2016-03-20 11:26:00

Vijana dumisheni amani, umoja na udugu!


Baba Mtakatifu Francisko baada ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Jumapili ya Matawi, tarehe 20 machi 2016, amewashukuru na kuwapongeza vijana wote waliokuwa wamejiunga naye kwa njia ya vyombo mbali mbali vya mawasiliano ya jamii, lakini kwa namna ya pekee, vijana walioshiriki katika Ibada ya Misa Takatifu, Kanisa linapoadhimisha Siku ya XXXI ya Vijana Duniani, itakayofikia kilele chake huko Jimbo kuu la Cracovia kuanzia tarehe 26 – 31 Julai 2016. Siku hii inaongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, umati mkubwa wa vijana utaweza kuhudhuria na kushiriki katika maadhimisho ya kilele cha Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Poland, mahali alikozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II, muasisi wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Baba Mtakatifu anawaweka vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yohane Paulo II, wakati huu wa maandalizi ya siku hii muhimu ambayo inakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; Jubilei ya Vijana Duniani!

Kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, walikuwepo pia vijana watakaojitolea wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Cracovia, Poland. Wamekusanya matawi ya Mizeituni kutoka Yerusalemu, Assisi na Montecasino na kubarikiwa wakati wa mwanzo wa Ibada ya Misa, changamoto ya kujenga na kudumisha amani, upatanisho na udugu. Baba Mtakatifu anawataka vijana kusonga mbele wakiwa na matumaini haya. Wamwombe Bikira Maria ili awasaidie kuishi vyema Juma Takatifu, ili kuweza kufanya tafakari ya kina kuhusu: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.