2016-03-18 14:42:00

Angalieni msimezwe na malimwengu!


Umoja, Utukufu na Ulimwengu ni mambo makuu matatu ambayo yamepewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana kusali na hatimaye kuwatuma wanachama wa Ukatekumeni mpya kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha sehemu mbali mbali za dunia! Tukio hili limefanyika, Ijumaa, tarehe 18 Machi 2016. Baba Mtakatifu anasema, changamoto ya kwanza kwa wale wanaotumwa ni kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha umoja unaojikita katika Injili na Sakramenti za Kanisa.

Waamini watambue kwamba, shetani bado anaendelea kupandikiza mbegu ya utengano kati ya waamini kwa kudhani kwamba wao ni bora na wana karama muhimu zaidi kuliko wengine! Karama kubwa ambayo wanachama wa Ukatekumeni mpya wamepokea ni upyaisho wa Sakramenti ya Ubatizo inayomwilishwa katika maisha, karama ambayo ni neema inayosaidia kukuza na kudumisha umoja. Umoja unahifadhiwa katika hali ya unyenyekevu na utii na kwa njia hii waamini wanakuwa tayari kutumwa kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji mpya!

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Kanisa ni Mama anayetaka kuwaona watoto wake wakiwa ni mashuhuda na vyombo vya umoja ulimwenguni, kwani Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo ameanzisha Kanisa lake. Hapa waamini wanalishwa kwa Neno la uzima; wanasamehewa dhambi zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na pole pole wanaelekezwa kwenda nyumbani kwa Baba wa mbinguni. Kanisa ni Mama anayetoa dira na mweleo kwa watoto wake; anayerithisha maisha kutoka kwa Yesu Kristo.

Umama wa Kanisa unajionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya Utume na maongozi ya wachungaji. Kanisa kama taasisi anasema Baba Mtakatifu linakita mizizi yake kwa Roho Mtakatifu, chemchemi ya maisha mapya. Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kuzima kiu yao ya ndani na maji ya uzima yanayowakirimia upendo, huduma na heshima ndani ya Kanisa; ili Kanisa zima liweze kukua na kukomaa, katika amani na utulivu, ili kuzaa matunda yanayokusudiwa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, neno la pili ambalo angependa kulipatia kipaumbele cha pekee ni Utukufu unaojionesha katika Fumbo la Msalaba; kielelezo cha upendo angavu unaong’aa na kusambaa mbele ya uso wa mwanadamu. Utukufu huu ni tofauti kabisa na utukufu unaotolewa na walimwengu kwani huo, hauna mng’ao unamezwa na sifa za uongo na kweli! Utukufu wa Msalaba unaiwezesha Injili kuzaa matunda yanayokusudiwa na hivyo kumwezesha Mama Kanisa kuwa ni kielelezo cha upendo wa huruma ya Mungu unaovutia na wala hauna shuruti na unazaa matunda kwa wakati wake. Wakristo wanapaswa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Mungu kwa jirani zao. 

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, neno la tatu ambalo angependa kulikazia ni ulimwengu kwa maana Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtuma Mwanaye wa pekee. Kumbe, Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwathamini wa watoto aliowaumba kwa sura na mfano wake, hata kama wakati mwingine wanaokena kuwa mbali sana na Muumba wao.

Waamini wanatumwa kuonesha na kushuhudia uso wa huruma ya Baba wa mbinguni! Wamissionari hawa wapya wawe na ujasiri wa kujitamadunisha; wepesi katika kujifunza lugha mpya pamoja na kuthamini mapokea mahalia, kwani hizi ni dalili za mbegu iliyopandwa na Roho Mtakatifu katika maisha ya watu. Wanatumwa kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika mambo msingi, yaliyo mazuri, makubwa na yenye kuvutia. Huu ni ujumbe ambao unapaswa kufanyiwa rejea ya mara kwa mara, vinginevyo, Mafundisho ya Kikristo yanaweza kukosa dira na mwelekeo katika maisha ya watu. Waamini hawa wa Ukatekumeni mpya wanapaswa Kuinjilisha kama familia kwa kuishi katika umoja na kiasi; kwa kuonesha ushuhuda makini. Kutokana na haya yote, Baba Mtakatifu anawapongeza na kuwatakia heri na baraka katika safari ya maisha yao ya kiroho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.