2016-03-17 16:18:00

Jubilei zina mguso katika maisha na utamaduni wa watu!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumanne tarehe 15 Machi 2016 amezindua onesho la maadhimisho ya historia ya Jubilei, kama sehemu ya kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki na kama sehemu ya maadhimisho ya mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Onesho hili ni kuanzia mwaka 1300 hadi nyakati hizi na litakuwa wazi kwa mahujaji na watalii wanaofika mjini Roma hadi Mei, Mosi, 2016. Onesho hili ni nyaraka mbali mbali kutoka Senate ya Italia na Maktaba ya Kitume ya Vatican pamoja na Ofisi ya Stamp kutoka Vatican.

Historia ya Kanisa inaonesha kwamba, kunako mwaka 1300 Papa Bonifasi VIII alitoa waraka ili kuitisha maadhimisho ya Jubilei na tangu wakati huo, maadhimisho haya yanaendelea kupamba moto ndani ya Kanisa Katoliki. Kardinali Pietro Parolin katika hotuba yake ya ufunguzi anasema, maadhimisho ya Jubilei yamekuwa na mguso wa pekee katika maisha ya kiroho miongoni mwa Wakristo na yameacha chapa ya kudumu katika historia ya mji wa Roma. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ulioitishwa na kutangazwa na Baba Mtakatifu Francisko ni tukio linaloadhimishwa sehemu mbali mbali za dunia, lakini Roma ina umuhimu wake wa pekee, kwani hapa kuna makaburi ya mashuhuda wa imani, hawa ni akina Mtakatifu Petro na Paulo, miamba wa imani. Roma imekuwa na nafasi ya pekee katika kuandaa na kuadhimisha Jubilei hizi; kwa kutoa nafasi kwa mahujaji na watalii kutembelea maeneo ya kihistoria na kiimani, ili kujichotea wenyewe utajiri unaofumbatwa na mji wa Roma.

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kutumia maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ili kutafakari kwa kina Fumbo la huruma ya Mungu, chemchemi  ya furaha, amani na utulivu wa ndani. Huruma ni dhana inayoweza kusaidia maboresho ya mchakato wa haki; umuhimu wa kutafuta na kudumisha misingi ya amani; matendo ya huruma na mapendo kwa jirani, kama kielelezo cha umwilishaji wa maadhimisho haya. Hii ni fursa ya toba na wongofu wa ndani, ili kuambata huruma na msamaha wa Mungu.

Maadhimisho ya Jubilei yanaliwezesha Kanisa kuendelea kutangaza uwepo endelevu wa Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu, ili kuwakirimia amani inayobubujika kutoka katika Lango la Huruma ya Mungu ambalo ni Kristo Yesu. Haki na huruma ni chanda na pete kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko; kielelezo cha utimilifu wa upendo wa Mungu kwa mwanadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.