2016-03-16 08:55:00

Vipaumbele: Kanisa, Sinodi na Familia!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi katika utangulizi wa kitabu kilichoandikwa na Bwana Maurizio Gronchi kuhusu: Kanisa, Sinodi na Familia na kuchapishwa na kitengo cha Uchapishaji cha Vatican anasema maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Wito na utume wa familia ndani ya kanisa na ulimwengu mamboleo” kilikuwa ni kipindi cha Kanisa kutembea kwa pamoja ili kuwa karibu na familia katika maisha, utume, fursa, changamoto na matatizo yake.

Kitabu hiki kimezinduliwa wakati ambapo Mama Kanisa anasubiri kwa hamu Waraka wa kichungaji kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo. Kwa muda wa miaka miwili anasema Kardinali Baldisseri Kanisa limeivalia njuga Injili ya familia, kwa kuzama katika undani wake, ili kuweza hatimaye, kuzisaidia familia kuwa ni wadau na mashuhuda wa Injili ya familia. Itakumbukwa kwamba, Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1981 alipembua dhana ya familia katika undani wake mintarafu mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusiana na familia, mwelekeo wa kitamaduni, kijamii na kisiasa.

Mwitikio kutoka sehemu mbali mbali za dunia ulikuwa mkubwa na kwamba, kwa miaka miwili, Kanisa kwa mara nyingine tena limeamua kutembea kwa pamoja na mashuhuda wa Injili ya familia, ili kuonesha na kushuhudia upya wa Injili ya familia katika maisha na utume wa Kanisa. Hapa Kanisa limeonesha dhana ya Sinodi na umuhimu wake katika maisha na utume wa Kanisa; kwa kuambata umoja na utofauti, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya ndoa na familia katika maisha na utume wa Kanisa. Dhana ya Sinodi ni wazo lililotolewa na Mwenyeheri Paulo VI, linaloihusisha Familia ya Mungu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Sinodi ndani ya Kanisa Katoliki, alilitaka Kanisa kuanza kumwilisha dhana hii katika maisha ya Makanisa mahalia; Mabaraza ya Maaskofu; Mashirikisho ya Kanda hadi kufikia Kanisa la Kiulimwengu. Katika kipindi cha miaka miwili, Kanisa limepyaisha dhana ya Sinodi kwa kuwa na mbinu mpya iliyowashirikisha Mababa wengi wa Sinodi kwa kutoa nafasi zaidi kwa makundi madogo madogo, yajulikanayo kitaaluma kama “Circuli minori”.

Kardinali Baldisseri anasema, mwandishi wa kitabu hiki amechambua vyema dhana ya Sinodi inayoweza kufupishwa kwa kusema, kweli hii imekuwa ni Injili ya familia, changamoto endelevu inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kutoa kipaumbele cha pekee kwa maisha ya ndoa na familia kama alivyofanya kwa kutoa Katekesi ya kina kwa kipindi cha mwaka mzima, ili kuimarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, tayari familia kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Injili ya familia katika ulimwengu mamboleo.

Lengo ni kushuhudia uzuri, utakatifu na umuhimu maisha ya ndoa na familia katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi anasema Kardinali Baldisseri wameona na kushuhudia matatizo, shida na vikwazo vinavyoendelea kuiandama taasisi ya ndoa na familia, kiasi hata cha kushindwa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Katika mazingira kama haya, Kanisa linaendelea kutangaza na kushuhudia mafundisho tanzu kuhusu ndoa na familia. Kanisa kama alivyokuwa Msamaria mwema, linaendelea kupiga magoti kwa familia zinazoogelea katika bahari ya matatizo na changamoto nyingi, ili kuweza kuganga na kuponya madonda yao, tayari kuambata huruma ya Mungu. Hapa Kanisa linaalikwa anasema Kardinali Baldisseri kuwasindikiza; kufanya mang’amuzi na kuwashirikisha wanandoa katika maisha na utume wa Kanisa.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anasema, kwa sasa Familia ya Mungu inaendelea kusubiri kwa imani na matumaini matunda ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia. Waraka huu utakuwa ni dira na mwongozo wa hija na maisha ya Kanisa la Kiulimwengu. Kardinali anamshukuru Bwana Maurizio Gronchi, mwandishi wa kitabu hiki kuhusu: Kanisa, Sinodi na Familia anayewasaidia wasomaji wake kufanya rejea tena kuhusu maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, ushuhuda wa kipaji cha ugunduzi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, ili kuondoa mashaka na wasi wasi yaliyokuwa yanatanda katika dhana ya ndoa na familia. Kitabu hiki kiwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua na kushuhudia wito na utume wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa binadamu na kwa ajili ya mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.