2016-03-16 16:36:00

Kama mmekomba fedha ya Ukimwi, mtakiona cha moto!


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amekagua Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kagera na kumpa siku tano Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa huo, Bw. Adam Swai amletee taarifa juu matumizi ya sh. Milioni 80 ambazo ni fedha za UKIMWI.  Pia amemtaka ifikapo Machi 20, nwaka huu awasilishe taarifa nyingine ya matumizi ya sh. Milioni 40 za ukarabati wa jengo la wagonjwa maalum (Grade A) Ametoa agizo hilo Jumanne, Machi 15, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa hospitali hiyo baada ya kutembelea maeneo kadhaa yakiwemo wodi ya watoto, wodi ya wazazi, chumba cha wagonjwa mahututi (ICU ) na chumba cha kuhifadhia maiti.

"Kulikuwa na fedha za ukimwi sh. Milioni 80 ambapo kila mtumishi alipaswa kupata sh. 200,000/- lakini ninyi mmewapa sh. 80,000 /-. RAS fedha hizi zimeenda wapi? Nataka uniletee taarifa ofisini kwangu Dar es Salaam ifikapo tarehe 20 mwezi huu," alisema huku akishangiliwa.  "Kwa mujibu wa taarifa ya CAG pale grade A kuna mgogoro wa sh. milioni 40. Wewe taarifa unayo lakini hujaifanyia kazi yoyote. Nataka tarehe 20 nayo hii pia niipate na nione umetoa mapendekezo gani."

Kuhusu tatizo la madaktari katika hospitali hiyo, Waziri Mkuu alisema atawasiliana na Waziri wa Afya ili madaktari watano ambao wanasubiri ajira rasmi lakini wameanza kazi kwa mkataba hospitali hapo wapewe ajira rasmi. Pia alisema amebaini upungufu wa madaktari bingwa uliopo katika hospitali hiyo.  Pia aliahidi kufuatilia maombi yao ya gari la wagonjwa hasa ikizingatiwa kuwa anayo maombi kama hayo kutoka hospitali za Mawenzi (Kilimanjaro), na Ligula (Mtwara).

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwapongeza watumishi wa hospitali hiyo kwa huduma zao nzuri wanazotoa kwa wagonjwa. "Nineridhishwa na kauli walizotoa wagonjwa juu yenu. Tofauti na hospitali nyingine nilizopita, wao wamesema hawajatozwa fedha ili wapatiwe dawa. Nimefarijika sana." "Endeleeni kuwa na huruma kwa wagonjwa. Endeleeni kuwa na lugha nzuri kwa wagonjwa. Hawa wagonjwa hawakuogopa kuelezea hisia zao. Wamesema kwa uwazi kabisa kwamba mnawajali," alisema.

Mapema, akisoma taarifa mbele ya Waziri Mkuu, Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Thomas Rutachunzibwa alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa wa madaktari bingwa pamoja na madaktari wa kawaida.  "Tunao madaktari 10 lakini wanaohitajika ni 30. Tunao madaktari wasaidizi wanane lakini wanaohitajika ni 23 na madaktari bingwa waliopo ni watatu tu lakini wanaohitajika ni 24. Tunaomba tupatiwe watumishi hawa ili tuweze kutoa huduma kulingana na matarajio ya wananchi wetu," alisema. Akifafanua kuhusu mahitaji ya hospitali hiyo, Dk. Rutachunzibwa alisema wanahitaji sh. bilioni 1.8 kwa mwaka bila ya kuweka mishahara ili waweze kufanya kazi yao kwa umakini. "Tunahitaji sh. milioni 802 kwa ajili ya matumizi ya kawaida lakini tunachopokea hivi sasa ni sh. milioni 299 ambayo ni sawa na asilimia 30 ya mahitaji yetu."

"Bajeti ya dawa tuliyotenga ni sh. milioni 960 lakini tunapokea sh. milioni 143 ambazo kiuhalisia zinatosha kwa matumizi ya miezi miwili tu. Tumelazimika kufanya marekebisho ya bei za dawa kwa ridhaa ya Bodi ya hospitali ili tuweze kumudu kutoa huduma kwa wananchi," alisema.  Alisema ili kubana mianya ya upotevu wa mapato, wanahitaji kuwa na kompyuta 15 lakini hadi sasa wamefanikiwa kununua kompyuta mbili tu ambazo ziko Grade A na idara ya wagonjwa wa nje (OPD) ili kuimarisha utaratibu wa ukusanyaji mapato.

SERIKALI KUDHIBITI UAGIZAJI SUKARI – WAZIRI MKUU

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kudhibiti uagizaji wa sukari kutoka nje ili kulinda soko la ndani. Ametoa kauli hiyo Jumatatu, Machi 14, 2016 wakati akizungumza na uongozi wa kiwanda cha sukari cha Kagera pamoja na uongozi wa mkoa wa Kagera alipotembelea kiwanda hicho ambapo alisema wamezuia sukari kutoka nje ili kuhakikisha sukari inaisha katika maghala yao. Akiwa katika siku ya pili ya ziara yake mkoani Kagera, Waziri Mkuu ameviagiza viwanda kuzalisha sukari nchini vizalishe sukari ya kutosha ili kukidhi mahitaji ya soko. Alisema mahitaji halisi ya sukari hapa nchini ni tani 420,000 huku uwezo wa viwanda vya ndani ni kuzalisha tani 300,000 hivyo alitoa wito kwa viwanda hivyo kuongeza uzalishaji. 

"Tunahitaji viwanda vya ndani vizalishe sukari ya kutosha na mahitaji yawe yamefikiwa kama tulivyokubaliana, lengo ni kuzuia uagizaji wa sukari kutoka nje ambao ukiendelea utavivuruga viwanda vya ndani," alisema. Pia alivitaka viwanda hivyo viwe vimefikia malengo ya kuzalisha sukari ya kutosha katika kipindi cha kuanzia miaka mitatu hadi minne kama walivyokubaliana katika kikao cha wadau wa sukari nchini kilichofanyika hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliupongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kufanya uwekezaji mkubwa katika mashamba ya miwa, ununuzi wa mitambo pamoja na kuajiri idadi kubwa ya watumishi ambao ni Watanzania.

Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho, Bw. Ash Rana alisema kwa sasa wanazalisha tani 60,000 za sukari na kwamba wana lengo la kuzalisha tani 120,000 katika kipindi cha miaka minne ijayo. Alisema uzalishaji wa sukari kiwandani hapo umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka ambapo mwaka wa fedha wa 2011/2012 walizalisha tani 35,362 na mwaka 2015/2016 wamezalisha tani 60,000. Ofisa huyo aliiomba Serikali ipunguze riba ya mikopo ya kwenye uwekezaji wa sekta ya kilimo ambapo kwa sasa wanatozwa asilimia 20 kiwango ambacho alisema ni kikubwa sana. Alisema wana mipango ya kukiboresha na kukipanua zaidi kiwanda hicho na hivi sasa wako katika hatua za mwisho za kupata mkopo wa Dola za Marekani milioni 68 ambao kati ya hizo, dola milioni 10 zitapelewa katika uboreshaji wa umwagiliaji na zilizobaki katika kuimarisha miundombinu ya kiwanda hicho.

Na Ofisi ya Waziri mkuu wa Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.