2016-03-16 07:51:00

Ziara ya Kardinali Parolin nchini Macedonia na Bulgaria!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 18 - 22 Machi 2016 anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Macedonia na Bulgaria. Atakapowasili mjini Skopje nchini Macedonia, jioni ya tarehe 18 Machi 2016 atakutana na kuzungumza na viongozi wakuu wa Serikali na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Moyo Mtakatifu wa Yesu. Baadaye, atazindua kitabu cha Baba Mtakatifu Francisko, “Jina la Mungu ni huruma” kilichotafsiriwa katika lugha ya Kimacedonia, kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kardinali Parolin, akiwa nchini Macedonia atapata pia fursa ya kuzindua makao makuu ya Askofu wa Jimbo Katoliki la Skopje pamoja na kuzungumza na Wakleri na Watawa pamoja na kutembelea Jumuiya za Kikatoliki huko Strumica zinazoadhimisha Ibada zao kwa kutumia madhehebu ya Kibizantini.

Kardinali Parolin, tarehe 20 Machi 2016 ataanza safari yake ya kikazi nchini Bulgaria. Akiwa mjini Sofia, atatabaruku Kanisa la “Dormitio Mariae” Makao makuu ya waamini wa Kanisa Katoliki wanaotumia madhehebu ya Kibizantini. Baadaye atatembelea  Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane XXIII lililojengwa katika ardhi ambayo ilinunuliwa na Papa ambaye hajulikani hadi wakati huu. Askofu mkuu Angelo Roncalli ambaye baadaye alichaguliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuchagua kuitwa Papa Yohane wa XXIII, wakati huo alikuwa ni mjumbe wa kitume nchini Bulgaria na ndiyo maana Kanisa hili limepewa jina lake kwa heshima hii!

Kardinali Parolin atapata pia fursa ya kutembelea Watawa wa Ekaristi Takatifu pamoja na Kituo cha Tiba cha Mtakatifu Yohane Paulo II, kinachohudumiwa na watawa hawa. Hiki ni kituo cha huduma ya upendo na mshikamano, mahali ambapo maskini, wakimbizi na wahamiaji wanapata tiba. Jumamosi, tarehe, 20 Machi 2016 Kardinali Parolin ataongoza Ibada ya Jumapili ya Matawi katika Kanisa la Mtakatifu Yosefu, mjini Sofia.

Na tarehe 21 Machi 2016, kardinali Pietro Parolin atakutana na kuzungumza na Patriaki Neofit na baadhi ya wajumbe wa Sinodi ya Kanisa la Kiorthodox la Bulgaria kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa majadiliano ya kiekumene. Baadaye atakutana pia na kuzungumza na Rais Rossen Plevneliev, Waziri mkuu Boyko Borissov pamoja na Mufti mkuu Mustafa Hadzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.