2016-03-19 08:20:00

Jimbo la Skopje lafungua makao mapya ya Askofu na Kituo cha kichungaji!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameanza safari yake ya kikazi nchini Macedonia, iliyokuwa Yugoslavia ya zamani, Ijumaa, tarehe 18 Machi 2016 kwa kufungua Makao makuu ya Askofu wa Jimbo Katoliki la Skopje pamoja na kituo cha shughuli za kichungaji jimboni humo, kielelezo makini cha umoja na mshikamano katika mchakato wa ujenzi wa mji wa binadamu, ili kusikiliza kwa makini matatizo, changamoto, fursa na matumaini ya familia ya Mungu Jimboni Skopje.

Mji wa Skopje umekarabatiwa upya baada ya maafa yaliyotokea kunako mwaka 1963, mji ambao kwa sasa una mwelekeo mpya wenye utajiri mkubwa wa kihistoria na maisha ya kidini; makutano ya tamaduni kutoka Ulaya na Asia; mwaliko wa kushuhudia na kudumisha mapokeo ya wananchi hawa katika historia yao. Kardinali Parolin anawapongeza kwa kujenga na kudumisha umoja na udugu; uelewano na ushirikiano; kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi kwa kuvuka kuta za kitamaduni na kidini.

Kanisa Katoliki kwa upande wake linaendelea kushiriki kikamilifu katika maisha na vipaumbele vya watu; kwa kuheshimu na kutetea Injili ya uhai; utu na heshima ya binadamu; haki na usawa; mshikamano na mafao ya wengi. Kanisa linapania pamoja na mambo mengine kuendelea kushirikisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu, ili kudumisha amani na utulivu katika maisha ya kijamii sanjari na kushiriki katika mchakato wa maendeleo endelevu kati ya watu.

Kardinali Parolin anakaza kusema, katika ulimwengu mamboleo, mwanadamu anakabiliana na changamoto ya umaskini wa hali na kipato; mmong’onyoko wa kimaadili na utu wema. Kanisa linapenda kushiriki katika kuwasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupambana na hali hii inayodhohofisha ustawi na maendeleo ya wengi: kiroho na kimwili. Linataka kuwekeza katika majiundo makini ya kimaadili na utu wema; kwa kushirikiana na waamini wa dini mbali mbali, ili kuweza kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani haki, amani na umoja wa kitaifa!

Kardinali Parolin amemtaja Mama Theresa wa Calcutta ambaye katika maisha yake amejipambanua kuwa kweli ni mmissionari wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Leo hii, Bara la Ulaya linakabiliwa na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha yao, lakini kwa bahati mbaya wanakumbana na pazia la chuma! Hapa Baba Mtakatifu Francisko aliwahi kushauri kwamba, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ishughulikiwe kimataifa na kamwe wasiliachie taifa moja tu, kama inavyoonekana kwa sasa!

Jumuiya ya Kimataifa itoe suluhu ya kudumu na endelevu badala ya mwelekeo wa sasa wa kila taifa kujichukulia maamuzi yake yanayojikita katika ubinafsi na utaifa usiokuwa na mashiko kwa wengi! Watu wananyimwa haki zao msingi, wanapotafuta usalama na hifadhi ya maisha Barani Ulaya.

Kardinali Pietro Parolin, anampongeza Askofu mahalia kwa kutaka kuyafanya makazi ya Askofu na Kituo cha shughuli za kichungaji kuwa kweli ni mahali pa ukarimu; eneo la upendo wa kidigu, ushirikiano na mshikamano. Ni mahali ambapo waamini wataweza kujenga mahusiano na Mungu kwa njia ya Neno la Sakramenti za Kanisa. Hapa ni mahali ambapo Jumuiya ya Kikatoliki itakutana na kuadhimisha mafumbo ya Kanisa, tayari kujibu kilio cha ndani kabisa cha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ni mahali ambapo familia zinatarajia kupata majiundo makini na endelevu; wazee na wagonjwa kupata faraja sanjari na kuibua sera na mikakati ya kitamaduni na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kardinali Parolin anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliochangia kwa hali na mali katika mchakato wa ujenzi wa Makao makuu ya Askofu na Kituo cha shughuli za kichungaji Jimbo Katoliki la Skopje, huko Macedonia, iliyokuwa Yugoslavia ya zamani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.