2016-03-15 15:49:00

Mama Theresa wa Calcutta!


Mama Theresa wa Calcutta alizaliwa kunako tarehe 26 Agosti 1910 huko Skopje, Macedonia na wazazi wake walikuwa wanatoka Albania. Akiwa na umri wa miaka 18 akajiunga na Shirika la Watawa wa Bikira Maria wa Loreto. Kunako mwaka 1928 akatumwa kwenda Ireland na baada ya mwaka mmoja akatumwa nchini India. Kunako mwaka 1931 akaweka nadhiri zake za kwanza na kupewa jina la Sr. Maria Theresa wa Mtoto Yesu. Kwa muda wa miaka 20 akafundisha historia na jiografia huko Calcutta na huko akakutana na umaskini mkubwa miongoni mwa watu!

Tarehe 10 Septemba 1946 akiwa njiani kuelekea mjini Darjeeling akasikia sauti ikimwambia ndani mwake,”nina kiu” na hivyo akayakumbuka maneno ya Yesu pale Msalabani! Haya ni maneno ambayo yataendelea kuandikwa kwenye nyumba zote zilizoanzishwa na Mama Theresa wa Calcutta, kama muasisi wa Shirika la Wamissionari wa Upendo na huduma ya upendo ni utambulisho na karama yao! Tarehe 16 Agosti 1948 akaondoka kutoka katika Shirika la Bikira Maria wa Loreto, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kunako mwaka 1949 akaungana na baadhi ya wanafunzi wake kuanzisha Shirika Jipya la kitawa kwa ajili ya kuwahudumia maskini kati ya maskini pamoja na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, huku akijitahidi kufuata na kuiga mfano wa Mtakatifu Francisko wa Assisi. Tarehe 7 Oktoba 1950 Shirika lake likatambuliwa rasmi na Kanisa mahalia, wakat iwa maadhimisho ya Siku kuu ya Rozari Takatifu, muhtasari wa Injili.

Mama Theresa wa Calcutta akaliweka Shirika lake chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu sanjari na Moyo Safi wa Maria. Licha ya nadhiri ya usafi wa moyo, ufukara na utii, watawa wa Mama Theresa wa Calcutta wanaweka pia nadhiri ya huduma kwa maskini zaidi. Kunako mwaka 1952 Mama Theresa wa Calcutta akafungua nyumba kwa ajili ya watu waliokuwa kufani na hatimaye, huduma hii ikapanuka kwa ajili ya wagonjwa na watoto yatima. Kunako mwaka 1965 Mwenyeheri Paulo VI akalipatia Shirika la Wamissionari wa Upendo hadhi na haki za Kipapa. Mwaka 1981 tawi la tafakari likaanzishwa kwa ajili ya Mapadre wa Jimbo, huku wakiwa na Ibada kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu.

Sifa na unyenyekevu na huduma makini ya Mama Theresa wa Calcutta ikaenea kwa kasi sehemu mbali mbali za dunia. Kunako mwaka 1979 akatunukiwa Tuzo ya Amani Duniani kwa kutambua mchango wake katika mapambano dhidi ya umaskini na hali ngumu ya maisha . Kutokana na utume wake kwa maskini, akajenga urafiki wa karibu sana na Mtakatifu Yohane Paulo II, kiasi cha kumwezesha kufungua nyumba tatu mjini Roma.

Tarehe 5 Septemba 1997 Mama Theresa wa Calcutta akiwa na umri wa miaka 87 akafariki dunia. Mwezi Julai 1999 mchakato wa kumtangaza kuwa Mwenyeheri ukaanza rasmi kwa ridhaa ya Mtakatifu Yohane Paulo II. Tarehe 19 Oktoba 2003 atakatangazwa kuwa Mwenyeheri na mfano wa Msamaria mwema, aliyethubutu kumwilisha Injili katika huduma ya mapendo kwa Mungu na jirani. Akajitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya wagonjwa, maskini na watoto yatima; huduma iliyorutubishwa kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Tarehe 17 Desemba 2015 Baba Mtakatifu Francisko akatambua muujiza uliotendwa kwa maombezi ya Mama Theresa wa Calcutta na huo ukawa ni mwanzo wa mchakato wa kumtangaza kuwa Mtakatifu.

Mama Theresa wa Calcutta ni shuhuda na chombo cha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini. Watawa wake, wanaendelea kumwilisha matendo ya huruma kiroho na kimwili kwa watu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi hata cha kuyamimina maisha yao kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha sadaka na majitoleo yao kwa maskini, kama ilivyotokea huko Yemen, hivi karibuni. Mama Theresa wa Calcutta atatangazwa kuwa Mtakatifu, Jumapili tarehe 4 Septemba 2016 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.