2016-03-18 14:26:00

Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu: Monsinyo Ayuso & Wells kuwekwa wakfu!


Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 19 Machi, majira ya Saa 4: 00 asubuhi kwa saa za Ulaya anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu atawaweka wakfu Monsinyo Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na Monsinyo Peter Bryan Wells, aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Balozi wa Vatican nchini Afrika ya Kusini, Botswana, Lesotho na Namibia kuwa Maaskofu.

Itakumbukwa kwamba, Monsinyo Guixot, ni Mmissionari wa Shirika la Comboni, aliyezaliwa kunako tarehe 17 Juni 1952 huko Sevila, Hispania. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapadrishwa hapo tarehe 20 Septemba 1980. Tarehe 29 Januari 2016 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu. Monsinyo Wells alizaliwa tarehe 12 Mei 1963 huko Tulsa, Oklahoma, Marekani. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre tarehe 12 Julai 1991. Tarehe 9 Februari 2016 akateuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.