2016-03-15 17:03:00

Monsinyo Emmanuel Abbo ateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo la Ngaoundèrè


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Emmanuel Abbo kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Ngaoundèrè nchini Cameroon. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Emmanuel Abbo alikuwa ni Msimamizi wa kitume jimboni humo! Askofu mteule alizaliwa tarehe 17 Julai 1969 huko Mbe, Jimbo Katoliki la Ngaoundèrè. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, mnamo tarehe 14 Juni 2000 akapewa Daraja Takatifu la Upadre, Jimboni Ngaoundèrè, nchini Cameroon.

Tangu wakati huo, amewahi kuwa ni Paroko Msaidizi Kanisa kuu kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2001. Kunako mwaka 2001 hadi mwaka 2004 alipelekwa masomoni kwenye Chuo kikuu cha Kikatoliki cha Yaoundè, Cameroon. Kunako mwaka 2004 hadi mwaka 2008alikuwa ni Katibu mkuu wa Idara ya Elimu Jimboni. Mwaka 2005 hadi mwaka 2015 akateuliwa kuwa Paroko, Mchumi wa Jimbo na Mkurugenzi wa Mashirika ya Kipapa Jimboni. Kunako mwaka 2006 hadi mwaka 2015 alikuwa ni Mkurugenzi wa Caritas Jimboni huko. Kunako mwaka 2010 hadi mwaka 2015 alikuwa ni Mratibu wa uchumi Jimbo na Makamu Askofu. Mwaka 2015 akateuliwa kuwa ni Msimamizi wa Kitume, Jimbo Katoliki Ngaoundèrè. Jimbo hili limekuwa wazi kutokana na kifo cha Askofu Joseph Djida, O.M.I kilichotokea tarehe 6 Januari 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.