2016-03-17 17:16:00

Ratiba elekezi ya Papa Francisko nchini Poland!


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuanzia tarehe 27-31 Julai 2016 kufanya hija ya kitume nchini Poland kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya thelathini na moja ya Vijana Duniani itakayoadhimishwa Jimbo kuu la Cracovia, Poland. Ratiba elekezi kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Poland inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Cracovia-Balice, atakutana na kufanya mazungumzo na Rais pamoja na Baraza ya Maaskofu Katoliki Poland. Jioni, akiwa kwenye Makao makuu ya Askofu wa Cracovia, Baba Mtakatifu atasalimiana na vijana, kutoka katika dirisha ambalo Mtakatifu Yohane Paulo II alipenda kulitumia kwa ajili ya kuzungumza na vijana.

Alhamisi tarehe 28 Julai 2016, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Czestochowa na hapo atafanya tafakari na sala ya binafsi na baadaye ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1, 050 tangu Sakramenti ya Ubatizo ilipotolewa kwa mara ya kwanza nchini Poland.

Ijumaa tarehe 29 Julai 2016, Baba Mtakatifu anatarajiwa kutembelea Kambi ya mateso ya Auschwitz-Birkenau na jioni ataongoza Ibada ya Njia ya Msalaba kwenye Uwanda wa Cracovia. Hapa vijana watasali na kuadhimisha Njia ya Msalaba, changamoto na mwaliko kwa vijana kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa jirani zao! Waguswe na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao, tayari kuwashirikisha ile Injili ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Jumamosi, tarehe 30 Julai 2016, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Madhabahu ya Huruma ya Mungu yaliyoko huko Lagiewniki. Hapa Baba Mtakatifu atapitia kwenye Lango la huruma ya Mungu na kuelekea pembeni kidogo mahali alipozikwa Mtakatifu Faustina Kowalska, mtume wa huruma ya Mungu. Hapa ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakleri, Watawa na Majandokasisi. Kama kawaida, Baba Mtakatifu anatarajiwa kushiriki katika kuaungamisha vijana, tayari kwa maadhimisho ya kilele cha Siku ya Vijana Duniani; maadhimisho ambayo yatatanguliwa na mkesha wa sala, tafakari na shuhuda kutoka kwa vijana, jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Asubuhi, Jumapili, tarehe 31 Julai 2016, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu na kuwatuma vijana kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kushuhudia upendo na huruma ya Mungu kwa waja wake. Alasiri, Baba Mtakatifu atafanya mazungumzo na watu wa kujitolea katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016, Kamati kuu pamoja na wafadhili. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko atafunga vilago, tayari kurejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro! Kama kawaida Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega wakati wa maadhimisho haya! Kwa wale wenye haraka zao, wanaweza kuangalia kwenye mtandao wetu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.