2016-03-18 09:13:00

Chagueni viongozi makini kwa ustawi na maendeleo ya wengi!


Baraza la Maaskofu Katoliki Cape Verde linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema nchini humo kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ucahguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini humo, Jumapili tarehe 20 Machi 2016. Wanawataka wananchi kushirikiana na kushikamana katika kutafuta, kulinda na kudumisha mafao ya wengi; kutetea uhuru wa kuabudu; kulinda zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kweli familia ziweze kushuhudia na kutangaza Injili ya familia.

Maaskofu wanasema, huu ni ushauri wa shughuli za kichungaji ili kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu nchini humo. Waamini wanahimizwa kuhakikisha kwamba, wanatumia haki ya kidemokrasia kushiriki katika mchakato wa kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakaosaidia kutoa dira na mwongozo wa maisha. Kura ni wajibu binafsi, lakini waamini na watu wenye mapenzi mema, wanapaswa pia kuongozwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa wanapowajibika kuwachagua viongozi, daima wawachague watu wanaojipambanua kwa kutafuta na kudumisha mafao ya wengi; viongozi watakaosimamia haki msingi za binadamu, kanuni maadili na utu wema!

Wananchi wawe makini kuwachagua viongozi watakaosaidia kuleta chachu ya maboresho katika maisha yao na kamwe wasikubali kununuliwa kwa “vijisenti” vya wanasiasa wanaotaka kuingia madarakani kwa kutumia rushwa na ufisadi. Wananchi wapige kura wakiwa na dhamiri nyofu inayowajibika kimaadili na kijamii, ili kuwapata viongozi watakaoleta maendeleo, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Kamwe wasiwachague viongozi wenye uchu wa mali na madaraka, watu wanaotaka kujitajirisha wenyewe kwa kutumia migongo ya watu maskini.

Maaskofu wanawahimiza wananchi kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa; haki na amani; demokrasia na utawala wa sheria. Katika mchakato huu mzima, hata Wakristo wanao wajibu wa kimaadili na kijamii kuhakikisha kwamba, wanatekeleza haki yao kikatiba kwani kwa kutopiga kura kwa uzembe, ni hatari wa demokrasia. Wananchi waheshimiane na kuthaminiana na kwamba, tofauti zao: kisiasa, kidini na kijamii ni utajiri unaopaswa kukumbatiwa na wala si tatizo na kikwazo katika mafungamano ya kijamii na kisiasa.

Kampeni za uchaguzi mkuu ziendelee kufanyika kwa amani, utulivu na heshima. Viongozi wanaowania madaraka na wapambe wao, waoneshe ukomavu wa kisiasa ili kukuza na kudumisha haki jamii, demokrasia na ushiriki wa wananchi wengi na kamwe asiwepo mwananchi anayebauliwa na kutengwa. Wananchi wawachague viongozi wenye sera makini kuhusu fursa za ajira, kwani hii ni kati ya changamoto kubwa nchini Cape Verde kwa wakati huu. Uhuru wa kidini ni mada tete inayopaswa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa, vinginevyo wananchi wanaweza kujikuta wakitumbukizwa kwenye maafa na majanga ya kujitakia. Haki, amani, umoja na upatanisho wa kitaifa ni mambo msingi, ili kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na kutangaza pamoja na kushuhudia Injili ya familia inayojikita katika upendo wa dhati kati ya bwana na bibi na matunda ya upendo huu ni watoto wanaopaswa kupewa makuzi na malezi bora.

Maaskofu wanawataka waamini na watu wenye mapenzi mema kupima sera za wale wanaogombea uongozi, ikiwa kama zitasaidia kulinda na kudumisha mazingira bora nyumba ya wote sanjari na ekolojia. Utunzaji bora wa mazingira ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa, ili kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Sera za uchumi zitoe kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi; kwa kuwasaidia maskini kupambana na mazingira yao, tayari kushiriki katika mchakato wa maboresho.

Elimu na afya ni maeneo ambayo yanapaswa pia kuanmgaliwa kwa jicho la pekee, ili kweli watu wengi waweze kupata maendeleo ya kweli yanayogusa mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili; kwa kulinda na kutetea haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Maaskofu wanahitimisha ujumbe wao kwa kuwakumbusha wananchi kwamba ushiriki wao katika mchakato wa kupiga kura ni fursa inayowawezesha kukoleza ushirikiano na demokrasia nchini Cape Verde.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.