2016-03-14 06:53:00

Wazee Roma wagawa Injili ya Huruma ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 13 Machi 2016 aliwagawia waamini na mahujaji waliokuwepo Uwanjani hapo Kitabu cha Injili ya Luka, kinachotumika Jumapili katika maadhimisho ya Liturujia ya Neno la Mungu. Kitabu hiki kinaitwa “Injili ya huruma ya Luka” na kwa namna ya pekee, waamini wanaalikwa kuwa na “huruma kama Baba wa mbinguni” kauli mbiu inayooongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatiufu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Watu wanaojitolea kutoka katika Zahanati ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican pamoja na wazee wa mji wa Roma, ndio waliotekeleza dhamana ya kugawa Injili ya huruma ya Luka kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu anakaza kusema, wazee wanayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba wanarithisha imani, maadili na utu wema kwa watoto wao.

Baba Mtakatifu anaendelea kuwahamasisha waamini kuhakikisha kwamba, wanajijengea utamaduni wa kusoma na kulitafakari Neno la Mungu katika maisha yao, ili kweli huruma ya Mungu iweze kukita mizizi yake katika sakafu ya mioyo ya waamini, tayari waamini hawa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku! Kitabu hiki pia kinaonesha matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, walau matendo haya ya huruma wanayafahamu kwa kichwa, tayari kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao! Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, huruma ya Mungu itaweza kutenda kazi ndani mwao! Baba Mtakatifu wakati huu anapofanya kumbu kumbu ya miaka mitatu tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anawaomba tena na tena waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kumwombea katika maisha na utume wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.