2016-03-19 11:42:00

Wakuu wa mikoa wapya nchini Tanzania na changamoto zao!


Rais wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli amewapa siku 15 mawaziri, wakuu wa taasisi na wakuu wa mikoa ambao amewaapisha hivi karibuni Ikulu Dar es Salaam, kuhakikisha kuwa wafanyakazi ambao wanalipwa mishahara hewa wanaondolewa katika mfumo wa mishahara na iwapo hali hiyo itajitokeza mwisho wa mwezi Machi, wakurugenzi wa halmashauri husika watawajibishwa na kupelekwa mahakamani. Aidha, amewataka wakuu wa mikoa kutumia mamlaka yao kwa kuwaweka rumande watu ambao hawafanyi kazi kwa muda wa masaa 48 ili waweze kubadilika na kuweka bayana kuwa asiyefanya kazi asile.

Dk. Magufuli alisema katika uchunguzi aliofanya kwenye mikoa ya Singida na Dodoma ambapo walipitia Halmashauri 14 wamegundua uwepo wa wafanyakazi 202 ambao wanalipwa mishahara huku wakiwa hapo kazini jambo ambalo linaingizia serikali hasara kubwa. Alisema katika uchanguzi huo walibaini wafanyakazi 3,320 ambao hawakuwepo kazini kwa sababu mbalimbali hivyo upo uwezekano idadi hiyo ya wafanyakazi hewa ikaongezeka siku za karibuni.

Rais, Magufuli alisema kulingana uchunguzi huo ambao umefanyika katika halmashauri 14 ni dhahiri kama halmashauri zote 180 zitafanyiwa ukaguzi upo uwezekano wa kubaini zaidi ya wafanyakazi 2,000 ambapo watakuwa wanalipwa zaidi ya shilingi bilioni 2.5 kwa mwezi bila sababu yoyote. "Huwa baada ya kiapo hakuna utaratibu wa kuzungumza ila nimelazimika kufanya hivi kutokana na matatizo ambayo yapo katika mikoa yenu kwani tumeangalia katika Halmashauri 14 tumegundua wafanyakazi 202 ambao wanalipwa mishara hewa hivyo nawapa siku 15 kuanzia leo kuhakikisha hali hiyo inaisha na kama mtashindwa sitawaelewa," alisema.

Alisema wakurugenzi wa Halmashauri wanahusika na hali hiyo hivyo iwapo mwisho wa mwezi huu watapatikana watumishi hewa atawawajibisha na kuwapeleka mahakamani. Dk. Magufuli alisema agizo hilo kwa wakuu wa mikoa litawahusu mawaziri na wakuu wa taasisi kuhakikisha wanafanya uchunguzi na kuondoa watumishi katika ngazi za wizara na taazisi zao na kama itabainika kuwepo na hali hiyo watawajibishwa. Alisema inasikitisha kuona serikali inahangaika kukusanya fedha kwa ajili ya kutoa huduma za kijamii huku watendaji wengine wakishirikiana kulipa mishahara hewa kwa watu waliostaafu, walikufa, waliofukuzwa na walifungwa.

Rais, Magufuli watumishi wa serikali zaidi ya 500,000 ambapo kila mwezi wanalipwa zaidi ya sh, bilioni 550 hivyo ni lazima fedha hizo zitolewe kwa kufuata utaratibu sahihi ili fedha zingine ziweze kuhudumia jamii.Aidha, alisema serikali kwa mwezi ulipita umelipa madeni ya njee zaidi ya sh. bilioni 800 hivyo kinachohitajika ni kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika kwa mambo yanayowahusu moja kwa moja. Rumande: Kwa upande mwingine Rais Magufuli, amewataka wakuu wa mikoa kutumia mamlaka zao kwa kuwachukulia hatua wananchi ambao hawataki kufanya kazi hasa vijana ambao kila siku wanajihusisha na kucheza pool table. Alisema wakuu hao wana mamlaka ya kuweka rumande mtu yoyote kwa masaa 48 hivyo wanapaswa kufanya hivyo ili kurejesha nidhamu ya nchi ambayo imepotea kwa muda sasa.

Magufuli, alisema ametumia muda mrefu wa kutafakari aina ya wakuu wa mikoa anaowataka hivyo atasononeka iwapo watamuangusha na kuwaka wasiogope mtu hasa katika kusimamia haki. Alisema iwapo watafanya kazi kwa kufuata weledi na haki za binadamu ni dhahiri kuwa hakutakuwa na mtu ambaye atalalamika huku akiwasisitiza kuacha kufanya siasa na kinachotakiwa ni kufanya kazi tu. "Tusiogope kuchukua maamuzi hata kama maamuzi hayo ni mabaya naamini baadae tutayarekebisha kama yatakuwa yanahitajika ili kupeleka nchi yetu mbele," alisema.

Rais, alisema wapo watendaji kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa ambao wamekuwa wakifanya kazi kinyume na taratibu hivyo wakuu hao wa mikoa wanapaswa kuwasweka rumande kwa masaa 48 ili waweze kujifunza. Alisema iwapo watashindwa kuendana na kasi yake wajiandae kuwajibika huku akitolea mfano mgogoro wa wakulima na wafugaji Mkoani Morogoro umeshindwa kutatuliwa hivyo hakuona sababu ya kuendelea kubakia na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo Dk. Rajab Rutengwa.

Aidha, aliwataka wakuu hao wa mikoa kusimamia upatikanaji wa elimu bora, madawati na vitendeakazi mbalimbali ambavyo vitakuza elimu ya nchi. Magufuli alisema pia wakuu hao wanawajibu wa kusimamia huduma mbalimbali za kijamii ambazo zinazunguka katika maeneo yao huku akiwasisitiza kuwa wbunifu kwa kila mkoa kutumia rasilimali zake. Aidha rais aliwataka wakuu wa mikoa hao kuhakikisha kuwa suala la ukosefu wa chakula katika mikoa yao inatokea na kama ikitokea hawatakuwa na sifa za kufanya kazi na serikali yake.

TRA na Takukuru: Aidha Dk. Magufuli, alimtaka Kamshina wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kujipanga kwa ili kuhakikisha kuwa taasisi hizo zinaenda na malengo ya Watanzania. Alisema wananchi wanahitaji huduma za msingi zitekelezwe kwa kiwango kizuri hivyo ufanisi wake utapatikana kwa kuwepo ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya ya rushwa na ufisadi.

Wakuu wa mikoa Mwanri:  Akizungumzia nafsi hiyo ya kuteuliwa kuwa mkuu wa Mkoa wa Tabora Agrey Mwanri, alisema atahakikisha kuwa anaitumikia nafasi hiyo kwa uadilifu wa hali ya juu ili kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na hitaji la wananchi. Alisema mkoa huo unakabiliwa na changamoto nyingi ila kinachohitajika ni kuwepo kwa ushirikiano wa viongozi wote ili kuhakikisha maendeleo ya mkoa yanapatikana. Mwanri alisema, pia anatarajia kusimamia miradi mbalimbali ambayo imekuwa katika utekelezaji ili kuhakikisha kuwa inakuwa na thamani inaayoendana na fedha iliyotolewa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Kebwe Stephen Kebwe, alisema amejipanga kuhakikisha kuwa anakabiliana na changamoto zinazowakabili wananchi wa Morogoro hasa migogoro ya wakulima na wafugaji. Alisema ataanza kwa kutumia taarifa mbalimbali ambazo zimefanywa na watangulizi wake ili kupata urahisi wa kutatua migogoro hiyo na kuwasaidia wananchi kufanya kazi kwa uhuru. "Natambua changamoto mbalimbali ambazo zipo mkoa wa Morogoro nimejipanga kukabiliana nazo kwa kushirikisha wadau mbalimbali ambao kwa njia moja au nyingine wanahusika," alisema.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Meja Jenerali Mstaafu, Raphael Muhuga, alisema changamoto ya ujambazi na uhalifu unaotokea katika mkoa huo atapambana nazo kwa kushirikisha vyombo vyote vya usalama. Muhuga, alisema iwapo vyombo hivyo vitashirikiana na wananchi ni dhahiri ujambazi na uhalifu wowote ambao unafanyika barabarani na majumbani utaweza kudhibitiwa kwa haraka. "Ni kweli changamoto zipo lakini natarajia kushirikiana na vyombo vyote vya usalama na wananchi ili kubaini njia ya kutatua matukio yote ambayo yanaukabili mkoa," alisema.

 Kwa upande wake Kamishna wa TRA, Alphayo Kidata, alisema katika kuhakikisha kuwa mamlaka hiyo inaongeza mapato wanajipanga kutoa elimu zaidi kwa mwananchi kulipa kodi ambapo kwa sasa wanaendelea na operesheni ya kuhamasisha matumizi ya machine za IFD. Alisema wananchi wengi hawana uelewa kuhusu dhana nzima ya ulipaji kodi hali ambayo inakosesha serikali mapato mengi hivyo huduma za kijamii kuonekana kutotekelezwa. "Kumekuwepo na changamoto mbalimbali za ukusanyaji mapato lakini tunatarajia kupitia elimu ya mlipa kodi hali itabadilika na mfano ni ongezeko la ukusanyaji wa mapato kuanzia mwezi Desemba hali inaenda vizuri," alisema. Alisema lengo la TRA, ilikuwa ni kukusanya trilioni 12.5 ambapo matarajio ni hadi kufikia Juni 30 hali makusanyo hayo yatakuwa yamefikiwa kwa asilimia 100.

Mkurugenzi Mpya wa Takukuru, Valentino Mlowola, alisema amejipanga kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanaongezeka hivyo ni vema kwa mtu yoyote anayefikiria rushwa akaacha kwani hatapona. Mlowola, alisema pamoja na mapambano ya rushwa Takukuru inajipanga kuendeleza vita ya ufisadi hapa nchini kwa kufuatilia nyendo zoto za watu ambao wapo katika mamlaka za serikali. 

Katika mchakato huo wa uapishaji wakuu wa mikoa na wakurugenzi hao Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Zelote Steven, alionesha ukakamavu wakati akielekea kula kiapo hali ambayo iliibua vicheko kwa wananchi na viongozi ambao walihudhuria hafla hiyo. Aidha Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shegela, alionesha kutetemeka wakati wa kula kiapo hali ambayo ilitajwa kuwa inatokana na upya wake kwenye nafasi hiyo.

Katika hafla hiyo ya kiapo ambayo ilichukua takribani saa moja Rais, Magufuli alionekana mwenye sura ya kazi kwani hakuweza kucheka muda wote hadi mla kiapo wa mwisho Mlowola alipomaliza kiapo na kuondoka na viapo hali ambayo ilibua kicheko hadi Rais mwenyewe. Wakuu wa Mikoa walioapishwa ni Meja Jeneral Mstaafu Ezekiel Elias Kyunga, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Meja Jenerali Mstaafu Salum Mustafa Kijuu Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Brigedia Jeneral Mstaafu Emmanuel Maganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma.

Wengine n: Godfrey Zambi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Dkt. Steven Kebwe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kamishna Mstaafu wa Polisi Zelote Steven Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Anna Malecela Kilango Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Methew Mtigumwe, Mkuu wa Mkoa wa Singida. Wengine ni: Antony Mataka Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Aggrey Mwanri Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Martine Shigela Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Jordan Mungire Rugimbana, Mkuu wa Mkoa Dodoma, Said Meck Sadick – Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Magesa Mulongo, Mkuu wa Mkoa Mara, Amos Gabriel Makalla Mkuu wa Mkoa Mbeya, John Vianey Mongella Mkuu wa Mkoa Mwanza.

Wengine ni: Daudi Felix Ntibenda Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amina Juma Masenza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Joel Nkaya Bendera Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Halima Omary Dendegu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Rehema Nchimbi Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhandisi Evarist Ndikilo Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Said Thabit Mwambungu Mkuu wa Mkoa Ruvuma. Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luten Mstaafu Chiku Galawa hajaapishwa hivyo wakuu wa mikoa walioapishwa ni 25 na wakurugenzi wawili mmoja kutoka TRA na Takukuru.

Na mwandishi maalum, Dar es Salaam.








All the contents on this site are copyrighted ©.