2016-03-18 08:21:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya Vijana Duniani 2016


Jumapili ya Matawi ni Siku ya Vijana Kijimbo, siku ambayo Maaskofu mahalia wanakutana na vijana wao, tayari kuanza maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Maadhamisho ya Siku ya Vijana Duniani kuanzia mwaka 2014 yameongozwa na Heri za Mlimani, kwanza kabisa, heri walio maskini wa roho, maana ufalme wa mbingu ni wao; heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu na kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka 2016 ni “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Kilele cha maadhimisho haya sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni huko Jimbo kuu la Cracovia, Poland.

Hii ni mara ya pili kwamba, Siku ya Vijana Duniani inakwenda sanjari na Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu, kama ilivyokuwa kunako mwaka 1983 – 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II kwa mara ya kwanza akawakusanya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuadhimisha pamoja, Jumapili ya Matawi na huo ukawa ni mwanzo wa Siku za Vijana Duniani. Kunako mwaka 2000 vijana kutoka katika nchi 165 wakakutana tena mjini Roma ili kuadhimisha Jubilei kuu ya Miaka elfu mbili ya Ukristo, sanjari na Siku ya kumi na tano ya Vijana Duniani.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 anasema, vijana wanatarajiwa kuwasha moto wa huruma ya Mungu huko Cracovia, Poland, mwezi Julai, 2016. Hii itakuwa ni Siku ya Jubilei ya Vijana Duniani; muda uliokubalika wa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani. Jubilei ni kipindi cha kuimarisha mahusiano mema na Mungu, jirani na viumbe sanjari na kufanya matendo ya huruma. Kwa ujio wake, Kristo Yesu anatangaza kwamba, Roho wa Bwana yu juu yake kwani amemtia mafuta ili kuwahubiria maskini Habari njema; wafungwa kufunguliwa kwao na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa. Jubilei inapata maana ya ndani kabisa katika Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo, changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanakiishi kipindi hiki cha neema kwa kujikita katika mambo msingi ya maisha na kuendeleza utume wa Kanisa ambalo linapaswa kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, kauli mbiu inayoongoza Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni “Iweni na huruma kama Baba”. Papa Francisko anachukua fursa hii kufafanua maana ya huruma ya Baba wa mbinguni ambaye ni mwaminifu, mpendelevu kwa watu wake; msamehevu na kwamba, kamwe hawezi kuwasahau watu aliowaumba kwa sura na mfano wake. Upendo wa Mungu kwa namna ya pekee ni aminifu na shirikishi; kumbe, vijana wanahimizwa kuwashirikisha jirani zao upendo huu usiokuwa na mipaka. Hata pale mwanadamu anapokosa na kukengeuka, Mwenyezi Mungu anaendelea kuwa mwaminifu katika pendo lake, kwani anasamehe na kusahau. Katika historia ya maisha ya binadamu, Mwenyezi Mungu amejifunua kuwa daima yupo, aliye karibu, mpaji, mtakatifu na mwenye huruma.

Agano Jipya linaonesha kwamba huruma ya Mungu ni muhtasari wa maisha na utume uliotekelezwa na Kristo Yesu hapa duniani, kwa kuganga na kuponya madhaifu ya binadamu; kwa kuonesha huruma na upendo kwa wahitaji zaidi; kwa kuponya na kusamehe wadhambi. Maisha yote ya Yesu yanaelezea huruma na kwamba, Kristo Yesu ni huruma ya Baba! Mwinjili Luka anazungumzia mfano wa Kondoo aliyepatikana tena; mfano wa shilingi iliyoonekana tena na mfano wa Baba mwenye huruma. Mifano yote hii inashuhudia kwa namna ya pekee, kabisa furaha ya Baba wa mbinguni kwa mdhambi anayetubu; furaha ya Mwenyezi Mungu kwa kusamehe na kusahau hata pale mwanadamu anapokengeuka na kutumia vibaya uhuru wake, lakini kamwe Mwenyezi Mungu hawezi kumtelekeza mja wake. Ni Baba mwaminifu, mpole na mvumilivu, yuko tayari kufanya sherehe pale mdhambi anapotubu na kumwongokea, kielelezo makini cha furaha ya Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kukimbilia ili kuambata huruma ya Mungu katika maisha.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba, huruma ya Mungu inapatikana kwa namna ya pekee katika Sakramenti ya Upatanisho, pale kijana anapoamua kumfungulia Mungu hazina ya moyo wake, tukio linaloleta mabadiliko makubwa katika maisha ya mtu, kwani hapa anaonja huruma ya Mungu inayotolewa na Kanisa kwa njia ya Padre muungamishaji.

Baba Mtakatifu anawahimiza vijana kukimbilia kwenye kiti cha huruma ya Mungu ili kujipatanisha na Mungu, Kanisa na jirani zao, kwani hapa ni mahali muafaka pa huruma ya Mungu inayosamehe. Vijana wanapokutana na Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, anawaangalia kwa jicho la huruma na mapendo na kwamba ameteseka, akafa na kufufuka kwa wafu ili kuwaonjesha huruma ya Baba wa milele! Msalaba wa Vijana uliozinduliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1984 umewasindikiza vijana wengi katika hija ya maisha yao; umekuwa ni changamoto ya toba na wongofu. Msalaba ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa mwanadamu. Hapa ni mahali ambapo mwamini anatambua dhambi zake, tayari kuomba huruma ya Mungu kama ilivyokuwa kwa yule mhalifu aliyeomba msamaha kwa Yesu. Msalaba ni chemchemi ya upendo usiokuwa na mipaka unaotambua na kuthamini maisha ya binadamu, tayari kuanza upya!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016  anawakumbusha vijana kwamba, kuna furaha kubwa ikiwa kama vijana hawa watakuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwani kuna furaha kubwa kutoa kuliko kupokea. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda upeo na hivyo wanapaswa kupendana pia wao kwa wao, kwani Mungu ni upendo! Vijana wanaweza kuwa vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa kupokea Ekaristi Takatifu; kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya maskini; kwa kujisadaka ili kuwasaidia, kuwasikiliza na kuwahudumia kama alivyofanya Mwenyeheri Piergiorgio Frassati.

Kwa maneno mafupi, vijana wanahamasishwa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha yao. Hiki ndicho kipimo ambacho watu watahukumiwa nacho Siku ya mwisho, Yesu anakapokuja kuwahukumu wazima na wafu. Matendo ya huruma ni kiini na utambulisho wa Mkristo kuwa kweli ni mfuasi wa Yesu. Baba Mtakatifu anawahamasisha vijana kujitahidi kumwilisha walau tendo moja katika maisha yao kama sehemu ya maandalizi ya Siku ya Vijana Duniani huko Cracovia. Sala ya Mtakatifu Faustina, mtume wa huruma ya Mungu iwasaidie vijana wa kizazi kipya kuwa na: macho na masikio yenye huruma; ulimi, miguu na mikono yenye huruma na mwishoni moyo wenye huruma, ili kuweza kushiriki katika mateso na mahangaiko ya jirani zao.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kutoa msamaha na kusahau pengine ni kati ya changamoto ngumu sana kuweza kutekelezwa katika maisha ya ujana! Ni vigumu kusamehe lakini bado msamaha ni chombo kilichowekwa kwenye mikono dhaifu ya binadamu ili kuwapatia moyo mkunjufu. Kuondoa hasira, ghadhabu, ukatili na kisasi ili kuishi kwa furaha. Bado kuna changamoto kubwa duniani kutokana na vita na vitendo vya kigaidi. Vijana wawe na ujasiri wa kumwomba Mwenyezi Mungu neema ya kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma kwa wale wanaowatenda mabaya, daima wakijitahidi kuiga mfano wa Kristo Yesu aliyewasamehe watesi wake. Huruma ni njia muafaka ya kushinda ubaya na kwamba, haki na huruma ni chanda na pete, vinakwenda sanjari; mwaliko kwa vijana kuomba huruma ya Mungu katika maisha yao na dunia katika ujumla wake!

Baba Mtakatifu anawakumbusha vijana kwamba, Cracovia ni mahali alipozaliwa Mtakatifu Yohane Paulo II na Mtakatifu Faustina Kowalska; watume mahiri wa huruma ya Mungu kwa nyakati hizi. Maisha na utume wa Mtakatifu Yohane Paulo II unasimikwa kwa namna ya pekee katika huruma ya Mungu kama mfereji wa neema ya Mungu unaomkirimia binadamu amani na furaha ya ndani! Baba Mtakatifu anawaambia vijana kwamba, Yesu anawategemea sana vijana, wasichoke kumkazia macho, ili aweze kuzima kiu ya upendo, amani na furaha ya kweli. Vijana wamtumainie Kristo na kuambata huruma yake, ili nao waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo na sala ili kuganga ubinafsi, chuki na hali ya kukata tamaa inayoendelea kujitokeza duniani. Vijana wawe na ujasiri pamoja na ari ya kuwasha moto wa huruma ya Mungu katika mazingira ya maisha yao ya kila siku, hadi miisho ya dunia. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaweka vijana wote chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.