2016-03-21 14:22:00

Dr. Ali Mohamed Shein atangazwa kuwa mshindi Zanzibar!


Tume ya Uchaguzi Zanzibar, Jumatatu tarehe 21 Machi 2016 imemtangaza Dr. Ali Mohamed Shein kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar baada ya kushinda kwenye uchaguzi wa marudio tarehe 20 Machi 2016. Dr. Shein aliyekuwa anarusha bendera ya Chama cha Mapinduzi amepata asilimia 91.4% ya kura halali 328, 327 zilizopigwa Visiwani humo. Kura zilizoharibika ni 13, 538 ambayo ni sawa na asilimia 4% ya kura zote zilizopigwa.

Uchaguzi wa marudio Visiwani Zanzibar umerudiwa, tarehe 21 Machi 2016 baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika nchini Tanzania hapo tarehe 25 Oktoba 2015 kutokana na sababu kwamba, uchaguzi haukuwa huru na wa haki. Vyama vingi vya upinzani vimesusia uchaguzi wa marudio, hali ambayo inaweza kuviweka Visiwa vya Zanzibar njia panda!

Hivi karibuni viongozi mbali mbali wa dini waliwataka watanzania Visiwani Zanzibar kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano; kwa kuheshimiana na kupokeana na kwamba tofauti zao za kisiasa zisiwe ni chanzo cha vurugu na mpasuko wa kijamii. Bila amani anasema Askofu mkuu Yuda Thaddeus  Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania hakuna maendeleo wala utangamano wa kijamii unaowasaidia watu kupokeana kama walivyo na kuunganisha nguvu zao katika kushughulikia maendeleo yao kwa kuzingatia: haki,ukweli na mafao ya wengi.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi anakaza kusema, mambo haya yanapaswa pia kuzingatiwa na vyama vya kisiasa Visiwani Zanzibar. Vyama hivi kamwe visiwe ni wakala wa kujenga chuki, uhasama na uchochezi kati ya watu pamoja na mivutano isiyokuwa na tija wala mashiko. Hali tete Visiwani Zanzibar kwa kiasi kikubwa imechangiwa na vyama vyote vya Kisiasa Visiwani humo. Ikumbukwe kwamba, hatima ya Zanzibar inategemea vyama hivi kuzingatia: ukweli, haki, mafao ya wengi, Umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.