uhuru na usitawi kwa watu wake endapo watalishika Agano lake na akaendelea kujidhihirisha kwa njia ya Manabii. Na mwisho huruma hiyo kuu ya Mungu imedhihirika katika Nafsi ya Mwanawe mpendwa, pale alipofanyika mwili na akakaa kwetu.

Huruma ya Mungu ikaendelea kujidhihirisha katika  mafundisho ya Kristo, maisha yake, miujiza yake na mifano yake; na mwisho katika mateso, kifo na ufufuko wake. Bado haikuishia hapo, huruma ya Mungu iliendelea kujidhihirisha katika ahadi ya Kristo ya kumleta  Roho Mtakatifu mwenye kutukumbusha na kutufundisha kweli zitakazotuelekeza katika njia ya uzima. Ni mwaliko kwetu kumsikiliza na kumtii Roho Mtakatifu anayeongea ndani mwetu na anayeongea ndani ya Kanisa kwa njia ya mamlaka halali za Kanisa. Tuitii sauti ya wachungaji wetu, ili ituelekeze kufika mbinguni.

Katika sura ya tatu, maaskofu wetu wanatufundisha kuwa Kanisa kama Taifa na Familia ya Mungu, ni wakala wa upendo na huruma ya Mungu. Hivyo sisi tulio waana wa Kanisa ni mawakala wa upendo na huruma ya Mungu. Na kwa vile huruma ya Mungu huwandea wanadamu wote, basi watu wote wenye mapenzi mema, wanaitwa kuwa mawakala wa huruma na upendo wa Mungu.  Hapa sote tunaalikwa kujichunguza, kuongoka na kuuvaa utume huu wa kuifahamu, kuiishi na kuitangaza huruma ya Mungu.

Wahashamu Maaskofu wetu katika sura hii ya tatu wanaendelea na ujumbe wao kwa kutualika sisi waamini wote kuuambata wajibu wetu wa kuitangaza habari njema. Tunaalikwa kumtangaza Kristo popote katika mazingira yetu ili afahamike, apendwe na afuatwe na wote. Ni mwaliko kwetu kuyasoma, kuyajifunza, kuyaishi na kuyatangaza mausia ya Injili Takatifu.

Kila mtu anaitwa na kutumwa kuwa mtangazaji wa ujumbe wa Injili. Na kila mtu kwa kiwango chake anaweza kutangaza ujumbe wa Injili. Tufanye hivyo kwa maneno, kwa matendo, na kwa njia ya uandishi. Hapa tunakazia maarifa; mpendwa msikilizaji, tumia njia zote sahihi za kuweza kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu kwa mwenzako. Leo hii kuna maendeleo makubwa sana ya sayansi ya mawasiliano. Hiyo simu yako mpendwa msikilizaji pamoja na vyombo vyote vya mawasiliano,  hakikisha vinakusaidia kutanganza Neno la Mungu. Kila mara tuma ujumbe wa faraja, imani, matumaini, mapendo na huruma.

Pamoja nalo, maaskofu wetu wamegusa pia kipengele nyeti cha mahusiano ndani ya familia, kwa kuwaalika wazazi kujenga mahusiano mwanana hati yao wenyewe; na pia mahusiano yenye afya kati yao na watoto wao. Kwa visingizio mbalimbali, wazazi wengi wanajiweka mbali na watoto wao. Watoto hao huonja uyatima, wazazi wao wakingali hai. Na pengine inakereketa zaidi pale ambapo magomvi ya kila sampuli yanatawala ndani ya familia. Nyumba iliyojaa upendo, huruma, uaminifu, uvumilifu, msamaha, kusaidiana, kuheshimiana na mambo mengine kama hayo; nyumba hiyo inatangaza huruma ya Mungu. 

Tusisahau kwamba, taifa lolote lile lenye amani, hujengwa na watu alioundwa katika familia zenye amani. Usitawi wa familia ndio usitawi wa taifa na Kanisa. Sala na neno la Mungu, vitasaidia kujenga dhamiri njema za wanafamilia. Hapo watafurahia umoja, amani na mshikamano wa daima. Na familia hiyo, kitakuwa ni kitalu cha kusitawisha watu wema wenye kuifaa jamii. Familia kama hiyo, hakika inatangaza huruma, upendo na utukufu mkuu wa Mungu, na itakuwa ni kao la Mungu. Kwa njia ya simu yako hamasisha upendo, msamaha, ukweli amani na uaminifu. Jitahidi kusimama kidete kupinga mambo yote yanayosaliti huruma ya Mungu kwa mwanadamu!

Mwisho Wahashamu Maaskofu wetu wanatualika kujibidisha kupokea Sakramenti za Kanisa. Kristo Bwana, ametuachia Sakramenti hizi, ili zitupatie neema za Wokovu. Ili kuifumbata zaidi huruma ya Mungu, tunaalikwa kukimbilia sakramenti ya Kitubio, tupate kuonjeshwa huruma na msamaha wa Mungu, na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu; ambamo sio tu tunapokea neema, bali tunampokea Kristo Mwenyewe aliye mtoaji wa neema tele. 

Ili kuzimwilisha neema hizo tunazojaaliwa na Kristo Mkombozi wa dunia katika Sakramenti tunazozipokea; tunaalikwa sote kujibidisha kutenda matendo ya huruma kimwili na kiroho. Matendo hayo ya huruma  ya kimwili ni: kuwalisha wenye njaa,  kuwanwesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwakaribisha wageni, kuwatembelea wagonwa, kuwasaidia wafungwa na kuwazika wafu. Na matendo ya huruma ya kiroho ni: kuwashauri wenye mashaka,  kuwafundisha wajinga, kuwafariji wenye huzuni, kuwaonya wakosefu, kusamehe makosa, kuwavumilia wasumbufu na kuwaombea wazima na wafu.

Tukiyafanya hayo, tutakuwa kweli na huruma kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo na huruma. Asante kwa kuitegea sikio Radio Vatican. Kukuletea makala hii kutoka katika Studi za Radio Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.