2016-03-18 12:03:00

Hatma ya Zanzibar inategemea: Ukweli, haki na mafao ya wengi!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza katika mahojiano maalum na Radio Vatican kuhusiana na uchaguzi wa marudio Visiwani Zanzibar unaotarajiwa kufanyika Jumapili tarehe 20 Machi 2016 anawataka wananchi pamoja na wadau mbali mbali Visiwani Zanzibar kwanza kabisa kujaliana na kupokeana kwa kutambua kwamba, kwa pamoja ni binadamu wanaounda jumuiya ya watanzania na kwamba wao pia ni raia wa ulimwengu huu.

Dhana hii ikipokelewa kwa dhati inaweza kusaidia kuzika tofauti zao mbali mbali na kuanza kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa ambalo ni hitaji kwa ajili ya amani ya kweli, maendeleo na ustawi wa wote. Bila amani anasema Askofu mkuu Ruwaichi hakuna maendeleo wala utangamano wa kijamii unaowasaidia watu kupokeana kama walivyo na kuunganisha nguvu zao katika kushughulikia maendeleo yao kwa kuzingatia: haki,ukweli na mafao ya wengi.

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi anakaza kusema, mambo haya yanapaswa pia kuzingatiwa na vyama vya kisiasa Visiwani Zanzibar. Vyama hivi kamwe visiwe ni wakala wa kujenga chuki, uhamasama na uchochezi kati ya watu pamoja na mivutano isiyokuwa na tija wala mashiko. Hali tete Visiwani Zanzibar kwa kiasi kikubwa imechangiwa na vyama vyote vya Kisiasa Visiwani humo. Ikumbukwe kwamba, hatima ya Zanzibar inategemea vyama hivi kuzingatia: ukweli, haki, mafao ya wengi, Umoja na mshikamano wa kitaifa kwa ajili ya mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.