2016-03-19 14:53:00

Dhamana ya Askofu: Kufundisha, kuongoza na kutakatifuza!


Askofu anao wajibu na dhamana ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa kutambua kwamba, Kristo ndiye mchungaji mkuu anayeunda na kuliongoza Kanisa; Kristo  ndiye nguzo na mhimili mkuu wa Kanisa lake. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu wao kadiri ya mipango ya Kristo mchungaji mwema! Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, mume wa Bikira Maria, Jumamosi tarehe 19 Machi 2016.

Baba Mtakatifu Francisko ametumia maadhimisho haya kufanya kumbukumbu ya miaka mitatau tangu alipoanza rasmi utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kuwaweka wakfu Monsinyo Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini na Monsinyo Peter Bryan Wells Balozi wa Vatican kusini mwa Afrika kuwa maaskofu. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake anakaza kusema, Yesu Kristo baada ya kutumwa na Baba yake wa mbinguni, aliteuwa Mitume kumi na wawili, wakiwa wamejawa na nguvu ya Roho Mtakatifu akawatuma kwenda duniani kutangaza na kushuhudia Injili sanjari na kuwajenga watu wote chini ya mchungaji mmoja, anayetakatifuza, anayefundisha na kuongoza. Kwa njia hii aliwapatia dira na mwelekeo kwenye wokovu!

Mitume walipewa dhamana ya kuhakikisha kwamba, wanaendeleza utume huu kizazi baada ya kizazi, kwa kuwachagua waandamizi wao na kuwawekea mikono, ili kupokea zawadi ya Roho Mtakatifu na kwa njia hii, akaiweka Sakramenti ya Daraja Takatifu. Mitume wameendeleza dhamana hii na kwamba, Maaskofu ni waandamizi wa mitume mintarafu Mapokeo hai ya Kanisa wanaoendeleza kazi ya ukombozi na utume ulioanzishwa na Kristo Yesu. Askofu akiwa amezungukwa na wakleri wake, Kristo Yesu, yuko kati kati yao, kwani Yeye ndiye Kuhani mkuu na wa milele!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, ni Kristo kwa njia ya Maaskofu wake anaendelea kuhubiri Injili ya Wokovu; anaendelea kuwatakatifuza watu wake kwa njia ya Sakramenti za Kanisa, chemchemi ya imani. Kristo kwa njia ya Askofu analijalia Kanisa kupata watoto wapya wanaokuwa na kuendeleza Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Ni kwa njia ya hekima na unyenyekevu wa Askofu, Kristo anaendelea kuwaongoza waamini wake wanaofanya hija ya maisha yao ya kiroho, kuelekea maisha ya uzima wa milele. Kwa ufupi, Baba Mtakatifu anasema, Kristo anafundisha, anaongoza na kuwatakatifuza waja wake. Hiki ndicho kielelezo cha Askofu.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwapokea na kuwashangilia Maaskofu wapya waliowekwa wakfu na kuingia katika hurika wa Maaskofu. Wapewe heshima kadiri ya dhamana na nafasi yao ndani ya Kanisa, kwani wao ni mashuhuda wa Injili. Maaskofu wenyewe watambue kwamba, wameteuliwa kutoka kati ya watu kwa ajili ya watu katika mambo matakatifu yamhusuyo Mungu. Uaskofu ni daraja la huduma kadiri ya amri na maagizo ya Kristo mwenyewe. Maaskofu wajitahidi kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huduma makini kwa familia ya Mungu. Wanapewa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu, kwa kukanya na kuonya pamoja na kuhimiza mafundisho ya Kanisa. Maaskofu wawe ni watu wa sala na tafakari ya Neno la Mungu; linalomwilishwa katika maisha na kushuhudiwa katika utekelezaji wa mikakati ya kichungaji.

Maaskofu wahakikishe kuwa wanakuwa ni wahudumu, watunzaji na waadhimishaji bora wa Mafumbo ya Kanisa; kwani wao ni wakuu wa familia ya Mungu iliyodhaminishwa kwao. Maaskofu wawe ni wachungaji wema, wanaowatambua watu wao kwa majina na sura zao. Waoneshe upendo wa dhati kwa watu wa Mungu pamoja na kutoa muda wa kukutana na kuzungumza na waamini wao. Maaskofu wawe karibu na wakleri wao kwani hawa ni wasaidizi wao wa karibu katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Maaskofu watoe kipaumbele cha pekee kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezomi mwa jamii, kwani hawa ni walengwa wa kwanza wa Habari Njema ya Wokovu! Maaskofu waoneshe moyo wa upendo kwa wote. Kwa njia ya kifungo cha upendo, wajitahidi kushikamana na kushirikiana na Maaskofu wenzao, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima, hasa yale Makanisa yenye uhitaji mkubwa zaidi!

Maaskofu wawaongoze watu wao kwa kutambua kwamba, wanatekeleza dhamana na wajibu huu kwa niaba ya Roho Mtakatifu aliyetumwa na Kristo na kwamba, wao ni walimu,  makuhani na wachungaji wema. Ni Roho Mtakatifu anayewasaidia na kuwanyanyua kutoka katika udhaifu wao wa kibinadamu. Kristo aliyewachagua anahitimisha Baba Mtakatifu mahubiri yake, awaongoze katika njia ya utakatifu wa maisha, waliyoianza maaskofu hawa wapya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.