2016-03-15 15:56:00

Mtakatifu mratajiwa: Josè Gabriel wa Rozari Takatifu wa Brochero


Mwenyeheri Josè Gabriel wa Rozari Takatifu wa Brochero alizaliwa kunako tarehe 16 Machi 1840 huko Argentina. Baada ya masomo na majiundo yake akapewa Daraja takatifu la Upadre kunako mwaka 1866. Kunako mwaka 1869 akapewa Uparoko kwenye Parokia ya Mtakatifu Albaerto, hapo akajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maboresho ya maisha ya waamini wake katika medani mbali mbali bila kusahau mahitaji yao ya maisha ya kiroho. Akajichanganya na watu wake katika huduma na maisha, kiasi kwamba, akaambukizwa ugonjwa wa Ukoma. Akarudishwa nyumbani kwao, lakini waamini wake wakamwomba arejee Parokiani mwao na tarehe 26 Januari 1914 akafariki dunia.

Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa ni mtumishi wa Mungu kunako mwaka 2004 na tarehe 14 Septemba 2013 akatangazwa kuwa Mwenyeheri chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko. Tarehe 22 Januari 2015, Baba Mtakatifu akatambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mwenyeheri Josè Gabriel wa Rozari Takatifu.

Baba Mtakatifu Francisko anamtambua Mwenyeheri Josè Gabriel kuwa ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu, aliyenukia harufu ya wanakondoo wake; akawaonjesha huruma na upendo wa Mungu; ni kiongozi aliyejikita katika mambo msingi ya maisha, akamwachia Mungu atende kazi ndani mwake. Ni mfano bora wa kuigwa kwa wagonjwa na wale wenye kiu ya kutaka kukutana na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huyu ni kati ya wenyeheri wanaotarajiwa kutangazwa kuwa watakatifu wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Mwenyeheri Josè Gabriele wa Rozari Takatifu wa Brochero atatangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 16 Oktoba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro Mjini Vatican.

 

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.